Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) amesema:

Inatakiwa kuamini kuwa al-Masiyh ad-Dajjaal atajitokeza. Kati ya macho yake kumeandikwa “kafiri”. Hadiyth zilizokuja juu ya hilo na kuamini kuwa hilo litakuwepo.

MAELEZO

Ahl-us-Sunnah wanaamini kuwa ad-Dajjaal atajitokeza katika zama za mwisho. Hili ni haki na limethibiti katika Sunnah. Hata kama Ahl-ul-Bid´ah wapotofu wanalipinga hilo atajitokeza pasi na shaka. Atatembea ulimwenguni kote isipokuwa tu Makkah na al-Madiynah. Malaika watasimama kwenye miji miwili hiyo na kumfukuza yeye, mayahudi na wazushi waliopotea, hawatoweza kuingia ndani ya miji miwili hiyo. Tetemeko la ardhi litaupata mji wa al-Madiynah ambapo kila mtu mchafu atatoka ndani yake na kumfuata ad-Dajjaal, hayo yamepokelewa katika mapokezi mengi.

Jicho lake la upande wa kulia limetoka na katikati ya paji lake kumeandikwa ك ف ر. Bi maana (كافر). Kila muumini atayasoma. Ni mamoja ni msomi au si msomi. Watayasom maandishi hayo na kumjua. Hili ni jambo ambalo wamepewa kwalo mtihani Ummah huu. Kujitokeza kwake ni moja katika zile alama kubwa. Atakaa ardhini kwa muda wa siku arubaini. Siku moja ni sawa na mwaka, siku ya pili ni sawa na mwezi mzima, siku ya tatu ni sawa na wiki na siku zilizobaki zitakuwa kama siku za kawaida. Hivo ndivo zinavosema khabari sahihi.

Imethibiti ya kwamba atakuwa na pepo na moto na kwamba atamuua mtu kisha ampe uhai tena. Wafuasi wake watakuwa na maisha mazuri na wale wataomkataa watapata tabu. Haya ni majaribio ambayo amesema (Ta´ala) juu yake:

الَّذِي خَلَقَ الْمَوْتَ وَالْحَيَاةَ لِيَبْلُوَكُمْ أَيُّكُمْ أَحْسَنُ عَمَلًا

“Ambaye ameumba mauti na kifo ili akujaribuni ni nani kati yenu mwenye matendo mazuri zaidi.”[1]

Vinginevyo yeye ni adui wa Allaah. Anaitwa kwa mujibu wa udanganyifu wake, lakini hatima yake atauawa yeye na wafuasi wake. Wakati ´Iysaa bin Maryam (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ataposhuka ardhini atamuua ad-Dajjaal na jeshi lake ambalo lina mayahudi na Khawaarij.

Kwa hiyo miongoni mwa misingi ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah ni kuamini kujitokeza kwa ad-Dajjaal. Hata kama Ahl-ul-Bid´ah na wapotofu wanalipinga hilo kupinga kwao kumejengwa juu ya ujinga. Ahl-us-Sunnah wanathibitisha juu ya kujitokeza kwake kutokana na elimu walionayo kutoka kwa yule mkweli na mwenye kusadikishwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Ametuamrisha (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuomba kinga dhidi ya ad-Dajjaal na akasema:

“Pindi mmoja wenu anapomaliza Tashahhud [ya mwisho] basi amuombe Allaah kinga dhidi ya mambo mane na aseme:

اللَّهُمَّ إِنِّي أَعُوذُ بِكَ مِنْ عَذَابِ جهنم و من عَذَابِ الْقَبْر ومِنْ فِتْنَةِ الْمَحْيَا وَالْمَمَاتِ وَ مِنْ شرِ فتنة الْمَسِيحِ الدَّجَّالِ

“Ee Allaah! Hakika mimi nakuomba ulinzi kutokamana na adhabu ya Moto, kutokamana na adhabu ya ndani ya kaburi, kutokamana na fitina ya uhai na kifo na kutokamana na shari ya al-Masiyh ad-Dajjaal.”

Kisha ajiombee kile anachotaka.”[2]

[1] 67:02

[2] Muslim (588), Abu ´Awaanah, an-Nasaa’iy na Ibn-ul-Jaaruud katika ”al-Muntaqaa” (27). Imetajwa katika ”al-Irwaa’” (350).

  • Mhusika: ´Allaamah Zayd bin Muhammad al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Latwiyfah ´alaa Usuwl-is-Sunnah al-Muniyfah, uk. 91-92
  • Imechapishwa: 16/10/2019