Kwa mujibu wa maoni sahihi zaidi jilbaab (جلباب) ni shuka anayojifunika nayo mwanamke juu ya nguo yake[1] na ambayo mara nyingi hutumiwa wakati anapotoka nyumbani kwake. ´Umm ´Atwiyyah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ametuamrisha kuwatoa katika [´Iyd] al-Fitwr na [´Iyd] al-Adhwhaa´; wanawali, wenye hedhi na wasichana mabikira. Ama wale wenye hedhi watajitenga na swalah.” Mwanamke mmoja akasema: ”Ee Mtume wa Allaah, mmoja wetu hana Jilbaab.” Akasema: “Dada yake ampe moja katika jilbaab zake.”[2]

Shaykh Anwar al-Kashmiyriy amesema alipokuwa anaifanyia maelezo Hadiyth hapo juu:

”Hilo limejulisha kuwa jilbaab inatakikana wakati wa kutoka na kwamba asitoke ikiwa hana jilbaab. Jilbaab ni ile shuka ya juu inayofunika kuanzia kichwani mpaka miguuni. Imekwishatangulia kwamba shungi huvaliwa nyumbani na jilbaab wakati wa kutoka nyumbani. Namna hiyo ndivo nilivofasiri Aayah mbili zinazohusu hijaab:

وَلَا يَضْرِبْنَ بِأَرْجُلِهِنَّ لِيُعْلَمَ مَا يُخْفِينَ مِن زِينَتِهِنَّ

”Na wala wasipige miguu yao [wanapotembea] yajulikane yale wanayoyaficha katika mapambo yao.”[3]

يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ قُل لِّأَزْوَاجِكَ وَبَنَاتِكَ وَنِسَاء الْمُؤْمِنِينَ يُدْنِينَ عَلَيْهِنَّ مِن جَلَابِيبِهِنَّ

“Ee Nabii! Waambie wake zako na mabinti zako – na wanawake wa waumini – wajiteremshie Jilbaab zao.”[4][5]

Amesema tena:

”Ukisema kwamba kujiteremshia jilbaab kunamfanya mtu kutohitaji kujiteremshia shungi juu ya kifua, nasema kuwa kujiteremshia jilbaab ni pale ambapo atatoka nje ya nyumbani kwake kwa sababu ya haja fulani. Kwa hivyo anahitaji kuvaa mtandio katika hali zote.”[6]

Kusema kwamba shungi ni wakati anapokuwa nyumbani ni jambo linahitaji kuangaliwa vyema kwa sababu linaenda kinyume na udhahiri wa Aayah:

وَقُل لِّلْمُؤْمِنَاتِ يَغْضُضْنَ مِنْ أَبْصَارِهِنَّ وَيَحْفَظْنَ فُرُوجَهُنَّ وَلَا يُبْدِينَ زِينَتَهُنَّ إِلَّا مَا ظَهَرَ مِنْهَا ۖ وَلْيَضْرِبْنَ بِخُمُرِهِنَّ عَلَىٰ جُيُوبِهِنَّ

“Na waambie waumini wanawake wainamishe macho yao na wahifadhi tupu zao na wala wasidhihirishe mapambo yao isipokuwa yale yanayodhihirika; hivyo waangushe shungi zao mpaka vifuani mwao.”

mpaka:

وَلَا يَضْرِبْنَ بِأَرْجُلِهِنَّ لِيُعْلَمَ مَا يُخْفِينَ مِن زِينَتِهِنَّ

”Na wala wasipige miguu yao [wanapotembea] yajulikane yale wanayoyaficha katika mapambo yao.”[7]

Makatazo ya kutembea kwa kupiga miguu chini ni kiashirio cha ishara ya wazi juu ya kwamba amri ya kujifunika shungi ni nje ya nyumba pia. Vilevile amesema (Ta´ala):

وَقُل لِّلْمُؤْمِنَاتِ يَغْضُضْنَ مِنْ أَبْصَارِهِنَّ وَيَحْفَظْنَ فُرُوجَهُنَّ وَلَا يُبْدِينَ زِينَتَهُنَّ إِلَّا مَا ظَهَرَ مِنْهَا

“Na waambie waumini wanawake wainamishe macho yao na wahifadhi tupu zao na wala wasidhihirishe mapambo yao isipokuwa yale yanayodhihirika… ”

[1] Haafidhw Ibn Hajar ametaja maoni saba katika ”Fath-ul-Baariy” ambapo hii ni moja katika maoni hayo. al-Baghawiy amethibitisha maoni hayohayo na akasema:

”Ni shuka ya juu ambayo mwanamke anaitumia juu ya nguo na mtandio wake.” (Ma´aalim-ut-Tanziyl (3/544))

Ibn Hazm amesema:

”Kwa mujibu wa kiarabu ambacho Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ametuzungumzisha nacho jilbaab ni ile inayofunika mwili mzima na si baadhi yake tu.” (al-Muhallaa (3/217))

al-Qurtwubiy amesahihisha maoni hayo katika ”al-Jamiy´ li Ahkaam-il-Qur-aan”. Ibn Kathiyr amesema:

”Jilbaab ni shuka ya juu inayovaliwa juu ya shungi.” (Tafsiyr al-Qur-aan al-´Adhwiym (3/517))

Pengine ndio zile abaya zinazotumiwa na wanawake wa Najd, ´Iraaq na kwenginepo.

[2] al-Bukhaariy, Muslim na wengineo.

[3] 24:31

[4] 33:9

[5] Faydhw-ul-Baariy (1/388).

[6] Faydhw-ul-Baariy (1/256).

[7] 24:31

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Jilbaab-ul-Mar-ah al-Muslimah, uk. 83-84
  • Imechapishwa: 18/09/2023