32. Qur-aan itarudi kwa Allaah


Mtunzi wa kitabu amesema:

“… Kwake ndiko itarudi.”

Anaashiria yatayokuwa katika zama za mwisho wakati itaponyanyuliwa Qur-aan na ifutwe kutoka vifuani na kutoka kwenye misahafu. Hakutobaki athari yake kabisa. Hiyo ni miongoni mwa alama za Qiyaamah. Kama ambavyo imeteremshwa kutoka Kwake kadhalika katika zama za mwisho itanyanyuliwa na kurudi Kwake (Subhaanahu wa Ta´ala). Ardhini hakutobaki Qur-aan[1]. Maneno yake:

“Amezungumza kwayo kihakika.”

ni Radd kwa wale wanaosema kuwa amezungumza kwayo kimafumbo. Kuegemezwa kwa Allaah ni kwa njia ya mafumbo. Kwa sababu Yeye ndiye ameiumba na hivyo inaegemezwa Kwake kimafumbo. Wala sio maana iliyosimama kwenye nafsi Yake, kama wanavoonelea Ashaa´irah. Wala haikuumbwa, kama wanavoonelea Jahmiyyah. Ni maneno ya Allaah kikweli. Jibriyl amesikia kutoka Kwake na akayapokea kutoka kwa Allaah (Jalla wa ´Alaa) na akamfikishia nayo Mtume Wake Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kwa hiyo Qur-aan ni kutoka kwa Muhammad, kutoka kwa Jibriyl, kutoka kwa Allaah (Jalla wa ´Alaa). Hii ndio mrorongo wa Qur-aan. Amesema (Subhaanahu wa Ta´ala):

إِنَّهُ لَقَوْلُ رَسُولٍ كَرِيمٍ ذِي قُوَّةٍ عِندَ ذِي الْعَرْشِ مَكِينٍ مُطَاعٍ ثَمَّ أَمِينٍ

“Hakika bila ya shaka hii ni kauli ya Mjumbe mtukufu, Mwenye nguvu na mwenye cheo kwa huyo Mwenye ´Arshi, anayetiiwa, tena muaminifu!”

Haya yote yanamuhusu Jibriyl. Kisha akasema:

وَمَا صَاحِبُكُم

“Na wala huyu mwenzenu… “

Bi maana Muhammad.

وَمَا صَاحِبُكُم بِمَجْنُونٍ

“Na wala huyu mwenzenu hana wazimu.”

Kama wanavosema makafiri.

وَلَقَدْ رَآهُ

”Na hakika yeye alimwona… “

Bi maana alimuona Jibriyl katika umbile lake la kikweli la ki-Malaika:

وَلَقَدْ رَآهُ بِالْأُفُقِ الْمُبِينِ

”Na hakika yeye alimwona kwenye upeo wa macho uliosafi.”[2]

Alimuona Jibriyl akiwa juu katika umbile lake katika upeo wa Makkah. Mara nyingine alimuona usiku wa kupandishwa mbinguni kwenye mkunazi:

وَلَقَدْ رَآهُ نَزْلَةً أُخْرَىٰ

“Na kwa hakika amemuona katika uteremko mwingine.”[3]

Bi maana alimuona Jibriyl kwenye mkunazi usiku wa kupandishwa mbinguni. Kwa hiyo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimuona Jibriyl katika umbile lake la ki-Malaika mara mbili. Mbali na mara hizo alikuwa akimjia katika umbile la mtu na Maswahabah zake wakimuona katika umbile la mtu na wakidhani kuwa ni katika watu na kwamba ni mjumbe aliyekuja kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)[4].

[1] Tazama ”Sunan Sa´iyd bin Mansuur” (02/335 nambari. 97).

[2] 81:19-23

[3] 53:13

[4] Tazama ”Swahiyh-ul-Muslim” (08).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh ´Aqiydat-il-Imaam Mujaddid Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab, uk. 52-53
  • Imechapishwa: 17/03/2021