33. Mama wa miaka 65 anatokwa na damu baada ya kupatwa na maradhi

Swali 33: Mimi ni mama ambaye nina umri wa miaka sitini na tano na nina muda wa miaka kumi na tisa sijapata mtoto. Hivi sasa anavuja damu kwa kipindi cha miaka tatu ikiwa ni maradhi ambayo kinachodhiri yamemjia katika kipindi hicho. Unamnasihi afanye nini kwa sababu anakabiliwa na swawm?

Jibu: Mwanamke huyu ambaye anavuja damu hukumu yake ni kwamba anatakiwa kuacha kuswali na kufunga kwa muda wa alivyozowea kupata ada yake kabla ya ajali hii iliyompata. Kwa mfano akiwa amezowea kupata ada yake kwa muda wa siku sita mwanzoni mwa kila mwezi basi atakaa mwanzoni mwa kila mwezi muda wa siku sita ambapo hatoswali na hatofunga. Muda huu ukimalizika basi ataoga, ataswali na kufunga.

Namna ya mwanamke huyu na wengine mfano wake ni kwamba anatakiwa kuosha tupu yake vizuri, kuweka kitambara juu yake na atawadhe na ayafanye hayo baada ya kuingia wakati wa swalah ya faradhi. Kadhalika ndivo anavotakiwa kufanya akitaka kuswali swalah iliyopendekezwa katika nyakati zisizokuwa za faradhi. Katika hali hii na kutokana na ule ugumu anaopata inafaa kwake kukusanya kati ya Dhuhr na ´Aswr na Maghrib na ´Ishaa ili kitendo chake hichi kifanye mambo mawili kwa wakati mmoja; Dhuhr na ´Aswr, Maghrib na ´Ishaa. Fajr ataiswali kivyake. Atafanya hivo mara tatu badala ya kufanya mambo hayo mara tano kwa siku.

Narudia tena kwa mara nyingine; pindi anapotaka kufanya twahara basi aoshe tupu yake na ajifunge vizuri kitambara au kitu kingine mfano wake ili kupunguza kile kinachotoka. Baada ya hapo atawadhe na kuswali. Ataswali Dhuhr Rak´ah nne, ´Aswr Rak´ah nne, Maghrib Rak´ah tatu, ´Ishaa Rak´ah nne na Fajr Rak´ah mbili. Kwa msemo mwingine ni kwamba hatofupisha swalah kama wanavofikiria kimakosa baadhi ya wasiokuwa wasomi.  Lakini hata hivyo inafaa kwake kukusanya kati ya swalah mbili; Dhuhr na ´Aswr, Maghrib na ´Ishaa. Dhuhr na ´Aswr anaweza kuziswali wakati wa Dhuhr au wakati wa ´Aswr, na pia Maghrib na ´Ishaa anaweza kuziswali wakati wa Maghrib au wakati wa ´Ishaa. Akitaka kuswali swalah zilizopendekezwa kwa wudhuu´ hakuna ubaya kwake.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: 60 su-aal wa jawaab fiy Ahkaam-il-Haydhw, uk. 30-31
  • Imechapishwa: 30/07/2021