Haakim bin Hizaam na ´Utbah bin Rabiy´ah wakajaribu kuwarudisha Quraysh nyuma na kusipowe vita, lakini Abu Jahl akakataa. Badala yake yeye pamoja na ´Utbah wakalidurusu suala hilo na akamuamrisha ndugu wa ´Amr bin al-Hadhwramiy kulipiza kisasi juu ya damu ya nduguye ´Amr. Akavimbisha misuli yake na akapiga ukelele: “´Amr! ´Amr!” Wale wengine wakajazika na vita vikawa kweli.

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akazipanga safu. Kisha akarudi kwenye kibanda yeye pamoja na Abu Bakr. Sa´d bin Mu´aadh na kundi katika Answaar wakasimama kwenye mlango wa kibanda kile wakimlinda Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). ´Utbah bin Rabiy´ah, Shaybah bin Rabiy´ah na al-Waliyd bin ´Utbah wakajitokeza wanaomba mapambano. Waislamu watatu wakawaendea na wote walikuwa wanatokamana na Answaar: ´Awf bin ´Afraa’, Mu´awwidh bin ´Afraa’ na Abdullaah bin Rawaahah. Wakawauliza: “Nyinyi ni kina nani?”Wakajibu: “Ni katika Answaar.”Wakasema: “Watukufu na wakarimu. Sisi tunawataka watoto wa maami zetu.” Badala yake wakapambana na ´Aliy, ´Ubaydah bin al-Haarith na Hamzah (Radhiya Allaahu ´anhum). ´Aliy akamuua al-Waliyd na Hamzah akamuua ´Utbah (imesemekana vilevile Shaybah). ´Ubaydah akakutana na vipigo viwili kutoka kwa wapinzani wake na kila mmoja anapambana na mwenzie. Hamzah na ´Aliy wakamuua kumuua na wakambebea ´Ubaydah ambaye alikuwa amekatwa mguu wake mmoja. Akaendelea kutokwa na damu mpaka akafa katika Swafraa´. Allaah amrehemu na Awe radhi naye. Imepokelewa Swahiyh ya kwamba ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh) alikuwa akionelea kuwa tafsiri ya maneno Yake (Ta´ala):

هَـٰذَانِ خَصْمَانِ اخْتَصَمُوا فِي رَبِّهِمْ ۖ فَالَّذِينَ كَفَرُوا قُطِّعَتْ لَهُمْ ثِيَابٌ مِّن نَّارٍ يُصَبُّ مِن فَوْقِ رُءُوسِهِمُ الْحَمِيمُ

“Hawa ni makhasimu wawili wamekhasimikiana juu ya Mola ao. Kuhusu wale waliokufuru watakatiwa nguo za moto watamwagiwa juu ya vichwa vyao maji yachemkayo.”[1]

ni yale mapambano yao siku ya Badr. Hapana shaka kwamba Aayah hii imeteremka Makkah na vita vya Badr vilikuwa baada ya hapo. Lakini hata hivyo mapambano yao ni katika mifano ya kwanza inayoingia katika maana ya Aayah.

[1] 22:19

  • Mhusika: Imaam Ismaa´iyl bin Kathiyr ad-Dimashqiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Fusuwl fiy Siyrat-ir-Rasuwl, uk. 49-50
  • Imechapishwa: 08/08/2018