10 – Umm ´Atwiyyah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ameeleza:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ametuamrisha kuwatoa katika [´Iyd] al-Fitwr na [´Iyd] al-Adhwhaa´; wanawali,  wenye hedhi na wasichana mabikira. Ama wale wenye hedhi watajitenga na swalah.” Katika upokezi mwingine imekuja: “… uwanja wa kuswalia na watashuhudia kheri na ulinganizi wa waislamu.”

ash-Shawkaaniy amesema:

“Hadiyth hii na nyenginezo zilizokuja kwa maana hiyo ni zenye kuhukumu juu ya Shari´ah ya wanawake kutoka kwenda kuswali swalah mbili za ´iyd mahali pa kuswalia bila kutofautisha kati ya bikira, mtumzima, msichana, mzee, mwenye hedhi na wengineo midhali si mwenye kukaa eda au ikawa kutoka kwake kuna fitina au akawa na udhuru.”[1]

Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah amesema katika “Majmuu´-ul-Fataawaa”:

“Amewakhabarisha wanawake waumini kwamba kuswali kwao majumbani mwao ni bora kwao kuliko kuhudhuria swalah ya ijumaa na za mkusanyiko isipokuwa swalah ya ´iyd. Amewaamrisha kutoka kuiendea na hilo – na Allaah ndiye mjuzi zaidi – huenda ni kwa sababu zifuatazo:

a) Katika mwaka ni mara mbili ndio ikakubaliwa tofauti na ijumaa na swalah ya mkusanyiko.

b) Haina badala tofauti na ijumaa na swalah ya mkusanyiko. Mwanamke kuswali nyumbani kwake Dhuhr ndio ijumaa yake.

c) Kutoka kwake kwenda katika jangwa kwa ajili ya kumdhukuru Allaah kumefanana na hajj kwa baadhi ya njia. Kwa ajili hii ikawa ile ´iyd kubwa ni yenye kuafikiana na wale mahujaji.”[2]

Wanachuoni wa ki-Shaafi´iy wameweka sharti kutoka kwa wanawake kwenda kuswali swalah ya ´iyd kwa wale wasiokuwa na mapambo. Imaam an-Nawawiy amesema katika “al-Majmuu´”:

“ash-Shaafi´iy na wenzake (Rahimahumu Allaah) wamesema: “Imependekezwa kwa wanawake, mbali na wale wenye mapambo, kuhudhuria swalah ya ´iyd. Ama wale wenye mapambo imechukizwa kuhudhuria kwao.” Mpaka aliposema: “Wakitoka basi imependekezwa watoke wakiwa na nguo za kazi na wasivae nguo zenye kuwashuhurisha. Imesuniwa wajisafishe kwa maji na yameharamishwa kwao manukato. Zote hizi ni hukumu za wale ambao hawatamaniwi na mfano wao. Ama kuhusu wasichana, warembo na wale wanaotamaniwa imechukizwa kwao kuhudhuria kutokana na ile fitina inayokhofiwa juu yao na kutokamana na wao. Kukisemwa kwamba hayo yanapingana na Hadiyth iliyotajwa ya Umm ´Atwiyyah, tutasema: “Imethibiti katika “as-Swahiyh” ya al-Bukhaariy na ya Muslim kupitia kwa ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) aliyesimulia:

“Lau Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) angeliwaona wanawake yale tunayoyaona basi angeliwazuia kutokamana na msikiti kama ambavo wana wa Israaiyl waliwazuia wanawake zao.”[3]

Jengine ni kwa sababu ya fitina na sababu za shari hii leo ni nyingi tofauti na zama za mwanzo – na Allaah ndiye anajua zaidi.”

Katika zama zetu ni kubwa zaidi. Imaam Ibn-ul-Jawziy amesema katika kitabu “Ahkaam-un-Nisaa´”:

“Nilikuwa nimebainisha kwamba kutoka kwa wanawake ni jambo limependekezwa. Lakini kukikhofiwa fitina kwao au kutokamana na wao basi kuwazuia kutoka itakuwa ni bora. Kwa sababu wanawake wa kizazi cha kwanza hawakuwa juu ya yale waliyokulia wanawake wa zama hizi na vivyo hivyo kwa wanaume.”[4]

Bi maana walikuwa wakimcha Allaah sana. Dada wa Kiilamu umepata kujua kupitia nukuu hizi kwamba kutoka kwako kwenda kuswali swalah ya ´iyd kumeruhusiwa Kishari´ah kwa sharti ya kulazimiana, kujiheshimu na kukusudia kujikurubisha kwa Allaah na kushirikiana na waislamu katika ulinganizi wao na kudhihirisha nembo za Uislamu. Makusudio sio kuonyesha mapambo na kujiweka katika fitina. Tanabahi juu ya hilo.

[1] (03/306).

[2] (06/458-459).

[3] (05/13).

[4] Uk. 38.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tanbiyhaat, uk. 61-63
  • Imechapishwa: 05/11/2019