32. Kuamini adhabu ya kaburi


Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) amesema:

“Inatakiwa kuamini adhabu ya kaburi na kwamba ummah huu utapewa mtihani katika makaburi yao. Wataulizwa juu ya imani na Uislamu na ni Mola na Mtume wao? Munkar na Nakiyr watamwendea yule maiti kama anavyotaka Allaah (´Azza wa Jall). Yanatakiwa kuaminiwa na kusadikishwa”

MAELEZO

Kumepokelewa Hadiyth nyingi kuhusu adhabu ya kaburi. Moja katika Aayah kuhusu hilo ni maneno ya Allaah (Tabaarak wa Ta´ala):

النَّارُ يُعْرَضُونَ عَلَيْهَا غُدُوًّا وَعَشِيًّا ۖ وَيَوْمَ تَقُومُ السَّاعَةُ أَدْخِلُوا آلَ فِرْعَوْنَ أَشَدَّ الْعَذَابِ

“Wanadhihirishiwa moto asubuhi na jioni, na Siku itakayosimama Saa [kutasemwa]: “Waingizeni watu wa Fir’awn katika adhabu kali kabisa!”[1]

Fir´awn, watu wake na makafiri wengine wote wanaonyeshwa Moto, asubuhi na jioni. Hii ni adhabu ya ndani ya kaburi. Kisha akataja adhabu ya siku ya Qiyaamah:

وَيَوْمَ تَقُومُ السَّاعَةُ أَدْخِلُوا آلَ فِرْعَوْنَ أَشَدَّ الْعَذَابِ

“… na Siku itakayosimama Saa [kutasemwa]: “Waingizeni watu wa Fir’awn katika adhabu kali kabisa!”

Kuna Aayah nyenginezo nyingi zinazoashiria hili.

al-Bukhaariy na Muslim wamepokea ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipita pembezoni mwa kaburi mbili na akasema:

“Hakika hawa wanaadhibiwa, hawaadhibiwi kwa kitu kikubwa. Bali ni jambo kubwa. Ama mmoja wao alikuwa akieneza uvumi na kuhusu mwengine alikuwa hajilindi na cheche za mkojo.”[2]

Wametumbukia katika madhambi makubwa na ndio maana Allaah amewaadhibu ndani ya kaburi. Hii ni dalili inayofahamisha kuwa watu wanaadhibiwa ndani ya makaburi kwa sababu ya madhambi yao.

Kadhalika al-Baraa´ amepokea kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ya kwamba Munkar na Nakiyr watamwendea yule maiti na kumuhoji. Muumini atasema:

“Muhammad ndiye Mtume wa Allaah. Alitujia kwa hoja na uongofu ambapo tukamuamini na kumfuata.”

Hivyo ndivyo ilivyotajwa katika Hadiyth ya Asmaa´. Katika Hadiyth ya al-Baraa´ imetajwa namna ambavyo muumini ataulizwa maswali yafuatayo:

“Ni nani Mola wako? Ni nani Mtume wako? Ni ipi dini yako?” Atasema: “Mola wangu ni Allaah, dini yangu ni Uislamu na Mtume wangu ni Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).” Baada ya hapo kutasemwa: “Tunakutambua. Ulikuwa muumini. Lala ikiwa ulikuwa muumini.” Hapo ndipo atapata kuiona nafasi yake Motoni lau angelikuwa ni kafiri. Kisha kutasemwa: “Allaah amekupa badala yake mahala Peponi.” Ndipo aseme: “Ee Allaah! Lete Qiyaamah!” ambapo ataambiwa: “Subiri.”

Malaika hao wawili watamwendea vilevile kafiri na kusema: “Ni nani Mola wako? Ni nani Mtume wako? Ni ipi dini yako?” Aseme: “Aah, sijui. Niliwasikia watu wakisema kitu na mimi nikakisema.”[3]

Tunamuomba Allaah usalama. Kunakhofiwa juu ya watu wengi. Kwa sababu hawajui ujumbe unahusiana na nini kikweli. Hawajui kuwa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuja na hoja na uongofu. Hawajui maana ya shahaadah. Si vinginevyo isipokuwa tu wanafuata kichwa mchunga.

