31. Kupata hedhi baada ya kuingia wakati wa swalah

Swali 31: Ni ipi hukumu ya mwanamke akipata hedhi baada ya kuingia wakati wa swalah? Je, ni lazima kuilipa pindi atapotwahirika? Vivyo hivyo endapo atatwahirika kabla ya kumalizika wakati wa swalah?

Jibu:

1 – Mwanamke akipata hedhi baada ya kuingia wakati wa swalah, basi ni lazima pindi ataposafika kulipa swalah hiyo ambayo alipata hedhi ndani ya wakati wake ikiwa hakuwahi kuiswali kabla ya yeye kujiliwa na hedhi. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yule mwenye kuwahi Rak´ah moja ya swalah basi ameiwahi swalah.”

Kwa hivyo mwanamke akidiriki katika wakati wa swalah kiwango cha kuwahi kuswaliwa Rak´ah moja kisha akapata hedhi kabla yeye kuiswali, basi akitwahirika atalazimika kuilipa.

2 – Ukitwahirika na hedhi kabla ya kumalizika wakati wa swalah, basi itamlazimu kuilipa swalah hiyo. Ikiwa atasafika kabla ya kuchomoza kwa jua kwa kiwango cha kuwahiwa kuswaliwa Rak´ah moja, basi itamlazimu kulipa swalah ya Fajr. Ikiwa atasafika kabla ya kuzama kwa jua kwa kiwango cha kuwahiwa kuswaliwa Rak´ah moja, basi itamlazimu kuswali swalah ya ´Aswr. Ikiwa atasafika kabla ya nusu ya usiku kwa kiwango cha kuwahiwa kuswaliwa Rak´ah moja, basi itamlazimu kulipa swalah ya ´Ishaa. Akitwahirika baada ya nusu ya usiku basi swalah ya ´Ishaa haitomuwajibikia. Itampasa kuswali Fajr itapofika wakati wake. Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amesema:

فَإِذَا اطْمَأْنَنتُمْ فَأَقِيمُوا الصَّلَاةَ ۚ إِنَّ الصَّلَاةَ كَانَتْ عَلَى الْمُؤْمِنِينَ كِتَابًا مَّوْقُوتًا

“Mtakapopata utulivu, basi simamisheni swalah. Kwani hakika swalah kwa waumini ni fardhi iliyowekwa nyakati maalum.”[1]

Bi maana ni faradhi iliopangiwa wakati katika nyakati maalum.

Haijuzu kwa mtu kuindoa swalah nje ya wakati wake wala kuianza kabla ya kuingia wakati wake.

[1] 04:103

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: 60 su-aal wa jawaab fiy Ahkaam-il-Haydhw, uk. 27-28
  • Imechapishwa: 29/07/2021