29. Sharti ya saba ya swalah: Kuingia kwa wakati

Shaykh-ul-Islaam na Imaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Sharti ya saba ni kuingia kwa wakati. Dalili ya hilo ni kutoka katika Sunnah kwenye Hadiyth ya Jibriyl (´alayhis-Salaam) alipomswalisha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) mwanzoni mwa wakati wa swalah na mwishoni wa wakati wake. Akasema:

“Ewe Muhammad! Swalah ni baina ya nyakati hizi mbili.”[1]

Kadhalika Amesema (Ta´ala):

إِنَّ الصَّلاَةَ كَانَتْ عَلَى الْمُؤْمِنِينَ كِتَابًا مَّوْقُوتًا

“Hakika swalah kwa waumini ni fardhi iliyowekewa nyakati maalumu.”

Bi maana imefaradhishwa kwa wakati wake. Dalili ya kuingia kwa wakati wake ni Kauli Yake (Ta´ala):

أَقِمِ الصَّلاَةَ لِدُلُوكِ الشَّمْسِ إِلَى غَسَقِ اللَّيْلِ وَقُرْآنَ الْفَجْرِ إِنَّ قُرْآنَ الْفَجْرِ كَانَ مَشْهُودًا

“Simamisha swalah pale jua linapoanza kupinduka mpaka kiza cha usiku na swalah ya alfajiri; hakika swalah ya alfajiri ni yenye kushuhudiwa.”

MAELEZO

Sharti ya saba… – Swala haisihi kabla ya kuingia kwa wakati wake pasi na tofauti yoyote[2]. Ambaye ataswali kabla ya kuingia kwa wakati wake basi swalah yake ni  batili na haisihi kwa maafikiano ya Ahl-us-Sunnah. Analazimika kuirudi baada ya kuingia kwa wakati wake. Akiswali kabla ya kuingia kwa wakati wake – kwa kusahau kisha baadaye ikambainikia kuwa ameswali kabla ya kuingia kwa wakati – basi analazimika kuirudi upya kwa maafikiano.

Jengine ni kwamba ni lazima kwa waadhini kuhakikisha kuwa wakati umekwishaingia. Kwani hii ni amana. Wasiharakishe kuadhini kabla ya kuingia wakati wake. Muadhini anapata dhambi akiadhini kabla ya wakati mgonjwa au msafiri akaswali kutokana na adhaana yake. Kwa sababu muadhini analazimika kujua ni lini wakati umeingia.

Dalili ya hilo… – Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Jibriyl (´alayhis-Salaam) aliniongoza katika swalah kwenye Nyumba mara mbili ambapo akaniswalisha Dhuhr wakati jua lilipopinduka wakati ambao kivuli cha kila kitu huwa ni kifupi kabisa, kisha akaniswalisha ´Aswr wakati ambao kivuli cha kila kitu kilikuwa kirefu sawia na vitu hivyo, kisha akaniswalisha – bi maana Maghrib – wakati ambao anafungua aliyefunga, halafu akaniliswalisha ´Ishaa mara tu ya kutoweka mwangaza wa siku na kisha akaniliswalisha Fajr wakati ambapo imekatazwa kwa mfungaji kula na kunywa. Ilipofika siku ya pili akaniliswalisha Dhuhr wakati ambapo kivuli cha kila kitu kilikuwa kirefu sawia na vitu hivyo, halafu akaniswalisha ´Aswr pindi ambapo kivuli cha kila kitu kinakuwa na ukubwa mara mbili ya kitu hicho, halafu akaniswalisha Maghrib wakati ambapo anafungua mwenye kufunga, kisha akaniswalisha ´Ishaa wakati ambapo robo theluthi tatu ya usiku imeshapita, halafu akaniliswalisha Fajr wakati ambao mwangaza umekwishaenea. Baada ya hapo akanigeukia na kusema: “Ee Muhammad! Hizi ndio nyakati za Mitume wengine kabla yako na nyakati sahihi ni baina ya mipaka yake miwili.”[3]

Maneno yake:

“Kadhalika Amesema (Ta´ala):

إِنَّ الصَّلاَةَ كَانَتْ عَلَى الْمُؤْمِنِينَ كِتَابًا مَّوْقُوتًا

“Hakika swalah kwa waumini ni fardhi iliyowekewa nyakati maalumu.”

Bi maana imefaradhishwa kwa wakati wake.”

Hiyo ni dalili juu ya kwamba zina nyakati ambapo hazisihi katika nyakati zengine.

Maneno yake:

“Dalili ya kuingia kwa wakati wake ni Kauli Yake (Ta´ala):

أَقِمِ الصَّلاَةَ لِدُلُوكِ الشَّمْسِ إِلَى غَسَقِ اللَّيْلِ وَقُرْآنَ الْفَجْرِ إِنَّ قُرْآنَ الْفَجْرِ كَانَ مَشْهُودًا

“Simamisha swalah pale jua linapoanza kupinduka mpaka kiza cha usiku na swalah ya alfajiri; hakika swalah ya alfajiri ni yenye kushuhudiwa.”

Baadhi ya wanachuoni wamenyofoa hukumu ya nyakati za swalah tano kutoka katika Aayah hii. Shaykh as-Sa´diy (Rahimahu Allaah) amesema:

“Anamwamrisha (Ta´ala) Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kusimamisha swalah kikamilifu kwa uinje na kwa ndani katika nyakati zake. Maneno Yake:

لِدُلُوكِ الشَّمْسِ

“… pale jua linapoanza kupinduka… “

bi maana hali ya kuelekea kupinduka na kuzama baada ya kupindukia. Kwa hivyo katika hilo kunaingia swalah ya Dhuhr na swalah ya ´Aswr. Maneno Yake:

إِلَى غَسَقِ اللَّيْلِ

“… mpaka kiza cha usiku… “

bi maana kiza chake. Kwa hivyo ndani yake kunaingia swalah ya Maghrib na swalah ya ´Ishaa. Maneno Yake:

وَقُرْآنَ الْفَجْرِ

“… na swalah ya alfajiri.”

bi maana swalah ya Fajr. Imeitwa hivo (قُرْآنَ الْفَجْرِ) kutokana na kule kusuniwa kurefusha kisomo cha Qur-aan zaidi kuliko katika swalah nyenginezo na pia kutokana na ubora wa kisomo kwa vile kinashuhudiwa na Allaah na Malaika usiku na mchana.”[4]

[1] Abu Daawuud (393) na tamko ni lake, at-Tirmidhiy (149), Ahmad (3081), Ibn Khuzaymah (325), al-Haakim (17193) na wengineo. Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh Sunan Abiy Daawuud (377).

[2] al-Kaafiy (01/123) ya Ibn-ul-Qayyim.

[3] Abu Daawuud (393) na at-Tirmidhiy (01/333) ambaye amesema:

“Hadiyth ya Ibn ´Abbaas ni Hadiyth nzuri na Swahiyh.”

Ibn Mulaqin amesema:

”Hadiyth hii ndio msingi wenye kutegemewa juu ya maudhui haya.” (al-Badr-um-Muniyr (03/150)).

Ibn Hajar amesema:

”Katika cheni ya wapokezi wake yuko ´Abdur-Rahmaan bin al-Haarith bin ´Ayyaash bin Abiy Rabiy´ah. Wanachuoni wametofautiana juu yake. Lakini ni yenye kusapotiwa kwa nyenginezo.” (at-Talkhiysw-ul-Habiyr (01/173)).

[4] Tafsiyr-us-Sa´diy, uk. 464-465.

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Shuruwt-is-Swalaah, uk. 44-47
  • Imechapishwa: 30/12/2021