1- Maana ya ´ibaadah

Msingi wa ´ibaadah ni udhalili na unyenyekevu. Katika Shari´ah ina taarifu nyingi lakini maana yake ni moja. Miongoni mwazo ni kwamba ´ibaadah ni kumtii Allaah kwa kutekeleza yale aliyoamrisha Allaah kupitia Mitume Wake. Miongoni mwazo ni kwamba ´ibaadah maana yake ni kujidhalilisha kwa Allaah (Subhaanah). Ni ujidhalilishaji wa hali juu kwa Allaah (Ta´ala) pamoja na kumpenda kwa hali ya juu. Taarifu yake ya kijumla ni kwamba ´ibaadah ni jina lililokusanya kila anachokipenda Allaah na kukiridhia katika maneno na matendo yaliyo waziwazi na yaliyojificha.

´Ibaadah imegawanyika ya kimoyo, kimdomo na viungo vya mwili. Khofu, kutaraji, kupenda, kutegemea, kuwa na shauku na kuogopa ni ´ibaadah za kimwili.

Kusema “Subhaan Allaah, Laa ilaaha illa Allaah, Allaahu Akbar, Alhamduli Allaah, kushukuru kwa ulimi na kwa moyo ni ´ibaadah za kimdomo na za kimoyo.

Kuswali, kutoa zakaah, kuhiji na kupambana Jihaad ni ´ibaadah za kimwili na za kimoyo. Ipo mifano mingine mingi ya ´ibaadah zinazopitika kwenye moyo, kwenye mdomo na kwenye viungo vya mwili. ´Ibaadah ndio ambayo viumbe wameumbwa kwa ajili yake. Amesema (Ta´ala):

وَمَا خَلَقْتُ الْجِنَّ وَالْإِنسَ إِلَّا لِيَعْبُدُونِ مَا أُرِيدُ مِنْهُم مِّن رِّزْقٍ وَمَا أُرِيدُ أَن يُطْعِمُونِ إِنَّ اللَّـهَ هُوَ الرَّزَّاقُ ذُو الْقُوَّةِ الْمَتِينُ

“Sikuumba majini na wana Aadam isipokuwa waniabudu. Sitaki kutoka kwao riziki yoyote na wala Sitaki wanilishe. Hakika Allaah ndiye Mwingi wa kuruzuku, Mwenye nguvu madhubuti.”[1]

Akaeleza (Subhaanaha) kwamba hekima ya kuumbwa majini na watu ni kusimama na kazi ya kumwabudu Allaah. Allaah amejitosheleza kutokamana na ´ibaadah zao. Si vyenginevyo isipokuwa wao ndio wenye kuihitajia kwa sababu ya ufakiri wao mbele ya Allaah (Ta´ala). Kwa hivyo wamwabudu Yeye kwa mujibu wa Shari´ah Yake. Kwa hivyo yule mwenye kukataa kumwabudu Allaah ni mwenye kiburi. Mwenye kumwabudu na akabudu pamoja Naye wengine ni mshirikina. Mwenye kumwabudu Yeye pekee kwa yale ambayo hakuyawekea Shari´ah ni mzushi. Mwenye kumwabudu Yeye pekee kwa yale aliyoyawekea Shari´ah ni muumini na mpwekeshaji.

[1] 51:56-58

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ´Aqiydat-ut-Tawhiyd, uk. 56-57
  • Imechapishwa: 25/02/2020