33. Madhara ya kutoacha Qur-aan na Sunnah vikahukumu

Miongoni mwa mambo yanayopasa kutambulika ni kutoacha Qur-aan na Sunnah vikahukumu katika kazi na hali zote ni miongoni mwa mambo yanayosababisha kuzuka madhara na maharibifu kwa kiwango kikubwa. Imaam Ibn-ul-Qayyim (Rahimahu Allaah) ameorodhesha baadhi ya maharibifu na athari hizi zenye kuangamiza. Amefanya vizuri. Allaah amfanyie vizuri. Amesema katika kitabu chake “al-Fawaa-id”:

“Wakati watu walipuuza kuhukumu kwa Qur-aan na Sunnah na kuhukumiwa kwavyo na wakaona kuwa havitoshelezi na wakaenda katika maoni, vipimo, kuyafanya mazuri maoni yao wao na ya wanachuoni wao, kutokana na sababu hizo ndio kukazuka maharibifu katika maumbile yao, giza katika mioyo yao, uchafu katika fahamu zao, upumbavu kwenye akili zao, mambo haya yakaenea na kughilibu kwao mpaka mtoto akakulia na mtumzima akazeekea katika mambo hayo. Matokeo yake hawakuyaona ni maovu. Kipindi kikasonga mpaka ikaja dola ambapo Bid´ah zikasimama mahali pa Sunnah, nafsi mahali pa akili, matamanivu mahali pa mwongozo, upotevu mahali pa uongofu, uovu mahali pa mema, ujinga mahali pa elimu, kujionyesha mahali pa kumtakasia nia Allaah, batili mahali pa haki, uongo mahali pa ukweli, kujikombakomba mahali pa nasaha na dhuluma mahali pa uadilifu. Ikawa mambo haya ndio yametapakaa sehemu kubwa ya nchi na watu wenye mambo haya ndio wenye kunyooshewa kidole. Kabla ya hapo mambo yalikuwa kinyume ambapo watu wa haki ndio walikuwa wakinyooshewa kidole. Ukiona mambo haya yameingia ndani ya nchi fulani, bendera zake zimekwishasimikwa na majeshi yake yameshapanda, basi kwa jina la Allaah kheri tumbo la ardhi kuliko mgongo wake, vilele vya majibali kuliko mabonde na kutangamana na wanyama kuliko kutangamana na watu.”[1]

Kwa hiyo ni lazima wa walinganizi wanaolingania kwa Allaah kulazimiana na Qur-aan na Sunnah katika hali zao zote. Kwa sababu katika kulazimaina na Qur-aan na Sunnah kuna kheri kubwa katika dini na dunia. Kwa ajili hiyo wakati Allaah alipoteremsha maneno Yake:

وَإِن تُبْدُوا مَا فِي أَنفُسِكُمْ أَوْ تُخْفُوهُ يُحَاسِبْكُم بِهِ اللَّـهُ

“Mkidhihirisha yale yaliyomo ndani ya nafsi zenu au mkiyaficha, basi Allaah atakuhesabuni kwayo.”[2]

jambo hilo lilikuwa gumu kwa Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum) ambapo wakamwendea Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kusema:

“Ee Mtume wa Allaah! Tumelazimishwa matendo tunayoyaweza kama mfano wa swaalah, swawm, jihaad na swadaqah. Lakini umeteremshiwa Aayah hii na hatuiwezi. Ndipo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akawaambia:

“Mnataka kusema kama walivosema wale watu wa vitabu viwili kabla yenu: “Tumesikia na tumeasi.” Bali semeni:

“samiina wa atwaana ghurfanaka rabana wa ilaina masir”

Pindi MAswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum) waliposema hivo Allaah akawafanyia wepesi na baada ya hapo akateremsha:

لَا يُكَلِّفُ اللَّـهُ نَفْسًا إِلَّا وُسْعَهَا

”Allaah hakalifishi nafsi yoyote isipokuwa kwa kadiri ya uwezo wake.”[3]

[1] al-Faa-id, uk. 48-49.

[2] 02:284

[3] 02:286 Muslim (125).

  • Mhusika: Shaykh ´Abdus-Salaam bin Barjas
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Usuwl-ud-Da´wah as-Salafiyyah, uk. 78-80
  • Imechapishwa: 19/11/2020