Allaah amefaradhisha kifo juu ya kila nafsi na akajifanyia Yeye pekee (Subhaanah) ndiye Mwenye kubaki. Amesema (Ta´ala):

كُلُّ مَنْ عَلَيْهَا فَانٍ وَيَبْقَىٰ وَجْهُ رَبِّكَ ذُو الْجَلَالِ وَالْإِكْرَامِ

“Kila aliyekuwa juu yake [ardhi] ni mwenye kutoweka na utabakia uso wa Mola wako wenye utukufu na ukarimu.”[1]

Inapokuja katika suala la jeneza akawahusu wana wa Aadam kwa hukumu ambazo ni lazima kwa wale waliohai kuzitekeleza. Katika sura hii tutataja yale ambayo ni maalum kwa wanawake ikiwa ni pamoja na yafuatayo:

1 – Ni wajibu kwa wanawake ndio wasimamie jambo la kumuosha yule maiti mwanamke. Haijuzu kwa wanaume kumuosha mwanamke isipokuwa mume ndiye ambaye inafaa kwake kumuosha mke wake. Vievile maiti ya kiume inatakiwa kusimamiwa suala la kuoshwa na wanaume isipokuwa mke ndiye ambaye inafaa kwake kumuosha mume wake. Kwa sababu ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh) alimwosha mke wake Faatwimah, msichana wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na (Radhiya Allaahu ´anhaa). Vilevile Asmaa´ bint ´Umays (Radhiya Allaahu ´anhaa) alimuosha mume wake Abu Bakr as-Swiddiyq (Radhiya Allaahu ´anh).

2 – Ni Sunnah kumtia sanda mwanamke kwa nguo tano nyeupe:

a) Nguo ya chini anayofungwa nayo.

b) Mtandio juu ya kichwa chake.

c) Kanzu anayoivaa.

d) Nguo mbili anazofungwa nazo juu ya hizo.

Laylaa ath-Thaqafiyyah amesema:

“Nilikuwa katika waliomuosha Umm Kulthuum, msichana wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipofariki. Kitu cha kwanza alichotupa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ilikuwa ni nguo ya chini, kisha dera, kisha mtandio, nguo ya juu kisha akafungwafungwa kwa nguo nyingine.”

Ameipokea Ahmad na Abu Daawuud.

Imaam ash-Shawkaaniy amesema katika “Nayl-ul-Awtwaar”:

“Hadiyth inafahamisha kwamba imesuniwa juu ya sanda ya mwanamke iwe nguo ya chini, dera, mtandio na nguo ya juu na nguo anayozungushiwa.”[2]

[1] 55:26-27

[2] (04/42).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tanbiyhaat, uk. 67-68
  • Imechapishwa: 05/11/2019