Kwa hivyo muumini anatakiwa kutahadhari, akizingatie Kitabu cha Allaah na afanye maandalizi kwelikweli juu ya maswali haya. Muhammad bin ´Abdillaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alitujia na hoja na uongofu ambapo tukamuamini na kumfuata.  Imani hii imefungamana na utambuzi wa uongofu na hoja ambayo imekuja na Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Haya ndio yenye kunufaisha katika mtihani huu mzito.

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakika nyinyi mtapewa mitihani katika makaburi yenu kama mfano, au karibu, na mtihani wa ad-Dajjaal.”[4]

Katika Tashahhud kunasemwa:

“Ee Allaah! Hakika mimi nakuomba ulinzi kutokamana na adhabu ya kaburi. Ninakuomba ulinzi kutokamana na mtihani wa al-Masiyh ad-Dajjaal. Ninakuomba ulinzi kutokamana na mtihani wa uhai na wa kifo.”[5]

Kuna dalili nyingi kuhusu adhabu ya kaburi na adhabu baada ya kifo kukiwemo zile tulizozitaja. Ni jambo limethibiti wanaloliamini Ahl-us-Sunnah ilihali Mu´tazilah na wafuasi wao wapotevu wanalipinga.

Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) amesema:

“Inatakiwa kuamini adhabu ya kaburi na kwamba ummah huu utapewa mtihani katika makaburi yao. Wataulizwa juu ya imani na Uislamu na ni Mola na Mtume wao? Munkar na Nakiyr watamwendea yule maiti vile Allaah (´Azza wa Jall) anavyotaka. Yanatakiwa kuaminiwa na kusadikishwa”

Ni vipi Munkar na Nakiyr watamwendea yule maiti kwenye kaburi? Kama anavyotaka Allaah. Malaika huingia kwenye kifuko cha uzazi cha mama na huamrishwa kuandika mambo mane; riziki, muda wake wa kuishi, matendo na kama kipomoko kile kitakuwa na masikitiko au na furaha. Wengine wanaingia kwenye kaburi na kuuliza. Vipi? Hatujui. Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) pekee ndiye anayejua hilo na Yeye ndiye katujuza hilo. Wewe huna jengine isipokuwa kuamini tu. Sifa bora ya muumini ni kuwa yeye anaamini yale mambo yaliyofichikana:

ذَٰلِكَ الْكِتَابُ لَا رَيْبَ ۛ فِيهِ ۛ هُدًى لِّلْمُتَّقِينَ الَّذِينَ يُؤْمِنُونَ بِالْغَيْبِ وَيُقِيمُونَ الصَّلَاةَ وَمِمَّا رَزَقْنَاهُمْ يُنفِقُونَ

“Hiki ni Kitabu – kisicho na shaka ndani yake – ni mwongozo kwa wenye kumcha Allaah, wale wanaoamini mambo yaliyofichikana, na husimamisha swalah na katika Tulivyowaruzuku hutoa.”[6]

Unatakiwa kuamini yale mambo yaliyofichikana ambayo yameangaziwa na Qur-aan, unatakiwa kuamini mambo yaliyofichikana ambayo Sunnah ya Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) imeyaangazia. Allaah amemwamrisha (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuifikisha Qur-aan hii na kuibainisha kukiwemo suala hili. Hadiyth hizi zinapambanua Aayah hizi zilizotaja adhabu au neema za ndani ya kaburi.

[1] 40:46

[2] al-Bukhaariy (218) Muslim (292).

[3] al-Bukhaariy (1374) na Muslim (2871).

[4] al-Bukhaariy (86) na Muslim (905).

[5] al-Bukhaariy (1377) na Muslim (589).

[6] 02:2-3

  • Mhusika: ´Allaamah Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Usuwl-is-Sunnah, uk. 395-397
  • Imechapishwa: 10/09/2017