Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Dalili ya Shahaadah ni Kauli Yake (Ta´ala):

شَهِدَ اللَّـهُ أَنَّهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ وَالْمَلَائِكَةُ وَأُولُو الْعِلْمِ قَائِمًا بِالْقِسْطِ ۚ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ

“Allaah ameshuhudia kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Yeye, Malaika na wenye elimu [pia wameshuhudia], ni Mwenye kusimamisha kwa uadilifu. Hapana mungu wa haki isipokuwa Yeye, Mwenye nguvu kabisa, Mwenye hekima.” (Aal ´Imraan 03:18)

Maana yake ni kwamba hapana mwenye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Allaah. “Hapana mungu” ni kukanusha kila kinachoabudiwa badala ya Allaah, wakati “isipokuwa Allaah” ni kuthibitisha ya kwamba ´ibaadah afanyiwa Allaah Pekee. Hana mshirika katika ´ibaadah Yake, kama ambavyo Hana mshirika katika Ufalma Wake. Tafsiri inayoweka wazi haya, ni Kauli Yake (Ta´ala):

وَإِذْ قَالَ إِبْرَاهِيمُ لِأَبِيهِ وَقَوْمِهِ إِنَّنِي بَرَاءٌ مِّمَّا تَعْبُدُونَ إِلَّا الَّذِي فَطَرَنِي فَإِنَّهُ سَيَهْدِينِ وَجَعَلَهَا كَلِمَةً بَاقِيَةً فِي عَقِبِهِ لَعَلَّهُمْ يَرْجِعُونَ

“Pindi Ibraahiym alipomwambia baba yake na watu wake: “Hakika mimi najitenga mbali na yale mnayoyaabudu, isipokuwa Yule aliyeniumba, basi hakika Yeye Ataniongoa! Na akalifanya neno hili kuwa ni lenye kubakia katika kizazi chake ili wapate kurejea.” (az-Zukhruf 43:26-28)

Na Kauli Yake (Ta´ala):

قُلْ يَا أَهْلَ الْكِتَابِ تَعَالَوْا إِلَىٰ كَلِمَةٍ سَوَاءٍ بَيْنَنَا وَبَيْنَكُمْ أَلَّا نَعْبُدَ إِلَّا اللَّـهَ وَلَا نُشْرِكَ بِهِ شَيْئًا وَلَا يَتَّخِذَ بَعْضُنَا بَعْضًا أَرْبَابًا مِّن دُونِ اللَّـهِ ۚ فَإِن تَوَلَّوْا فَقُولُوا اشْهَدُوا بِأَنَّا مُسْلِمُونَ

“Sema: “Enyi watu wa Kitabu! Njooni katika neno lililo sawa baina yetu na baina yenu – kwamba tusiabudu yeyote isipokuwa Allaah Pekee wala tusimshirikishe Yeye na chochote wala wasiwafanye baadhi yetu wengine kuwa ni waungu badala ya Allaah.” Wakikengeuka; basi semeni: “Shuhudieni kwamba sisi ni waislamu.” (Aal ´Imraan 03:64)

MAELEZO

Nguzo ya kwanza ya Uislamu ni kushuhudia ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah. Kwayo mja anaingia katika Uislamu. Ashuhudie ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah. Maana yake hakuna mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah. Shahaadah ina kukanusha na kuthibitisha. Kunakanusha ya kwamba hapana mungu anayeabudiwa kwa haki isipokuwa Allaah na kuthibitisha ya kuwa Allaah pekee ndiye mwenye haki ya kuabudiwa. Allaah (Ta´ala) amesema:

إِيَّاكَ نَعْبُدُ وَإِيَّاكَ نَسْتَعِينُ

“Wewe pekee ndiye tunakuabudu na Wewe pekee ndiye tunakuomba msaada.” (01:05)

وَمَا أُمِرُوا إِلَّا لِيَعْبُدُوا اللَّـهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ

“Hawakuamrishwa jengine isipokuwa wamwabudu Allaah kwa imani safi kabisa na ya asli hali ya kumtakasia Yeye dini.” (98:05)

ذَٰلِكَ بِأَنَّ اللَّـهَ هُوَ الْحَقُّ وَأَنَّ مَا يَدْعُونَ مِن دُونِهِ هُوَ الْبَاطِلُ وَأَنَّ اللَّـهَ هُوَ الْعَلِيُّ الْكَبِيرُ

“Hivyo ni kwa kuwa Allaah ndiye wa haki na kwamba vile wanavyoomba badala Yake ndio batili na kwamba Allaah ndiye Aliye juu, Mkubwa.” (22:62)

Shahaadah pasi na matendo haina maana yoyote. Hakunufaishi kitu kusema ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah endapo mtu hatomtakasia Allaah ´ibaadah. Shahaadah kama hii hainufaishi kitu. Wanafiki wanatamka shahaadah pasi na kuiamini na ndio maana wako katika tabaka la chini kabisa Motoni. Yule mwenye kusema kuwa hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na anaabudu makaburi na masanamu shahaadah haitomfaa kitu, kwa kuwa ni batili.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 40-41
  • Imechapishwa: 09/01/2017