Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) amesema:

“Inatakiwa kuamini Hodhi na kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ana hodhi ambayo Ummah wake siku ya Qiyaamah wataijia. Upana wake ni kama urefu wake na ni sawa na masafa ya safari ya mwezi. Vikombe vyake ni sawa na idadi ya nyota mbinguni, kama yalivyopokelewa mapokezi Swahiyh kupitia njia nyingi.”

MAELEZO

Ni lazima kwa mja kuamini Hodhi. Kumepokelewa Hadiyth nyingi juu ya Hodhi. Upana wake ni sawa na urefu wake[1] na ni sawa na masafa ya safari ya mwezi[2]. Hadiyth zinasema kuwa urefu wake ni sawa na mwendo kati ya al-Madiynah na Swan´aa´[3] na kati ya Swan´aa´ na Ayla[4].

Hodhi ni moja katika zawadi ya Allaah kwa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Amesema juu yake:

إِنَّا أَعْطَيْنَاكَ الْكَوْثَرَ فَصَلِّ لِرَبِّكَ وَانْحَرْ إِنَّ شَانِئَكَ هُوَ الْأَبْتَرُ

“Hakika Sisi tumekupa [mto wa] al-Kawthar! Hivyo basi swali na uchinje kwa ajili ya Mola wako! Hakika mbaya wako, yeye ndiye atakayekatiliwa mbali.”[5]

Hodhi ni miongoni mwa vitu vizuri kabisa ambavyo Allaah amempa na kumtukuza kwavyo mja Wake na Mtume Wake Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) duniani na Aakhirah.

Imepokelewa namna ambavyo kuna watu ambao watatimuliwa mbali na Hodhi hiyo. Ni wenye kuritadi wakiwa pamoja na Ahl-ul-Bid´ah, hivyo ndivyo alivyosema al-Qurtwubiy na wengine. Kuhusiana na Hadiyth yenye kutaja jinsi kuna watu wataofukuzwa mbali na Hodhi ambapo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aseme:

“Maswahabah zangu! Maswahabah zangu!”[6]

Haafidhw Ibn Hajar ametaja kuwa al-Bukhaariy amesema kuwa wenye kutimuliwa ni wale walioritadi. Wengine wakawaingiza pia Ahl-ul-Bid´ah. Kwa nini? Ndio, ni kwa sababu wamezusha baada ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Ni kwa nini wafukuzwe? Ni kwa sababu walibadilisha dini ya Allaah na wakazusha ndani yake yasiyokuwemo. Hadiyth inawagusa pia wao.

Imaam Ahmad amesema:

Vikombe vyake ni sawa na idadi ya nyota mbinguni… “

Hili ni jambo linalojulikana.

[1] Muslim (2300).

[2] al-Bukhaariy (6579).

[3] al-Bukhaariy (6580) na Muslim (2303).

[4] al-Bukhaariy (6591) na Muslim (2298).

[5] 108:1-3

[6] al-Bukhaariy (6582) na Muslim (2304).

  • Mhusika: ´Allaamah Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Usuwl-is-Sunnah, uk. 393-394
  • Imechapishwa: 10/09/2017