33. Sifa na majina ya Allaah yaliyothibiti katika Sunnah III

Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

Dalili kwamba Allaah yuko mbele ya mswalaji

“Anaposimama mmoja wenu katika Swalah, asiteme mate mbele yake wala kuliani kwake, kwani hakika Allaah Yuko mbele Yake. Badala yake [ateme] kushotoni kwake au chini ya mguu wake.”

Allaah yuko juu ya ´Arshi na wakati huo huo yuko mbele ya mwenye kuswali. Hakuna kipingamizi. Hakika Allaah yuko pamoja nasi popote tunapokuwa. Amesema (Ta´ala):

وَهُوَ مَعَكُمْ أَيْنَ مَا كُنتُمْ

“Naye Yu pamoja nanyi popote mlipo.” (57:04)

Dalili ya Allaah kuwa kila mahali kwa ujuzi Wake

“Kiwango bora cha Imani ni wewe ujue kuwa Allaah Yuko pamoja na wewe popote ulipo.”

Yeye yuko pamoja naye kwa ujuzi Wake na wakati huo huo yuko juu ya mbingu kwa dhati Yake (Jalla wa ´Alaa). Yuko juu na wakati huo huo yuko pamoja nasi kwa kutuzunguka kielimu (Jalla wa ´Alaa). Yeye (Subhaanah) yuko juu ya ´Arshi na juu ya viumbe wote na wakati huo huo ujuzi Wake uko kila mahali. Hakuna chochote asichokijua kutokana na ujuzi Wake (Jalla wa ´Alaa). Allaah (Jalla wa ´Alaa) amesema katika kisa cha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akiwa pamoja na as-Swiddiyq (Radhiya Allaahu ´anh) pindi (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliposema ilihali wamo pangano:

لَا تَحْزَنْ إِنَّ اللَّـهَ مَعَنَا

“Usihuzunike, hakika Allaah Yu Pamoja nasi.” (09:40)

Vilevile amesema katika kisa cha Muusa na Haaruun (´alayhimaas-Swalaatu was-Salaam):

قَالَ لَا تَخَافَا ۖ إِنَّنِي مَعَكُمَا أَسْمَعُ وَأَرَىٰ

“Hakika Mimi Niko pamoja nanyi, Nasikia na Naona.” (20:46)

وَاصْبِرُوا ۚ إِنَّ اللَّـهَ مَعَ الصَّابِرِينَ

“Na subirini. Hakika Allaah Yu Pamoja na wanaosubiri.” (08:46)

Huu ni upamaja wa kimaalum na ulioenea:

وَهُوَ مَعَكُمْ أَيْنَ مَا كُنتُمْ

“Naye Yu pamoja nanyi popote mlipo.” (57:04)

Ni wajibu kwa waislamu kuyatambua mambo haya ya kwamba Allaah yuko pamoja na viumbe Wake kwa kuwazunguka kielimu. Kadhalika kwamba yuko pamoja na mawalii Wake kwa kiujuzi, kuwaangalia, kuwahifadhi na kuwajali (Subhaanahu wa Ta´ala) na wakati huo huo yuko juu ya ´Arshi (Subhaanahu wa Ta´ala) na juu ya viumbe wote. Amesema (Ta´ala):

إِنَّ رَبَّكُمُ اللَّـهُ الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ فِي سِتَّةِ أَيَّامٍ ثُمَّ اسْتَوَىٰ عَلَى الْعَرْشِ

“Hakika Mola wenu ni Allaah Ambaye Ameumba mbingu na ardhi katika siku sita kisha akalingana juu ya ´Arshi.” (07:54)

Yeye (Jalla wa ´Alaa) yuko juu ya ´Arshi na ujuzi Wake umeenea kila mahali (Subhaanahu wa Ta´ala).

Ni wajibu kwa kila muislamu ambaye ´ibaadah ni yenye kumuwajibikia kuitakidi ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah ikiwa ni pamoja na kuamini kuwa Allaah yuko juu na amelingana juu ya ´Arshi, hakuna chochote kinachofichikana Kwake na ujuzi Wake umewazunguka waja Wake popote wanapokuwa.

  • Mfasiri: Firqatunnajia.com