1- Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mfano wa kutangamana na mtu mwema ni kama muuza manukato. Asipokupa kitu angalau utapatwa na harufu yake. Mfano wa kutangamana na mtu muovu ni kama muhunzi. Asipounguza nguo zao angalau utapatwa na moshi wake.”

2- Ni wajibu kwa mwenye busara kuacha kutangamana na mpumbavu na mjinga kama ambavyo vilevile anawajibika kutangamana na mtu mwenye akili na mwerevu. Hata kama hatopata akili zake, angalau atachuma mafunzo kutoka kwake. Hata kama hutopata ujinga wa mtu mpumbavu utachafuka kwa kusuhubiana naye.

3- Yaasir bin ´Amr amesema:

“Msuse mpumbavu. Hakuna lililo na kheri kwa mpumbavu isipokuwa kumsusa.”

4- Miongoni mwa sifa za mpumbavu ambazo yule mwenye busara anatakiwa kuzitazama ikiwa haijui hali yake ni kukasirika haraka, kuacha kuthibitisha, kucheka kwa kupindukia, kugeukageuka sana, kuwatusi watu wema na kutangamana na watu waovu.

5- Ukimpa mgongo mpumbavu, anavunjika moyo. Ukitangamana naye, anajiona. Ukiwa mlaini kwake, anakufanyia ujinga. Ukimfanyia ujinga, anakuwa mpole kwako. Ukimfanyia vizuri, anakufanyia vibaya. Ukimfanyia vibaya, anakufanyia vizuri. Ukimfanyia uadilifu, anakudhulumu. Ukimdhulumu, anakufanyia uadilifu.

6- Sa´iyd bin Abiy Ayyuub amesema:

“Usitangamane na mtu muovu. Kwani ni kipande cha moto. Mapenzi yake si ya kweli na wala hatimizi ahadi zake.”

7- Giza ya visa ni upumbavu kama ambavyo akili ndio umaizi wa kisawasawa. Mtu akipewa mtihani wa kutangamana na mpumbavu, basi ahakikishe anashikamana na tabia zake na kujiepusha na za yule mpumbavu. Wakati huohuo amshukuru Allaah sana kwa kumzindua kitu ambacho hakuwapa wengine.

8- al-A´mash amesema:

“Kumnyamazia mpumbavu ndio kumjibu.”

9- Mtu akitiwa katika mtihani kwa kutangamana na mtu sampuli hii, basi wakati mwingine ajifanye kama hakuna kitu. Wakati fulani upole ni kujisalimisha na wakati mwingine ndio nguzo ya busara.

10- Sufyaan ath-Thawriy amesema:

“Mwanaadamu hakuzaliwa isipokuwa mjinga. Vinginevyo asingenufaika kwa maisha yake.”

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Hibbaan al-Bustiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Rawdhat-ul-´Uqalaa’ wa Nuzhat-ul-Fudhwalaa’, uk.
  • Imechapishwa: 02/05/2018