33. Mfano wa aina za ´ibaadah ambazo Allaah ameamrisha

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Mfano wa aina za ´ibaadah ambazo Allaah ameamrisha ni Uislamu, Imani na Ihsaan. Miongoni mwa hizo ni du´aa pia, khofu, matarajio, utegemeaji, shauku [raghbah] na woga [rahbah], unyenyekeaji, tisho, kurejea (Inaabah), kutaka msaada, kutaka kinga, kutaka kuokolewa, kuchinja, kuweka nadhiri na aina nyinginezo zote miongoni mwa aina za ´ibaadah ambazo Allaah ameamrisha. Zote ziwe kwa ajili ya Allaah pekee.

MAELEZO

Baada ya mtunzi (Rahimahu Allaah) kubainisha kwamba ni wajibu kwetu kumuabudu Allaah peke yake asiyekuwa na mshirika, ndipo akabainisha baadhi ya aina za ´ibaadah kama Uislamu, Imani na Ihsaan.

Sampuli tatu hizi, Uislamu, Imani na Ihsaan, ndio dini yenyewe. Imepokelewa na Muslim kutoka katika Hadiyth ya ´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye amesimulia:

“Siku moja tulipokuwa tumekaa na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alitutokea  mtu ambaye  nguo zake zilikuwa nyeupe pepe na nywele zake zilikuwa nyeusi sana. Hakuwa na alama  ya kuonesha kuwa ni msafiri na wala hapakuwa na hata mmoja katika sisi aliyemtambua. Alienda akakaa karibu na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akaweka magoti yake karibu na mago yake na akaweka viganja vyake juu ya mapaja yake.” Akasema: “Ee Muhammad, nieleze kuhusu Uislamu!” Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Uislamu ni kushuhudia kuwa hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na kwamab Muhammad ni Mtume wa Allaah, kusimamisha swalah, kutoa zakaah, kufunga Ramadhaan na kwenda kuhiji ukiweza.”  Akasema: “Umesema kweli.” Tukashangazwa kwa kumuuliza kwake Mtume na kumsadikisha. Kisha akasema: “Nieleze kuhusu imani!”  Akasema: “Ni kumuamini Allaah, Malaika Wake, Vitabu Vyake, Mitume Yake na siku ya Mwisho na  kuamini Qadar; kheri na shari yake.” Akasema: “Umesema kweli!” Akasema: “Nieleze kuhusu Ihsaan!”  Akasema: “Ni kumuabudu Allaah kama vile unamuona. Ikiwa wewe humuoni, basi Yeye anakuona.”  Akasema: “Nieleze kuhusu Qiyaamah.”  Akasema: “Muulizwaji si mjuzi  kama asivyo vilevile muulizaji.” Akasema: “Nieleze kuhusu alama zake!” Akasema: “Kijakazi kumzaa bibi yake na utaona wachunga wanatembea peku, uchi na mafukara wakishindana kujenga majumba marefu.” Amesema: “Kisha akaondoka na tukatulia muda mrefu. Halafu akasema (Swallla Allaahu ´alayhi wa sallam): “Ee ‘Umar! Je, unamjua ni nani yule aliyekuwa akiuliza?” Nikajibu: “Allaah na Mtume Wake ndio wanajua zaidi.”  Akasema Mtume: “Ilikuwa ni Jibriyl ambaye amekuja kuwafundisha Dini yenu.””

Hivyo akafanya (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) mambo haya kuwa ndio dini kwa sababu yameizunguka dini yote.

… na aina nyinginezo zote miongoni mwa aina za ´ibaadah.. – Bi maana aina zote za ´ibaadah zilizotajwa na nyinginezo ni kwa ajili ya Allaah pekee na si mwingine. Kwa hivyo, haijuzu kumfanyia yeyote katika hizo asiyekuwa Allaah (Ta´ala).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 53-54
  • Imechapishwa: 22/05/2020