30. Mtazamo wa wapotevu juu ya kumuamini Allaah na siku ya Mwisho

Mfumo wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), Maswahabah zake na wale wenye kuwafuata kwa wema ni Njia iliyonyooka sawa kiujuzi na kimatedo. Haya anayajua kila ambaye anadurusu hilo kwa elimu na kiuadilifu. Walikuwa na mtazamo sahihi juu ya kumuamini Allaah na siku ya Mwisho na wakakubali kwamba ni haki. Matendo yao yalikuwa yenye kufanywa kwa ajili ya Allaah pekee na wakifuata Shari´ah Yake. Walikuwa hawashirikishi, hawazushi, hawapotoshi wala hawakadhibishi.

Kuhusu wale wapotofu ambao wameacha mfumo wao, wanagawanyika makundi matatu: kundi lililofuata mawazo, kundi lililofuata tafsiri za kimakosa na kundi lenye kuonelea kuwa wengine ndio wajinga.

Ama kuhusu kundi linalofuata mawazo (Ahl-ut-Takhyiyl), ni wanafalsafa, Baatwiniyyah na wale waliowafuata katika wanafalsafa na wengineo. Wanaonelea kuwa ujumbe wa Mitume juu ya kuamumini Allaah na siku ya Mwisho ni ndoto na mawazo yasiyokuwa na uhakika wowote katika uhalisia. Makusudio ya ujumbe ni kuwanufaisha watu wajinga na wengi katika watu. Watu wakielezwa kuwa wana Mola mkubwa ambaye ni muweza, mwenye huruma na mwenye nguvu na kwamba mbele yao wana siku kubwa ambapo ndani yake watafufuliwa na kulipwa kwa ajili ya matendo yao, basi watanyooka juu ya njia ya sawa hata kama ni mambo ya kubuni.

Watu hawa wamegawanyika makundi mawili; waliopindukia na ambao hawakupindukia.

Wale waliopindukia wanamaanisha kuwa Mitume hawajui uhakika wa mambo haya tofauti na wanafalsafa wa kiungu na wanaodaiwa kuwa ni mawalii. Wanadai kwamba wanafalsafa ni watambuzi zaidi juu ya Allaah na siku ya Mwisho kuliko Mitume ambao uhakika wa mambo wao ndio wajuzi zaidi katika mambo haya.

Wale ambao hawakupindukia wanaonelea kuwa Mitume kweli wanajua uhakika wa mambo haya, lakini kwamba waliwaambia watu mambo ya ndoto kwa ajili ya maslahi yao. Wanadai kwamba maslahi ya waja yanapatikana tu kwa njia kama hii jambo ambalo lina maana kwamba Mitume walisema uongo juu ya mambo ambayo ni makubwa na ya yenye umuhimu zaidi.

Kwa hivyo kundi la kwanza limewahukumu Mitume kuwa ni wajinga. Kundi la pili limewahukumu kuwa ni wafanya khiyana na ni waongo. Hii ndio ´Aqiydah yao juu ya kumuamini Allaah na siku ya Mwisho.

Kuhusiana na matendo, kuna ambao wanaonelea kuwa ni ya kihakika na kwamba kila mmoja ni lazima kuyatekeleza. Wengine wanayafanya kuwa ni ndoto tu na nembo wanazoamrishwa watu wajinga tofauti na wale wasomi. Kwa hivyo wanasema kuwa swalah maana yake ni kuwa na ujuzi juu ya siri zao, maana ya swawm ni kuzifichika, hajj maana yake ni kusafiri kwenda kwa wanachuoni wao na mfano wa hayo. Watu hawa ni wale wakanamungu kati ya Ismaa´iyliyyah, Baatwiniyyah na wengineo. Ubatilifu wa maoni ya watu hawa unathibitishwa kilazima na hisia, akili na Shari´ah. Sisi tunaona alama nyingi juu ya uwepo wa Allaah na ukamilifu wa sifa Zake:

Katika kila kitu Anayo alama

Inayojulisha kuwa Yeye ni Mmoja

Matokeo haya yaliyoko kimpangilio hayawezi kutoka kwa mwengine asiyekuwa mwendeshaji wa mambo, mwenye hekima na ambaye ni muweza juu ya kila kitu.

Shari´ah zote zimethibitisha kuamini siku ya Mwisho. Hekima ya Allaah ya hali ya juu imepelekea vilevile juu ya jambo hilo. Haya hayakanushwi na yeyote isipokuwa mtu mkaidi au mwendawazimu. Watu sampuli hii hawahitajii kuraddiwa sana. Ni jambo lenye kujulikana kuwa watu wanawakimbia.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fath Rabb-il-Bariyyah, uk. 78-80
  • Imechapishwa: 11/05/2020