Swali 31: Ni ipi hukumu ya ambaye ananyanyua mikono yake wakati ambapo Khatwiyb anawaombea waislamu katika Khutbah ya pili pamoja na kunitajia dalili[1]?

Jibu: Kunyanyua mikono ni kitu hakikuwekwa katika Shari´ah katika Khutbah ya ijumaa wala katika Khutbah ya ´iyd. Ni mamoja kwa imamu wala maamuma. Kilichowekwa katika Shari´ah ni kumnyamazia Khatwiyb na kuitikia “Aamiyn” du´aa yake. Mtu afanye hivo kati yake yeye na nafsi yake pasi na kunyanyua sauti. Kuhusu kunyanyua mikono ni jambo halikuwekwa katika Shari´ah.

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakuwa akinyanyua mikono yake katika Khutbah ya ijumaa wala katika Khutbah za ´iyd. Pindi baadhi ya Maswahabah walipowaona baadhi ya viongozi wananyanyua mikono yao katika Khutbah ya ijumaa waliwakemea kitendo hicho na wakawaambia kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakuwa akiinyanyua.

Akiomba du´aa ya kuteremshiwa mvua katika Khutbah ya ijumaa hapo atanyanyua mikono yake katika ile hali ya kuomba kuteremshiwa mvua. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akinyanyua mikono yake katika hali hii. Akiomba kuteremshiwa mvua katika Khutbah ya ijumaa au katika Khutbah ya ´iyd basi imesuniwa kwake kunyanyua mikono yake kwa ajili ya kumwigiliza Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

[1] Majmuu´-ul-Fataawaa (12/338-339).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam Swalaat-il-Jumu´ah wal-Jamaa´ah, uk. 70-71
  • Imechapishwa: 02/12/2021