30. Kuzungumza kwa Allaah na waumini siku ya Qiyaamah

Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) amesema:

“Inatakiwa kuamini kuwa Allaah atawazungumzisha waja siku ya Qiyaamah, hakuna baina yao na baina Yake mkalimani. Hili linatakiwa kuaminiwa na kusadikishwa.”

MAELEZO

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakuna yeyote katika nyinyi isipokuwa Mola Wake atamzungumzisha bila ya kuwepo baina yake na baina Yake mkalimani.”[1]

Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) ataita siku ya Qiyaamah:

وَيَوْمَ يُنَادِيهِمْ أَيْنَ شُرَكَائِي قَالُوا آذَنَّاكَ مَا مِنَّا مِن شَهِيدٍ وَضَلَّ عَنْهُم مَّا كَانُوا يَدْعُونَ مِن قَبْلُ ۖ وَظَنُّوا مَا لَهُم مِّن مَّحِيصٍ

“Siku Atakayowaita: “Wako wapi [sasa hao] washirika Wangu?”  – watasema wakijibu: “Tunakiri Kwako hapana miongoni mwetu anayeshudia [kwamba wapo].” Yatawapotea yale waliyokuwa wakiyaomba kabla na watayakinisha hawana mahali pa kukimbilia.”[2]

وَيَوْمَ يُنَادِيهِمْ فَيَقُولُ أَيْنَ شُرَكَائِيَ الَّذِينَ كُنتُمْ تَزْعُمُونَ

“Siku Atakayowaita na aseme: “Wako wapi hao washirika Wangu mliokuwa mkinishirikisha nao?”[3]

Wito hauwi isipokuwa kwa herufi na sauti. Wito ni maneno. Atanadi kwa watu wa Peponi:

“Mmeridhika? Niwapeni zaidi?”[4]

Atazungumza na kuongea. Atamzungumzisha (Subhaanahu wa Ta´ala) mmoja baada ya mwingine pasi na mkalimani. Atawazungumzisha watu wote. Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) siku zote anasifika na ukamilifu huu. Hii ni miongoni mwa sifa Zake (Tabaarak wa Ta´ala) kamilifu ya kwamba anazungumza na watu siku ya Qiyaamah kama Alivyozungumza na Muusa, Muhammad, Jibriyl na Malaika (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam). Makusudio ni kwamba Atazungumza na waumini siku ya Qiyaamah.

[1] al-Bukhaariy (6539) na Muslim (1016).

[2] 41:47-48

[3] 28:62

[4] Muslim (181).

  • Mhusika: ´Allaamah Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Usuwl-is-Sunnah, uk. 392
  • Imechapishwa: 26/08/2017