31. Haifai kujadiliana juu ya Qur-aan


Imaam al-Barbahaariy (Rahimahu Allaah) amesema:

Na kujadiliana juu yake ni kufuru.

MAELEZO

Bi maana kubishana juu ya Qur-aan kama imeumbwa au haikuumbwa. Mtu akawa na shaka na kusema sijui kwa sababu kuna ambao wanasema imeumbwa na wengine wanasema haikuumbwa na akaonelea kuwa ni masuala yaliyo na tofauti – kama wanavyosema hivi leo. Kumejitokeza mtindo wenye kusema:

“Masuala haya yana tofauti.”[1]

Tunasema wakati wa tofauti kinachofuatwa ni dalili. Hatukufanywa tukaabudu kwa mujibu wa tofauti za watu na maoni ya watu. Bali tumefanywa kuabudu kwa mujibu wa dalili. Tunachotakiwa kufanya ni kupima tofauti na dalili. Yale ambayo yatakuwa yamesimama juu ya dalili, basi ndio haki. Yanayokwenda kinyume na dalili, basi ni batili. Allaah Hakutuacha juu ya maoni na kauli na tofauti mbalimbali. Uhakika wa mambo ni kuwa amesema:

فَإِن تَنَازَعْتُمْ فِي شَيْءٍ فَرُدُّوهُ إِلَى اللَّـهِ وَالرَّسُولِ

“Mkizozana katika jambo, basi lirudisheni kwa Allaah na Mtume.” (04:59)

وَمَا اخْتَلَفْتُمْ فِيهِ مِن شَيْءٍ فَحُكْمُهُ إِلَى اللَّـهِ

“Jambo lolote lile mlilokhitilafiana ndani yake, basi hukumu yake ni kwa Allaah.” (42:10)

Ni wajibu kurudi katika Kitabu cha Allaah na Sunnah za Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kunachukuliwa yale yaliyosimama juu ya dalili na kuacha yale yenye kwenda kinyume na dalili.

Kuhusu ambaye anachukua maoni yanayoafikiana na hawaa na matamanio yake, hata kama yatakuwa yanaenda kinyume na dalili, huyu ni mpotevu. Huyu anaabudu matamanio yake. Ama anayemuabudu Allaah, huchukua maoni yaliyosimama juu ya dalili kutoka katika Kitabu cha Allaah na Sunnah za Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

[1] Tazama http://firqatunnajia.com/kuna-tofauti-katika-mambo-haya-ima-mjinga-au-jitu-linalofuata-matamanio/

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Sharh-is-Sunnah, uk. 70-71
  • Imechapishwa: 27/01/2018