30. Mlango kuhusu kuomba kunyeshewa mvua kwa sayari


Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

1- Allaah (Ta´ala) amesema:

وَتَجْعَلُونَ رِزْقَكُمْ أَنَّكُمْ تُكَذِّبُونَ

”… na mnafanya shukurani za riziki yenu kuwa nyinyi mnakadhibisha.” (al-Waaqi´ah 56:82)

2- Abu Maalik al-Ash´ariy (Radhiya Allaahu ´anhu) ameeleza kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mambo mane katika Ummah wangu ni miongoni mwa mambo ya kipindi cha kikafiri na hawatoyaacha; kujifakhari kwa unasabu, kutukaniana nasabu, kuinasibisha mvua kwa nyota na kuomboleza.”

Vilevile amesema:

“Mwanamke mwenye kuomboleza ikiwa hakutubia kabla ya kufa kwake, basi atafufuliwa siku ya Qiyaamah na huku akiwa amevishwa nguo ya shaba iliyoyeyuka na kanzu ya ukoma.”[1]

Ameipokea Muslim.

3- al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kupitia kwa Zayd bin Khaalid (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye ameeleza:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alituswalisha swalah ya Fajr Hudaybiyah baada ya mvua iliyonyesha usiku. Alipomaliza kuswali akawaelekea watu na akasema: “Je, mnajua nini Kasema Mola wenu?” Wakasema: “Allaah na Mtume wake ndio wanajua zaidi.” Akasema: “Katika asubuhi hii kuna baadhi ya waja Wangu wamepambaukia wakiwa ni wenye kuniamini na wengine wamekufuru. Ama yule aliyesema kwamba: “Tumenyeshewa mvua kwa fadhila na rehema ya Allaah”, basi huyo ndiye aliyeniamini Mimi na amekufuru sayari. Ama yule aliyesema ya kwamba tumenyeshewa mvua kutokana na sayari fulani na fulani, basi huyo amenikufuru Mimi na ameamini sayari.”[2]

Imepokelewa na al-Bukhaariy na Muslim.

4- al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kupitia kwa Ibn ´Abbaas upokezi wenye maana kama hio na ndani yake imekuja:

“Baadhi yao wamesema: “Sayari fulani imesema kweli.” Ndipo Allaah akateremsha Aayah ifuatayo:

فَلَا أُقْسِمُ بِمَوَاقِعِ النُّجُومِ وَإِنَّهُ لَقَسَمٌ لَّوْ تَعْلَمُونَ عَظِيمٌ إِنَّهُ لَقُرْآنٌ كَرِيمٌ فِي كِتَابٍ مَّكْنُونٍ  لَّا يَمَسُّهُ إِلَّا الْمُطَهَّرُونَ تَنزِيلٌ مِّن رَّبِّ الْعَالَمِينَ أَفَبِهَذَا الْحَدِيثِ أَنتُم مُّدْهِنُونَ وَتَجْعَلُونَ رِزْقَكُمْ أَنَّكُمْ تُكَذِّبُونَ

“Basi Naapa kwa maangukio ya nyota – na hakika hicho ni kiapo kikubwa mno, lau mngelielewa! – hakika hii bila shaka ni Qur-aan karimu, katika Kitabu kilichohifadhiwa, hakuna akigusaye isipokuwa waliotakaswa, ni uteremsho kutoka kwa Mola wa walimwengu! Je, kwa maneno haya nyinyi ni wenye kuitweza na kuikanusha na mnafanya shukurani za riziki yenu kuwa nyinyi mnakadhibisha… ” (al-Waaqi´ah 56:75-82)

MAELEZO

Allaah ameweka katika Shari´ah kuomba kunyeshewa mvua. Kuomba kunyeshewa mvua maana yake ni kunyenyekea mbele ya Allaah wakati wa ukame. Washirikina wao hawafanyi hivo ambao wanaziomba nyota kuwanyeshea mvua, kufungamana nazo na kuziomba msaada. Walikuwa wakiziomba nyota kuwateremshia mvua. Nyota ndio sayari. Mwezi na jua vinaizunguka. Mwezi unaenda kwa mwezi na jua linaenda kwa mwaka. Wakati wa kipindi cha kikafiri walikuwa wakifungamana navyo na wakiviomba msaada. Hili ni kutokana na shirki na upotevu wao.

