Shaykh-ul-Islaam na Imaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Sharti ya tisa ni nia na mahala pale ni moyoni. Kuitamka ni Bid´ah. Dalili ni Hadiyth:

“Matendo huzingatiwa kwa nia. Kila mmoja atalipwa kutokana na kile alichonuia.”[1]

MAELEZO

Nia ni sharti ya kusihi kwa swalah. Bali ni sharti ya ´ibaadah zote. Matendo hayasihi pasi na nia. Nia ni lile kusudio. Kusudio la kufanya ´ibaadah. Ni lazima ukusudie ´ibaadah. Iwapo mtu atatawadha ambapo akaosha uso, mikono, akafuta kichwa na akaosha miguu na asinuie kutia wudhuu´ bali amenuia kujitia baridi kidogo, basi haitosihi kwa kukosekana kwa nia. Iwapo mtu ambaye yuko na janaba ataoga na asikusudie kuondosha hadathi bali amekusudia kujitia baridi kidogo, basi janaba haitoondoka. Janaba yake ni yenye kubaki kwa sababu ya kukosekana kwa nia. Akifanya yale yanayofanywa katika swalah lakini pasi na nia bali alichokusudia ni kujitia baridi mwili wake, basi swalah yake haitosihi kwa sababu ya kukosekana kwa nia. Endapo atatoa mali yake na asikusudie zakaah basi haitokuwa zakaah. Aidha kama amekusudia swadaqah ya kawaida haitokuwa zakaah mpaka anuie kuwa ni zakaah.

Maneno yake:

“Mahala pale ni moyoni.”

Sehemu ya nia ni moyoni.

Maneno yake:

“Kuitamka ni Bid´ah.”

Hakuna haja ya kuitamka.

Yale yanayofanywa na baadhi ya watu ambapo wanatamka nia mfano wa kusema:

“Nimenuia kuswali swalah ya Fajr nyuma ya imamu huyu Rak´ah mbili.”

“Nimenuia kufunga kuanzia kuzama kwa jua la alfajiri mpaka jua kuzama katika Ramadhaan.”

yote haya ni uzushi. Hayana msingi wowote. Hayana dalili. Shaykh-ul-Islaam bin Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema:

“Yale yote yaliyozuliwa na watu kama mfano wa kuitamka nia kabla ya kuanza kuswali, kabla ya Talbiyah, kabla ya kutawadha na ´ibaadah nyenginezo ni jambo la kizushi ambalo halikusuniwa na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Bali Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akidumu juu ya ´ibaadah hali ya kuacha kufanya hivo. Kwa hiyo kufanya na kudumu juu ya jambo hilo ni Bid´ah na upotevu.”[2]

Dalili ni Hadiyth – Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim kupitia kwa ´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anh).

[1] al-Bukhaariy (1) na Muslim (1907).

[2] Majmuu´-ul-Fataawaa (22/223).

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Shuruwt-is-Swalaah, uk. 49-51
  • Imechapishwa: 30/12/2021