32. Sifa na majina ya Allaah yaliyothibiti katika Sunnah II

Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema:

Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa salam):

“Hakuna yeyote katika nyinyi isipokuwa Mola Wake Atamsemeza. Kutakuwa hakuna baina yake na baina Yake mwenye kutarjumu.”[1]

Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuhusu Ruqyah ya mgonjwa:

“Mola Wetu ni Allaah Ambaye Yuko juu ya mbingu, Limetakasika Jina Lako. Amri Yako iko mbinguni na ardhini. Teremsha Rahmah yako katika ardhi kama jinsi Rahmah Yako iko mbinguni. Tusamehe madhambi yetu makubwa na madogo. Wewe ni Mola wa wazuri. Teremsha Rahmah katika Rahmah Yako na dawa katika Dawa Yako kwa huyu mwenye maumivu.”[2]

Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Je, hamniamini na mimi nimeaminiwa na Aliye juu ya mbingu?”[3]

“… na ´Arshi iko juu ya maji, na Allaah Yuko juu ya ´Arshi, Naye Anajua yale mliyomo.”[4]

Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kumwambia kijakazi:

“Yuko wapi Allaah?” Akasema: “Mbinguni.” Kisha akamuuliza: “Mimi ni nani?” Akasema: “Wewe ni Mtume wa Allaah.” Akasema: “Muache huru, hakika ni muumini.”[5]

“Kiwango bora cha Imani ni wewe ujue kuwa Allaah Yuko pamoja na wewe popote ulipo.”[6]

“Anaposimama mmoja wenu katika Swalah, asiteme mate mbele yake wala kuliani kwake, kwani hakika Allaah Yuko mbele Yake. Badala yake [ateme] kushotoni kwake au chini ya mguu wake.”[7]

MAELEZO

Hizi ni sehemu ya Hadiyth ambazo zimepokelewa kuhusu sifa. Baadhi ya sifa hizi zimekwishatangulia. Lengo la mwandishi (Rahimahu Allaah) ni kutaja sehemu katika Aayah na Hadiyth zilizothibiti kuhusu sifa ili muislamu apate kujua yaliyoko nyuma yake. Ametaja jumla ya Aayah na Hadiyth zilizothibiti kuhusu majina na sifa za Allaah na kwamba Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah wanaamini yale mambo yanayotolewa dalili na majina na sifa hizo. Wanazipitisha kama zilivyokuja pasi na kuzipotosha, kuzikanusha, kuzifanyia namna na kuzilinganisha. Ahl-us-Sunnah hawazipingi kama wanavyofanya Jahmiyyah na Mu´tazilah. Hawazifasiri kwa kupindisha maana kama wanavyofanya baadhi ya Maaturiydiyyah, Ashaa´irah na wengineo. Wanazipitisha kama zilivyokuja. Sambamba na hilo wanaziamini, wanazithibitisha na wanaitakidi yale yenye kufahamishwa na majina na sifa hizo na wakati huo huo wanamtakasa Allaah kufanana na viumbe Wake. Ahl-us-Sunnah hawaonelei ukanushaji wala ufananizi. Ni Ayaah na Hadiyth vilivyothibiti na maana yake ni sahihi. Ndani yavyo hamna ufananizi, ushabihishaji wala ukanushaji. Miongoni mwazo ni maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhiwa salam):

Dalili ya Kuzungumza kwa Allaah

“Hakuna yeyote katika nyinyi isipokuwa Mola Wake Atamsemeza. Kutakuwa hakuna baina yake na baina Yake mwenye kutarjumu… “

Bi maana mkati kati.

“Atazame kuliani mwake asione jengine isipokuwa yale aliyoyatanguliza, kushotoni mwake asione jengine isipokuwa yale aliyoyatanguliza na atazame mbele yake asione jengine isipokuwa Moto ukimkabili. Hivyo basi, uogopeni Moto ijapokuwa kwa kipande cha tende. Asiyekipata basi angalau [azungumze] neno zuri.”

Hii ni dalili yenye kuonyesha kuwa kuzungumzishwa itakuwa kwa watu wote siku ya Qiyaamah.

“Hakuna yeyote katika nyinyi isipokuwa Mola Wake Atamsemeza… “

Lakini hata hivyo waovu watazungumzishwa kwa maneno yenye kuwadhuru na ya kuwaghadhibikia. Upande mwingine wema watazungumzishwa kwa maneno yenye kuwafurahisha.

Dalili ya kwamba Allaah yuko juu

Amesema (´alayhis-Swalaatu was-Salaam):

“Je, hamniamini na mimi nimeaminiwa na Aliye juu ya mbingu?”[8]

Bi maana yuko juu.

“Mola Wetu ni Allaah Ambaye Yuko juu ya mbingu, Limetakasika Jina Lako. Amri Yako iko mbinguni… “

Bi maana iko juu.

“Mola Wetu ni Allaah Ambaye Yuko juu ya mbingu, Limetakasika Jina Lako.”

Bi maana juu.

“Teremsha Rahmah yako… “

Hii ni dalili yenye kuonyesha Ujuu.

Maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“´Arshi iko juu ya maji, na Allaah Yuko juu ya ´Arshi, Naye Anajua yale mliyomo.”

Haya ni kama mfano wa yale yaliyotangulia katika Kauli Yake (Ta´ala):

الرَّحْمَـٰنُ عَلَى الْعَرْشِ اسْتَوَىٰ

Mwingi wa Rahmah amelingana juu ya ´Arshi.” (20:05)

[1] al-Bukhaariy (7443) na Muslim (1016)

[2] Abuu Daawuud (3892), an-Nasaa´iy (10876), al-Haakim (1/344) na (3/218) na wengine.

[3] al-Bukhaariy (4351) na Muslim (1064).

[4] Abuu Daawuud (3451). Imaam al-Albaaniy (Rahimahu Allaah) kasema kuwa ni dhaifu katika kitabu cha Ibn Abiy ´Aasim ”Kitaab-us-Sunnah” (577).

[5] Muslim (537).

[6] Abuu Nu´aym (6/124). Katika isnadi kuna udhaifu. Katika isnadi kumekuja Nu´aym bin Hamaad. Imaam al-Albaaniy (Rahimahu Allaah) kasema kuwa ni mdhaifu katika ”Dhwa´iyf al-Jaami´ as-Swaghiyr” (1100).

[7] al-Bukhaariy (406) na Muslim (547).

[8] al-Bukhaariy (4351) na Muslim (1064).

 

  • Mfasiri: Firqatunnajia.com