31. Mwenye busara na anavyochagua wa kusuhubiana nao

1- Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Roho ni wanajeshi walioshikamana. Zile zinazoendana katika hizo hushikana na zile zisizoendana katika hizo hutengana.”

2- ´Aliy bin Abiy Twaalib amesema:

“Roho ni wanajeshi walioshikamana. Zile zinazoendana katika hizo hushikana na zile zisizoendana katika hizo hutengana.”

3- Baada ya mipango ya Allaah iliyotangulia roho ndio sababu za kuungana kwa watu na kutengana. Pindi roho mbili zinapokuwa na kitu kinachozifanya kuhisi urafiki, basi zinaungana. Pindi roho mbili zinapokuwa na kitu kinachozifanya kutohisi urafiki, zinatengana.

4- Mujaahid amesema:

“Ibn ´Abbaas alimuona mtu akasema: “Huyu ananipenda.” Wakasema: “Umejuaje?” Akasema: “Kwa sababu mimi nampenda na moyo ni wanajeshi walioshikamana. Zile zinazoendana katika hizo hushikana na zile zisizoendana katika hizo hutengana.”

5- Qataadah amesema:

“Wale wanaomtii Allaah basi nyoyo zao na matamanio yao yanakuwa ni yenye kukutana japokuwa watakuwa ni wenye kuishi sehemu mbalimbali. Ama wale wenye kumuasi Allaah nyoyo zao zinakuwa zenye kutofautiana japokuwa watakuwa wanaishi sehemu moja.”

6- Moja katika alama kubwa za kuyajua yaliyomo ndani ya mtu ni kutazama ni nani anayezungumza naye na anayempenda. Kwa sababu mtu anakuwa katika dini ya rafiki yake na ndege mbinguni huruka na wale wanaofanana nao. Sijaona kitu kinachofahamisha vyema kitu kingine, wala moshi haufahamishi moto, kama rafiki wa mtu.

7- Hubayrah amesema:

“Wachukulie watu kutokamana na marafiki zao.”

8- Maalik amesema:

“Watu wako tabaka mbalimbali kama ndege. Njiwa anakuwa na njiwa. Jogoo anakuwa na jogoo. Bata anakuwa na bata. Kibwirosagi anakuwa na kibwirosagi[1]. Kila mtu anakuwa na wa aina yake.”

9- Mwenye busara anajiepusha kutangamana na watu wenye mashaka. Anajiepusha na watu wenye mashaka katika dini zao. Kwa sababu mwenye kutangamana na watu fulani basi atatambulika kupitia wao na atakayeishi na mtu atanasibishwa naye. Mtu hataamiliani isipokuwa na mtu kama yeye au mfano wake. Endapo mtu atalazimika kutangamana na watu basi awatafute watu ataopambika kwa kusuhubiana nao na hawatompa tuhuma mbaya. Akimuona anafanya tendo jema, atalihesabu. Akimuona anafanya tendo ovu, atamsitiri. Akimnyamazia, basi yeye ndiye atamuanzisha kumzungumzisha. Akimuomba kitu, atampa. Ama kuhusu leo undani wa watu wengi unatofautiana na uinje wao.

10- Sababu inayopelekea mtu kuonyesha masikitiko pindi ndugu wawili wanapotengana ni mtu kutoridhia makadirio. Yule mwenye kuiambia nafsi yake tokea mwanzo wa udugu kwamba matangamano yanaweza kwisha vibaya haonyeshi kusikitishwa wala kuhuzunishwa isipokuwa kwa kiasi cha vile elimu inavopelekea.

[1] Tazama https://sw.wikipedia.org/wiki/Kibwirosagi

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Hibbaan al-Bustiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Rawdhat-ul-´Uqalaa’ wa Nuzhat-ul-Fudhwalaa’, uk. 107-112
  • Imechapishwa: 15/04/2018