Tutapoangalia mwongozo wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) basi tutaona kuwa mfumo wake ni kwamba siku moja aliingia mtu msikitini siku ya ijumaa wakati ambao Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa anatoa Khutbah ambapo mwanaume yule akakaa chini. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema:

“Je, umeswali?” Akajibu: “Hapana.” Akasema: “Basi simama uswali Rak´ah mbili.”

Hapana shaka ni jambo linalojulikana kwamba kuswali Rak´ah mbili wakati mtu anapoingia msikitini ni katika mambo mema. Lakini hata hivyo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakumwamrisha kufanya hivo papo kwa hapo mpaka kwanza alipohakikisha kuwa hakufanya. Wewe unaweza kumwamrisha mtu kufanya kitu ambapo tayari ameshakifanya. Hivyo unakuwa umefanya haraka, kutothibitisha na kupunguza hadhi yako. Lakini unachotakiwa kufanya ni wewe kuhakikisha kwanza, ikiwa hakufanya ndio umwamrishe.

Kadhalika inapohusiana na maovu wapo watu ambao wanaweza kumkataza kitu ambacho wao wanaona kuwa ni maovu ilihali sio maovu. Mfano wa hilo mtu amemuona mtu mwengine anaswali swalah ya faradhi hali ya kukaa chini ambapo akamkataza na kwamba hana haki yoyote ya kuswali kwa kuketi chini, kufanya hivi sio sawa. Lakini unachotakiwa ni wewe kuuliza kwanza ni kwa nini ameswali kwa kukaa chini. Pengine yuko na udhuru katika kuketi kwake chini na wewe hujui. Matokeo yake unakuwa ni mwenye kukurupuka na kuipunguza hadhi yako.

Kuna kitu kingine ambacho pia ni cha lazima: unatakiwa kuijua hukumu ya Shari´ah. Vilevile unatakiwa uijue hali ya yule mwamrishwaji na mkatazwaji ili uwe juu ya elimu katika jambo lako.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Manhaj Ahl-is-Sunnah wal-Jamaa´ah fiy-´Aqiydah wal-´Amal, uk. 43-44
  • Imechapishwa: 26/08/2019