Allaah (Ta´ala) amesema:

وَلَا تَمُدَّنَّ عَيْنَيْكَ إِلَىٰ مَا مَتَّعْنَا بِهِ أَزْوَاجًا مِّنْهُمْ

“Na wala usikodolee macho yako kwa yale Tuliyowastareheshea baadhi ya watu miongoni mwao.” (20:131)

208- Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakika kila Ummah una mtihani na mtihani wa Ummah wangu ni pesa.”[1]

209- Wanachuoni wetu (Rahimahumu Allaah) wamesema kuwa haya ni maelezo ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) juu ya kwamba kila Ummah ni wenye kupewa mtihani. Kuna waliopewa mtihani kwa masanamu wayakaabudu, kuna waliopewa mtihani kwa jua wakaliabudu, kuna waliopewa mtihani kwa mwezi na nyota, wengine wakapewa mtihani kwa Mtume wao kama mayahudi waliomuabudu ´Uzayr na wakasema kuwa ni mwana wa Allaah, wengine wakapewa mtihani kwa ndama na wakaiabudu, manaswara mtihani kwa ´Iysaa ambapo baadhi wakasema kuwa ni Allaah na wengine wakasema kuwa ni mwana wa Allaah. Ummah huu umepewa mtihani kwa kupenda pesa. Wengi wao wamepitiliza katika kuipenda na ndio maana ´ibaadah zao kwa Allaah zimechafuka.

210- Kwa haya na mfano wake wametumia kama hoja wale wenye wasiyoonelea kuikusanya na kulimbikiza. Wanamaanisha kwamba yote hayo uanapelekea katika ufisadi na yanamzuia mtu na kheri na faida mbalimbali. Hata hivyo hawana hoja yoyote kwa wanayodai. Kwa sababu watu wanatafautiana. Vilevile Hadiyth zifuatazo ni zenye kutoa dalili:

“Ameangamia mja wa dirani! Ameangamia mja wa dirhamu! Ameangamia mja wa Khamiyswah! Ameangamia mja wa kitambaa! Ukimpa ni mwenye kuridhia na usipompa ni mwenye kukasirika. Aangamie! Mwiba wenye kumdunga usimtoke!”

Kisha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema:

“Twuubaa kwa mja anayechukua khatamu ya farasi wake katika njia ya Allaah; nywele zake zako timtim na miguu yake imejaa vumbi. Akilinda analinda kweli na akiandama anaandama kweli. Akiomba idhini haidhinishwi na akishufaia haitikiwi.”[2]

211- Wanachuoni wetu (Rahimahumu Allaah) wamesema kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ametafautisha kati ya mja wa pesa na matamanio na mja wa Mola mtakasifu. Ameomba dhidi ya yule wa kwanza arejee kwa Mola wake na amemsifu huyu wa pili. Mali yenye kumzuia mtu na kumdhukuru Allaah na kutekeleza haki Zake ni mali mbaya. Vinginevyo ni nzuri. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Ni uzuri wa mali iliyoje ilio na mwanaume mwema.”[3]

Lakini ilipokuwa mara nyingi mali ni yenye kuathiri dini na inapelekea katika mitihani na majanga, inatakiwa iwe kidogo na isiwe ni jambo la kupendelea. Ndio maana inatakiwa kwa mtu kuwa na chenye kutosheleza ili kutatua haja na dharurah. Wajuzi wamesema:

“Kila chenye kukushughulisha na Mola wako katika familia na mali ni kibaya kwako.”

212- Yahyaa bin al-Mutawakkil amesema:

“Nilitembea na Sufyaan ath-Thawriy na nikapita karibu na mtu anayejenga nyumba ndefu. Sufyaan akasema: “Usiitazame. Ameijenga ili tu watu waitazame.”

213- Hishaam bin ´Urwah amesema:

“Baba yangu alikuwa anapompitia mtu aliye na kitu katika mapambo ya kidunia anarejea haraka sana nyumbani, anasimama nyuma ya mlango na kuita:

وَلَا تَمُدَّنَّ عَيْنَيْكَ إِلَىٰ مَا مَتَّعْنَا بِهِ أَزْوَاجًا مِّنْهُمْ زَهْرَةَ الْحَيَاةِ الدُّنْيَا

“Na wala usikodolee macho yako kwa yale Tuliyowastareheshea baadhi ya watu miongoni mwao, kwani hayo ni mapambo ya uhai wa dunia tu.” (20:131)

Kisha anaita kwa ajili ya swalah na wanaswali wote.

[1] at-Tirmidhiy (2439) ambaye amesema: ”Hadiyth ni Swahiyh, nzuri na geni.”

[2] al-Bukhaariy (2887).

[3] Ahmad (4/202).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Ahmad al-Qurtwubiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Qam´-ul-Hirsw biz-Zuhd wal-Qanaa´ah, uk. 124-126
  • Imechapishwa: 18/03/2017