Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Mola ndiye mwabudiwa. Dalili ni maneno Yake (Ta´ala):

 يَا أَيُّهَا النَّاسُ اعْبُدُوا رَبَّكُمُ الَّذِي خَلَقَكُمْ وَالَّذِينَ مِن قَبْلِكُمْ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ الَّذِي جَعَلَ لَكُمُ الْأَرْضَ فِرَاشًا وَالسَّمَاءَ بِنَاءً وَأَنزَلَ مِنَ السَّمَاءِ مَاءً فَأَخْرَجَ بِهِ مِنَ الثَّمَرَاتِ رِزْقًا لَّكُمْ ۖ فَلَا تَجْعَلُوا لِلَّـهِ أَندَادًا وَأَنتُمْ تَعْلَمُونَ

“Enyi watu! Mwabuduni Mola wenu ambaye amekuumbeni na wale wa kabla yenu mpate kumcha. Ambaye amewafanyieni ardhi kuwa ni tandiko na mbingu kuwa ni paa na akateremsha kutoka mbinguni maji, akawatolea kwayo matunda kuwa ni riziki zenu. Hivyo basi, msimfanyie Allaah waliolingana naye na hali ya kuwa nyinyi mnajua.” (al-Baqarah 02 : 21-22)

MAELEZO

Mtunzi wa kitabu (Rahimahu Allaah) anaashiria maneno ya Allaah (´Azza wa Jall):

إِنَّ رَبَّكُمُ اللَّـهُ الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ فِي سِتَّةِ أَيَّامٍ ثُمَّ اسْتَوَىٰ عَلَى الْعَرْشِ يُغْشِي اللَّيْلَ النَّهَارَ يَطْلُبُهُ حَثِيثًا وَالشَّمْسَ وَالْقَمَرَ وَالنُّجُومَ مُسَخَّرَاتٍ بِأَمْرِهِ ۗ أَلَا لَهُ الْخَلْقُ وَالْأَمْرُ ۗ تَبَارَكَ اللَّـهُ رَبُّ الْعَالَمِينَ

“Hakika Mola wenu ni Allaah ambaye ameumba mbingu na ardhi katika siku sita, kisha akalingana juu ya ‘Arshi. Zindukeni! Ni Vyake pekee uumbaji na amri. Amebarikika Allaah, Mola wa walimwengu.” (al-A´raaf 07 : 54)

Mola ndiye mwabudiwa. Kwa msemo mwingine ndiye ambaye anastahiki kuabudiwa, au Yeye ndiye mwenye kuabudiwa kwa sababu anastahiki kuabudiwa. Haina maana kila mwenye kuabudiwa ni mola. Miungu inayoabudiwa badala ya Allaah na ikafanywa kuwa ni miungu badala ya Allaah, sio miungu ya kweli.

Mola ndiye Muumbaji, Mfalme na Mwenye kuendesha mambo yote.

Dalili – Bi maana dalili juu ya kwamba Mola ndiye mwenye kustahiki kuabudiwa.

Enyi Watu! – Wito unawaelekea watu wote. Allaah (´Azza wa Jall) amewaamrisha watu kumwabudu Yeye pekee pasi na kumshirikisha na kumfanyia washirika. Halafu amebainisha kwamba Yeye pekee ndiye anastahiki kuabudiwa kwa sababu Yeye pekee ndiye Muumbaji, asiyekuwa na mshirika.

… ambaye amekuumbeni… – Hii ni sifa ya wazi inayotolea sababu yaliyotangulia. Mwabuduni Allaah, kwa sababu Yeye ndiye Mola Wenu aliyekuumbeni. Kwa vile Yeye ndiye Mola na Muumbaji, basi inawalazimu kwenu nyinyi kumuabudu. Kwa ajili hii tunasema kila aliyekubali uola wa Allaah, basi anatakiwa amwabudu Allaah pekee. Vinginevyo anakuwa ni mwenye kujigonga.

… mpate kumcha… – Bi maana ili mfikie kumcha Allaah. Taqwa ni kuchukua kinga kutokamana na adhabu ya Allaah (´Azza wa Jall) njia ya kwamba kutekeleza maamrisho Yake na kujiepusha na makatazo Yake.

Ambaye amewafanyieni ardhi kuwa ni tandiko – Ameifanya kuwa ni tandiko na godoro. Tunastarehe juu yake bila ya matatizo wala tabu kama jinsi mtu anavyolala juu ya kitanda chake.

… na mbingu kuwa ni paa – Bi maana juu yetu, kwa sababu ya paa, ambayo ni paa juu ya wakazi wa ardhi, iko juu ya mbingu na ni dari iliyohifadhiwa. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَجَعَلْنَا السَّمَاءَ سَقْفًا مَّحْفُوظًا ۖ وَهُمْ عَنْ آيَاتِهَا مُعْرِضُونَ

“Tukajaalia mbingu kuwa ni dari ilohifadhiwa. Lakini wao wanazikengeuka ishara zake.” (al-Anbiyaa´ 21 : 32)

… na akateremsha kutoka mbinguni maji… – Ameteremsha maji masafi kutoka juu mbinguni. Amesema (Ta´ala):

لَّكُم مِّنْهُ شَرَابٌ وَمِنْهُ شَجَرٌ فِيهِ تُسِيمُونَ

“… katika hayo mnapata kinywaji na kwa hayo inatoa miti ambayo humo mnalisha.” (an-Nahl 16 : 10)

… akawatolea kwayo matunda kuwa ni riziki zenu – Kipao kwenu. Katika Aayah nyingine:

مَتَاعًا لَّكُمْ وَلِأَنْعَامِكُمْ

”Ni manufaa kwenu na kwa wanyama wenu wa mifugo.” (an-Naazi´aat 79 : 33)

Hivyo basi, msimfanyie Allaah waliolingana naye… – Msimuwekee washirika Yule aliyekuumbeni nyinyi na wale waliokuwa kabla yenu, akawafanyieni ardhi kuwa ni tandiko na mbingu kuwa paa, akawateremshieni maji kutoka mbinguni, akawatolea kwayo matunda kuwa ni riziki zenu. Msimfanyie washirika ambao mnawaabudu au kuwapenda kama jinsi mnavyomuabudu au kumpenda Allaah. Haiwastahikii kwenu kufanya hivo, si kiakili wala kidini.

… na hali ya kuwa nyinyi mnajua – Nyinyi mnajua kuwa Hana mshirika yeyote na kuumba, kuruzuku na kuendesha mambo kuko mikononi Mwake. Hivyo basi, msimfanyie mshirika katika kumwabudu.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 50-52
  • Imechapishwa: 22/05/2020