31. ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah juu ya mikono ya Allaah


Allaah (Jalla wa ´Alaa) ana sifa za kidhati na za kimatendo. Sifa za kimatendo ni kama Ujuu, kushuka, kuumba, kuruzuku, maneno na sifa nyenginezo za matendo Yake (Subhaanahu wa Ta´ala).

Miongoni mwa sifa Zake za kimatendo ni mikono miwili. Imethibiti katika maneno ya Allaah (´Azza wa Jall) na katika Sunnah za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Amesema (Ta´ala):

وَالسَّمَاوَاتُ مَطْوِيَّاتٌ بِيَمِينِهِ

“Mbingu zitakunjwa mkononi Mwake wa kulia.” (39:67)

قَالَ يَا إِبْلِيسُ مَا مَنَعَكَ أَن تَسْجُدَ لِمَا خَلَقْتُ بِيَدَيَّ

“Akasema: “Ee Ibliys! Nini kilichokuzuia usimsujudie Niliyemuumba kwa mikono Yangu?”” (38:75)

Bi maana Aadam (´alayhis-Swalaatu was-Salaam).

Katika Hadiyth imekuja:

“Mikono ya Allaah imejaa inatoa usiku na mchana.”[1]

Kuna Hadiyth zingine Swahiyh ambazo zimemthibitishia Allaah (´Azza wa Jall) kuwa na mikono miwili na mmoja. Maana yake inajulikana katika lugha. Ni mikono miwili ya kihakika. Lakini hata hivyo sio kama mikono ya viumbe. Ni mikono miwili inayolingana na utukufu na ukubwa wa Allaah. Hakuna anayejua namna ilivyo isipokuwa Allaah (Jalla wa ´Alaa). Sisi tunaithibitisha kutokana na maana yake ya kihakika na wakati huo huo tunakanusha ufananishaji na ushabihishaji. Haifanani na mikono ya viumbe. Haya ndio madhebeu ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah. Ni madhehebu yanaenda kwa mujibu wa Qur-aan na Sunnah. Mwenendo wao katika hayo ni mwenendo ule ule inapokuja katika majina na sifa za Allaah (´Azza wa Jall) zingine.

[1] al-Bukhaariy (7419) na Muslim (36) na (993)