1- Allaah (Ta´ala) amesema:

وَتَجْعَلُونَ رِزْقَكُمْ أَنَّكُمْ تُكَذِّبُونَ

”… na mnafanya shukurani za riziki yenu kuwa nyinyi mnakadhibisha.”

Wanakadhibisha kwamba ni Allaah ndiye ameteremsha mvua na kukunyweshelezeni. Badala yake mnaziomba nyota na kuzitaka msaada. Ndipo Allaah akawakadhibisha, kwa sababu nyota hizi hazinufaishi, hazidhuru na wala hazimiliki kitu katika mambo hayo. Kwa hivyo ni wajibu kwa waumini kuamini yale aliyoeleza Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), kushikamana nayo na kujiepusha na matendo ya kipindi cha kikafiri. Mfano miongoni mwa matendo yao ni:

2- Abu Maalik al-Ash´ariy (Radhiya Allaahu ´anhu) ameeleza kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mambo mane katika Ummah wangu ni miongoni mwa mambo ya kipindi cha kikafiri na hawatoyaacha; kujifakhari kwa unasabu, kutukaniana nasabu, kuinasibisha mvua kwa nyota na kuomboleza.”

Watu wataendelea kuyafanya mambo haya na kuwaiga makafiri ikiwa ni pamoja na:

1- Kujifakhari kwa unasabu. Ina maana kwamba mtu akajifakhari kwamba baba yake ni fulani, akajikweza kwa hilo na akatumia hoja juu ya batili yake na kujifakharisha kwa wengine. Unasabu ni yale waliokuwa nayo mababu kama vile athari, ushujaa, wingi wa kutoa na ukarimu. Hii ni sifa ya wakati wa kipindi cha kikafiri. Mtu anakuwa juu kutokamana na matendo yake na si kwa matendo ya wengine.

2- Kutukaniana nasabu. Ina maana kwamba mtu akamtukana mwengine kwa sababu ni fundi seremala, mshumaji, anazungumza kwa njia ya kumtweza. Ama akizungumza kwa njia ya kuelezea hakuna neno.

3- Kuinasibisha mvua kwa nyota. Ima anasema kuwa tumepata mvua kwa sababu ya nyota fulani au mtu anaiomba moja kwa moja.

4- Kuomboleza. Pindi maiti anapokufa basi wanapiga ukelele, wanachana nguo,  wanakokota nywele zao na kujirushia udongo usoni. Haya yote yanafanywa na baadhi ya waislamu. Ni wajibu kutahadhari nayo na kukipiga vita kitendo hichi. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa salllam) amesema:

“Si katika sisi yule mwenye kujipiga mashavu, akachana nguo au akaita kwa wito wa kipindi cha kikafiri.”[3]

Amesema vilevile:

“Mimi niko mbali kabisa na mwanamke anayenyanyua sauti yake, mwenye kuzinyoa nywele zake na  mwenye kuzipasua nguo zake wakati wa msiba.”[4]

Vilevile amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa salllam):

“Mwanamke mwenye kuomboleza ikiwa hatotubia kabla ya kufa kwake, basi atafufuliwa siku ya Qiyaamah na huku akiwa amevishwa nguo ya shaba iliyoyeyuka na kanzu ya ukoma.”

Mara nyingi wanawake ndio wenye kuomboleza. Ndio maana (Swalla Allaahu ´alayhi wa salllam) amemtaja mwanamke. Inawezekana vilevile mwanaume akaomboleza. Kuomboleza kumeharamishwa kwa wanaume na kwa wanawake wote wawili. Imetajwa nguo ya shaba iliyoyeyuka kwa sababu apate adhabu yenye kuumiza kwelikweli. Kadhalika kanzu ya ukoma kwa sababu ya maudhi. Haya yanaonyesha ubaya wa mwisho wake ikiwa hatotubia.

Masuala: Ni sawa kwa mtu kumuoa mwanamke mwenye dini asiyetokamana na familia yenye kabila tukufu ikiwa mwanaume huyo anachelea watu wake wasije kumuudhi. Kwa sharti asiwe amewaacha kwa sababu ya kuwatweza na kuwadharau.

