30. Mwenye busara na mapenzi kwa ndugu zake

1- Iwapo Allaah atamruzuku mwenye busara mtu muislamu aliye na mapenzi ya kweli na mwenye kuyachunga, basi analazimika kuyashikamana nayo barabara. Halafu baada ya hapo ajizoweze kumuunga pindi anapoyakata, kumkimbilia pindi anapompa mgongo, kumpa pindi anapomnyima, kumsogelea pindi anapojitenga naye mbali kama kwamba ni nguzo miongoni mwa nguzo zake.

2- Moja katika msiba mkubwa ni mtu kuwa kinyonga katika mapenzi yake.

3- al-Asma´iy amesema:

“Kuna mbedui alisema: “Mtu aliyeshindwa kabisa ni yule mtu asiyeweza kuwafuta ndugu. Ambaye ameshindwa zaidi ni yule aliyekuwa na ndugu kisha akayapoteza mapenzi yao. Yule mwenye kujifanyia mwenyewe vizuri ndiye awafanyiaye vizuri wengine.”

4- Mwenye busara hazembei kuyachunga mapenzi.  Hawi mwenye rangi mbili wala mioyo miwili. Undani wake ni kama uinje wake. Maneno yake yanaafikiana na matendo yake. Hakuna kheri kati ya ndugu wawili ambao kasoro zao zinazidi na makosa yao yanaongezeka.

5- Yahyaa bin Abiy Kathiyr ameeleza kuwa Sulaymaan (´alayhis-Salaam) alisema kumwambia mwanawe:

“Ee mwanangu kipenzi! Shikamana na yule kipenzi wa kwanza. Mwingine hawi kama yule wa kwanza.”

6- Mwenye busara hajengi urafiki na mtu mwenye rangi nyingi na wala hejengi udugu na mtu kigeugeu. Haonyeshi mapenzi isipokuwa yale alionayo ndani yake. Hata hivyo kwa ndani anakuwa na mapenzi zaidi kuliko yale anayoonyesha. Wakati kunapotokea majanga anakuwa kama alivyokuwa kabla ya majanga hayo kutokea. Kwa sababu hakuna ndugu anayesifiwa isipokuwa aliye namna hii.

7- Hishaam bin ´Urwah ameeleza kuwa baba yake amesema:

“Katika vitabu vya kale kumeandikwa: “Mpende rafiki yako na rafiki wa baba yako.”

8- Moja katika alama kubwa za kujua mapenzi ya kweli na mapenzi yasiyokuwa ya kweli ni mtazamo wa jicho. Jicho linapotazama linakaribia kutoficha mapenzi isipokuwa yale yaliyomo ndani ya moyo. Moyo unakaribia kutoficha ule woga uliyomo ndani ya moyo. Mwenye busara anayazingatia mapenzi kupitia moyo wake na kupitia macho ya nduguye.

9- Ibraahiym bin Shiklah amesema:

“Tambua kwamba mtu akikuonyesha kile unachokipenda au unachokichukia basi uchukulie moyo wake kwa kile anachosema mdomoni mwake. Huhitajii kuyajua yale anayoficha moyoni mwake. Kwa hivyo mchukulie kwa vile anavyokuonyesha mdomoni mwake.

10- Ibraahiym al-Jahniy amesema:

“Dalili ya mapenzi utayaona kwa mtu anayekupenda hata kama ulimi wake hausemi kuwa anafanya hivo.”

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Hibbaan al-Bustiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Rawdhat-ul-´Uqalaa’ wa Nuzhat-ul-Fudhwalaa’, uk. 103-107
  • Imechapishwa: 15/04/2018