30. Ni lazima kwa mume azijue haki za mke

Mume ndio kiongozi wa safina na ndiye msimamizi wa nyumba. Kama jinsi mume ana haki zake vilevile na yeye ana uwajibu. Mume wa Kiislamu anamuabudu Allaah kwa kutimiza haki zake. Anatekeleza haki zake kwa kuwa yeye ndiye mchungaji wake. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Nyote ni wachungaji na kila mmoja ataulizwa kwa kile alichokichunga. Kiongozi ni mchungaji na ataulizwa kwa kile alichokichunga. Mwanaume ni mchungaji wa familia yake na yeye ataulizwa kwa kile alichokichunga. Mwanamke ni mchungaji na yeye ataulizwa juu ya nyumba ya mume wake.”[1]

Mwanaume mwema anajua kuwa ana kazi ya kumchunga mke wake na kwamba ataulizwa juu yake. Ndio maana anafanya juhudi ya kumtakia mema na kumtimizia haki zake. Kwa sababu anajua kufanya hivo ni katika kumcha Allaah. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mcheni Allaah juu ya wanawake.”[2]

Mwanaume mwema anatimiza haki za mke wake zilizo juu yake. Anajua kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameusia hivo na kwa hiyo anaogopa kupuuza wasia ambao kipenzi chake na kiigizo chake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameusia. Kipenzi chetu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Watendeeni wanawake wema.”[3]

Mwanaume mwema alobarikiwa anatekeleza haki za mke wake zilizo juu yake kwa kuwa anajua kuwa yeye [mwanamke] ni amana kwake. Kwa nani? Kwa Allaah, Mola wa mbingu na ardhi. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Watendeeni wanawake wema! Hakika mmewachukua kwa amana [mkataba] wa Allaah… “[4]

Mume Muislamu alobarikiwa hatekelezi haki za mke wake kwa njia ya kutoa huduma. Anafanya hivo kwa sababu ataulizwa juu ya hilo mbele ya Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Kwa ajili hiyo ni lazima kwetu sisi wanaume kujifunza haki za wake zetu na kuwafunza nazo watoto wetu ili tuwe tumetekeleza wajibu ulio kwenye mabega yetu.

[1] al-Bukhaariy (893) na Muslim (1829).

[2] Muslim (1218).

[3] al-Bukhaariy (5186) na Muslim (1468).

[4] Abu Daawuud (1905) na Ibn Maajah (3074).

  • Mhusika: Shaykh Sulaymaan bin Saliym ar-Ruhayliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Haqq-uz-Zawjayn, uk. 45-46
  • Imechapishwa: 24/03/2017