Faida: Baadhi ya vijiji wanachinja vichinjwa juu kwenye vilele vya milima ili waweze kupata mvua. Hii ni shirki kubwa kwa sababu ni kuwachinjia majini, mawe na masanamu. Huenda kweli wakanyeshewa na mvua, inakuwa ni majaribio kwao.

3- al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kupitia kwa Zayd bin Khaalid (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye ameeleza:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alituswalisha swalah ya Fajr Hudaybiyah baada ya mvua iliyonyesha usiku. Alipomaliza kuswali akawaelekea watu na akasema: “Je, mnajua nini Kasema Mola wenu?” Wakasema: “Allaah na Mtume wake ndio wanajua zaidi.” Akasema: “Katika asubuhi hii kuna baadhi ya waja Wangu wamepambaukia wakiwa ni wenye kuniamini na wengine wamekufuru. Ama yule aliyesema kwamba: “Tumenyeshewa mvua kwa fadhila na rehema ya Allaah”, basi huyo ndiye aliyeniamini Mimi na amekufuru sayari. Ama yule aliyesema ya kwamba tumenyeshewa mvua kutokana na sayari fulani na fulani, basi huyo amenikufuru Mimi na ameamini sayari.”

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anapomaliza kuswali alikuwa na mazowea ya kumuomba Allaah msamaha mara tatu kisha anasema:

اللَّهُمَّ أَنْتَ السَّلاَمُ وَمِنْك السَّلاَمُ تَبَارَكْتَ يَا ذَا الْجَلاَلِ وَالإِكْرام

“Ee Allaah! Hakika Wewe ni mkamilifu usiyokuwa na mapungufu na amani inatoka Kwako. Umetukuka, ee Mwenye utukufu na ukarimu.”

Halafu anawaelekea watu na anasoma adhkaar zilizobaki.

Watu wakasema:

“Allaah na Mtume wake ndio wanajua zaidi.”

Hii ilikuwa ni katika adabu waliokuwa nayo Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum). Baada ya kufa kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) inatakiwa kusema “Allaah ndiye anajua zaidi” peke yake. Kwa sababu Wahy umekatika. Yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hajui yanayoendelea baada ya kufa kwake. Dalili ya hilo ni Hadiyth ya hodhi. Isipokuwa tu yale anayoonyeshwa na Allaah kama pale anaposwaliwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

“…  basi huyo ndiye aliyeniamini Mimi na amekufuru sayari.”

Kwa sababu ametambua kuwa Allaah ndiye kateremsha mvua. Mvua hii inatokamana na rehema na fadhilah za Allaah.

Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

“Ama yule aliyesema ya kwamba tumenyeshewa mvua kutokana na sayari fulani na fulani, basi huyo amenikufuru Mimi na ameamini sayari.”

Ni aina ya kufuru. Haitakiwi kusema sayari fulani ilisema kweli au kwamba tumepata mvua kwa sababu ya sayari fulani. Bali kinachotakiwa kusema ni:

“Tumenyeshewa mvua kwa fadhila na rehema ya Allaah.”

Mwenye kusema kuwa tumepata mvua kwa sababu ya sayari fulani na wakati huohuo anamaanisha kwamba sayari ndio imeumba mvua na kuiendesha, basi hiyo ni kufuru kubwa. Ama ikiwa anamaanisha kuwa sayari hiyo ni sababu iliopelekea katika kupata mvua, basi hiyo ni kufuru ndogo kwa sababu anaona kuwa Allaah (Ta´ala) ndiye kaumba mvua na sio sayari. Nyota hutokea kwa matukio kama vile michana na nyusiku vinavyotokea kwa matukio. Hata hivyo mtu akisema kwa mfano kwamba wakati wa kipwa tulipata mvua hakuna neno kwa sababu huku ni kueleza tu yaliyotokea katika wakati. Kwa hivyo ni wajibu kutahadhari na tabia hizi za kipindi cha kikafiri na kuzitambua neema za Allaah (Subhaanah) kwa moyo.

[1] Muslim (934).

[2] al-Bukhaariy (1038) na Muslim (71).

[3] al-Bukhaariy (1294) na Muslim (103).

[4] al-Bukhaariy kwa cheni ya wapokezi iliopungua na Muslim (104).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kitaab-it-Tawhiyd, uk. 102-104
  • Imechapishwa: 18/10/2018