30. Shubuha ya tatu: “Washirikina wa zamani walikuwa hawatamki shahaadah tofauti na sisi” na majibu juu yake

Miongoni mwa shubuha zao ni kwamba wanasema washirikina wa mwanzo hawatamki “hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah”, lakini watu hawa wanaoabudu makaburi, mawalii na waja wema wanasema “hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah”. Vipi mtamfanya yule asiyetamka shahaadah ni sawa na yule mwenye kutamka shahaadah?

Tunawajibu kwa kusema: Allaah ametakasika kutokamana na kasoro zote. Wao ni kweli wametamka shahaadah, lakini wameivunja. Shahaadah haimfai chochote isipokuwa pale ambapo itakuwa imesalimika na vitenguzi vyake. Watu hawa ni kweli wameitamka lakini wameivunja kwa kufanya kwao shirki. Ni nini maana ya hapana mungu isipokuwa Allaah? Maana yake ni kwamba hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah. Watu hawa wanatamka neno hili lakini hawalitendei kazi. Wao wanaabudu makaburi, mawalii, watu wema, makaburi na huku wanatamka “hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah”. Washirikina wa hapo kabla ni wajuzi kuhusu shahaadah kuliko wao. Pindi Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipowaambia: “Semeni ´hapana mungu wa haki isipokuuwa Allaah` walimwambia:

أَجَعَلَ الْآلِهَةَ إِلَـٰهًا وَاحِدًا

“Hivi amewafanya miungu wote kuwa ni mungu Mmoja pekee?” (Swaad 38:05)

Walijua maana ya ´hapana mungu wa haki isipokuuwa Allaah` na kwamba mwenye kuitamka ni lazima aache ´ibaadah zengine zote badala ya Allaah. Watu hawa, kutokana na kwa ujinga na upumbavu wao ni kwamba, wamekusanya baina ya migongano miwili; kutamka kwao kwamba “hapana mwabuidwa wa haki isipokuwa Allaah” na wakati huhuo kumuabudu asiyekuwa Allaah (´Azza wa Jall). Hawakufahamu maana ya shahaadah kama walivyoifahamu washirikina wa hapo kabla. Huu ndio ukomo wa upumbavu. Hapana njia wala namna isipokuwa kwa msaada wa Allaah. Lakini matamanio ndio yanamfanya mtu kutumbukia katika upotevu.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Nawaaqidh-il-Islaam, uk. 52
  • Imechapishwa: 02/08/2018