Shaykh-ul-Islaam na Imaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Sharti ya nane ni kuelekea Qiblah. Dalili ni Kauli Yake (Ta´ala):

قَدْ نَرَى تَقَلُّبَ وَجْهِكَ فِي السَّمَاء فَلَنُوَلِّيَنَّكَ قِبْلَةً تَرْضَاهَا فَوَلِّ وَجْهَكَ شَطْرَ الْمَسْجِدِ الْحَرَامِ وَحَيْثُ مَا كُنتُمْ فَوَلُّواْ وُجُوِهَكُمْ شَطْرَهُ

“Hakika Tumeona unavyogeuzageuza uso wako mbinguni, basi Tutakuelekeza Qiblah kinachokuridhisha. Hivyo basi uelekeze uso wako upande wa Msikiti mtakatifu; na popote mtakapokuwepo basi zielekezeni nyuso zenu upande wake.”[1]

MAELEZO

Kuelekea Qiblah ni sharti miongoni mwa sharti za kusihi kwa swalah.

Mtunzi amesema:

“Dalili ni Kauli Yake (Ta´ala):

قَدْ نَرَى تَقَلُّبَ وَجْهِكَ فِي السَّمَاء فَلَنُوَلِّيَنَّكَ قِبْلَةً تَرْضَاهَا فَوَلِّ وَجْهَكَ شَطْرَ الْمَسْجِدِ الْحَرَامِ وَحَيْثُ مَا كُنتُمْ فَوَلُّواْ وُجُوِهَكُمْ شَطْرَهُ

“Hakika Tumeona unavyogeuzageuza uso wako mbinguni, basi Tutakuelekeza Qiblah kinachokuridhisha. Hivyo basi uelekeze uso wako upande wa Msikiti mtakatifu; na popote mtakapokuwepo basi zielekezeni nyuso zenu upande wake.”

Maneno Yake:

فَوَلِّ

“Hivyo basi uelekeze… “

yamekuja kwa njia ya amri. Maneno Yake:

وَجْهَكَ شَطْرَ الْمَسْجِدِ الْحَرَامِ

“… uso wako upande wa Msikiti mtakatifu…. “

Bi maana katika Ka´bah. Hapana tofauti juu ya hilo[2].

Zipo aina mbili za kuelekea Qiblah:

1 – Wako ambao wanalazimika kuilenga Ka´bah kwa macho. Huyo ni yule ambaye yuko Makkah au karibu nayo nyuma ya kizuizi. Pale anapojua kuwa ameielekea Ka´bah basi atatendea kazi ujuzi wake. Asipojua – kama mfano wa kipofu na mgeni Makkah – basi atatosheka na kuelezwa na mwaminifu au ashuhudie kuwa ni mwenye kuswali kwa kuielekea Ka´bah yenyewe.

2 – Ambaye inamlazimu kuelekea upande wa Ka´bah. Huyo ni yule ambaye yuko mbali na Ka´bah. Mtu huyu haimlazimu kuilenga kwa macho.”[3]

Yule mwenye kuswali kinyume na Qiblah kwa kuamini au kudhani kuwa ameelekea Qiblah swalah yake ni batili. Kujengea juu ya hilo itamlazimu kuirudi swalah yake. Ni lazima kwake kuuliza kama anaweza kufanya hivo. Lakini akiwa jangwani na asipate Mihraab au ambaye atamweleza, basi itamlazimu kujitahidi ni wapi kiko Qiblah na ataelekea kule ilipofikia ijtihaad yake. Akijitahidi na akaswali basi swalah yake ni sahihi ingawa baadaye itabaini kuwa ni kinyume na Qiblah.

[1] 02:144

[2] Tafsiyr-ul-Qurtwuubiy (02/159).

[3] al-Kaafiy (01/117-118).

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Shuruwt-is-Swalaah, uk. 47-49
  • Imechapishwa: 30/12/2021