Si lazima ukiona jambo jema kwa mtazamo wako likawa ni jema kwa mtazamo wa wengine. Labda katika kitu ambacho hakuna nafasi ya Ijtihaad ndani yake. Katika mambo ambayo ni ya Ijtihaad mimi naweza kuona kitu fulani kuwa ni katika wema na mwengine akaona kinyume na hivo. Hapo marejeo itatakiwa iwe Qur-aan na Sunnah:

فَإِن تَنَازَعْتُمْ فِي شَيْءٍ فَرُدُّوهُ إِلَى اللَّـهِ وَالرَّسُولِ إِن كُنتُمْ تُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ

“Mkizozana juu ya jambo, basi lirudisheni kwa Allaah na Mtume mkiwa mnamuamini Allaah na siku ya Mwisho.”[1]

Mfumo wa Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah katika mlango huu mkubwa, ambao Ummah huu umefadhilishwa juu ya nyumati zengine, wanaona kuwa kazi ya kuamrisha mema na kukataza maovu ni katika nyenzo kubwa zinazoijenga jamii ya Kiislamu. Lakini kunahitajia mambo yafuatayo:

1- Mtu awe ni mtambuzi wa hukumu kwa njia ya kwamba anajua kuwa kitu fulani ni jema na kitu fulani ni uovu. Ama kufanya ujinga kisha akaamrisha jambo ambalo yeye anadhani kuwa ni jema, ilihali sio jema, jambo hili madhara yake yanaweza kuwa makubwa kuliko manufaa yake. Tukadirie mtu amekulia katika jamii ambayo inaona Bid´ah fulani kuwa ni wema kisha akaenda katika jamii nyingine isiyofanya ambapo akaanza kuwakemea kwa kutokufanya kwao na akawaamrisha nayo. Hili ni kosa. Usiamrishe jambo isipokuwa uwe na uhakika kuwa ni wema kwa mujibu wa Shari´ah ya Allaah na si vile unavyoamini wewe na pale ulipokulia. Ni lazima uijue hukumu na kwamba jambo fulani ni wema ili uweze kuliamrisha. Hali kadhalika maovu.

2- Unapaswa ujue kuwa jema hili halikufanywa na uovu huu umefanywa. Ni watu wangapi wamewaamrisha wengine wema na tamahaki wao wenyewe wanalifanya! Anakuwa katika jambo hili ni mzigo juu ya wengine na huenda jambo hilo likampunguzia hadhi yake mbele ya watu.

[1] 04:59

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Manhaj Ahl-is-Sunnah wal-Jamaa´ah fiy-´Aqiydah wal-´Amal, uk. 42-43
  • Imechapishwa: 22/08/2019