32. Ulazima wa kulala na nia


Ni lazima kwa muislamu kuweka nia wakati wa usiku juu ya swawm ya lazima. Mfano wa funga hizo ni funga ya Ramadhaan, funga ya kafara na swawm ya nadhiri. Hilo linakuwa kwa yeye kuitakidi kuwa anafunga Ramadhaan, kulipa deni lake, swawm ya nadhiri au kafara. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hakika si vyenginevyo kila kitendo kinategemea na nia na kila mmoja atalipwa kwa lile alilonuia.”

´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ameeleza kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliyesema:

“Hakika yule ambaye hakulaza nia kabla ya kuchomoza alfajiri basi hana funga.”[1]

Kwa hiyo ni lazima juu ya funga ya wajibu kunuia wakati wa usiku.

Ambaye ataweka nia wakati wa mchana (kama mfano wa ambaye ataamka asubuhi na asipate chakula chochote baada ya kuchomoza kwa alfajiri kisha matokeo yake akanuia), basi haitoshi isipokuwa kama ni funga iliyopendekezwa. Kuhusu swawm ambayo ni ya lazima haifunguki nia wakati wa mchana. Kwani wakati wote wa mchana ni lazima kwa mtu kufunga na nia haifunguki juu ya kitu kilichokwishapita.

Kuhusu funga iliyopendekezwa inafaa kuweka nia wakati wa mchana. ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ameeleza:

“Siku moja Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliingia ambapo akasema: “Je, mna chochote?” Tukasema: “Hapana.” Ndipo akasema: “Basi mimi nimefunga.”

Wameipokea kikosi cha wanachuoni isipokuwa al-Bukhaariy[2].

Katika Hadiyth kuna faida kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa mwenye kula kwa sababu aliomba chakula. Pia kuna dalili nyingine ya kufaa kuchelewesha nia ya funga ikiwa ni swawm iliyopendekezwa. Kwa hiyo inafanywa kuwa maalum kutokana na zile dalili zinazokataza.

Sharti ya kusihi funga iliyopendekezwa kwa kuweka nia kipindi cha mchana ni kwamba kusipatikane kabla ya nia hiyo kitu kinachopingana na swawm kama mfano wa kula, kunywa, jimaa na mfano wa hivyo. Akifanya moja katika vitu vinavyomfunguza basi swawm yake haitosihi kwa maafikiano.

[1] an-Nasaa´iy (2340).

[2] Abu Daawuud (2454), at-Tirmidhiy (729), an-Nasaa´iy (2330) na Ibn Maajah (1700).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Mulakhasw al-Fiqh (01/393)
  • Imechapishwa: 03/05/2021