31. Ni lipi jukumu la wanafunzi juu ya vijana wanaoingia katika mapote potevu?


Swali 31: Ni lipi jukumu letu sisi kama wanafunzi kwa ndugu zetu vijana ambao wameanza kuingia katika vipote ambavyo umeviashiria katika baadhi ya vitabu na darsa zako zilizoandikwa? Je, una nasaha kuhusiana na maudhui hii ambayo inastahiki kutiliwa umuhimu mkubwa.

Jibu: Jukumu la wanafunzi ambao wanafuata mfumo wa Salaf katika mlango huu linatakiwa kuwa kubwa. Wanatakiwa kuwa na juhudi kubwa. Mara wanatakiwa kulingania katika dini na katika njia ya Allaah na vilevile katika mfumo wa haki ambao ni mfumo wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Wakati mwingine wanatakiwa kubainisha makosa ambayo yanapitika kwa watu walio na mifumo mipya. Kadhalika wanaweza pia kufanya hilo kwa kuandika. Vilevile wanaweza kufanya hivo kwa maneno mazuri na watoe nasaha za kisiri na zisizo za kisiri. Wanatakiwa kufanya yote hayo huenda Allaah (´Azza wa Jall) akamuokoa mwenye kumuokoa na akamjaalia kurejea yule ambaye atakuwa amewafikishwa. Sisi tukifanya sababu tutakuwa tumeitakasa dhimma yetu kutokamana na waangamivu hawa. Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) ameeleza juu ya watu wa mji ambao waliivunja sabato. Walikuwa wamegawanyika mafungu matatu. Fungu la kwanza walikuwa wakivua [samaki] siku ya jumamosi ambapo wanatega siku ya jumamosi na wanakuja siku ya jumapili wanavua kwa hoja kwamba wamevua siku ya jumapili na sio siku ya jumamosi. Hii ni hila walioifanyia Shari´ah ambayo Allah aliwawekea. Kukawepo watu wenye kuwakemea na wengine wakanyamaza mpaka wakafikia kusema:

لِمَ تَعِظُونَ قَوْمًا ۙ اللَّـهُ مُهْلِكُهُمْ أَوْ مُعَ ذِّبُهُمْ عَذَابًا شَدِيدًا ۖ قَالُوا مَعْذِرَةً إِلَىٰ رَبِّكُمْ وَلَعَلَّهُمْ يَتَّقُونَ

“Kwa nini mnawawaidhi watu ambao Allaah atawaangamizi au atawaadhibu adhabu kali?” Wakasema [wale wakemeaji]: “Tupate kuwa na udhuru mbele Mola wenu na huenda wakaogopa.”” (07:164)

Pindi Alipowaangamiza watu wale inasemekana kuwa maangamivu yaliwapata wale watendaji wa jarima na wale walionyamaza. Kwa kuwa hawakutakasa jukumu lao juu ya jambo hili. Waliosalimika na adhabu ni wale waliosimama na kazi ya kukaripia hila hizi za kuvua siku ya jumamosi.

Kwa hiyo ni wajibu kwa wanafunzi na wasomi wenye kutambua mfumo wa Salaf na mifumo mingine wawabainishie wengine, wazungumze, waongee na wahubiri. Wanatakiwa waweke wazi kila mahali na katika kila mnasaba. Haki ndio inatakiwa ifuatwe na batili iepukwe.

Kuhusu wale wanaonyamazia kubainisha haki, hawapewi udhuru kwa kunyamaza kwao hata kama watasema kuwa hawako pamoja nao. Sio wenye kupewa udhuru. Hata kama watasema kuwa wao hawako pamoja na mapote haya yaliyopotea na njia ya haki. Isipokuwa ikiwa kama watakemea ule upotevu waliyomo.

  • Mhusika: ´Allaamah Ahmad bin Yahyaa an-Najmiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Fataawaa al-Jaliyyah
  • Imechapishwa: 23/07/2017