31. Kujigonga kwa Ahl-ut-Ta´wiyl na kuharibika kwa akili yao

Kuhusu wale waliofuata tafsiri za kimakosa (Ahl-ut-Ta´wiyl), ni wale wanafalsafa katika Jahmiyyah, Mu´tazilah na wafuasi zao.

Mfumo wao ni kwamba maandiko kuhusu sifa ambayo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekuja nayo ni majazi na hayafahamiki kama yalivyo kidhahiri. Makusudio yake ni maana inayotofautiana na udhahiri. Yanatambua Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), lakini aliwaachia watu wayafikirie na kufikia malengo yake. Halafu wanajaribu kuyafasiri kwa kutumia yale maandiko ya dhahiri. Lengo la kufanya hivo ni kupima akili ya kiuanadamu na thawabu nyingi zinazopatikana kwa kuyafahamu maneno kimajazi kupitia vipengele visivyo vya kawaida, vya ajabu na vya kilugha.

Hakuna watu waliochanganyikiwa na wenye kujigonga zaidi kama watu hawa. Kwa sababu hawana msingi imara wanaosimamia ili kujua ni kipi kinachotakiwa kufasiriwa na kipi kisichofasiriwa na namna ambavyo maana mpya na ilioteuliwa inavyotakiwa kuwa. Mara nyingi mtu hujua zile maana ambazo wanafalsafa wanajaribu kufikia, sizo ambazo zilizokusudiwa katika yale mazingira ambayo yeye amefasiri kimakosa.

Watu hawa hujidhihirisha kuwa ni wenye kuinusuru Sunnah na hujificha nyuma ya matamshi kwamba wanamtakasa Allaah kutokamana na mapungufu. Hata hivyo Allaah amewafedhehesha kwa kuraddi utata wao na kuziponda hoja zao. Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah na wengineo wamewaraddi zaidi kuliko wengine kwa sababu wengi wao huhadaika nao kwa kuwa wao wanajidhihirisha kuwa ni wenye kuinusuru Sunnah.

Kuhusu mtazamo wao juu ya siku ya Mwisho ni kwamba ni wenye kuyaamini pasi na kuyafasiri kimakosa. Pindi ilipokuwa ni wenye kuyafasiri kimakosa maandiko ya sifa na kuyatoa nje ya uhakika na kuyapeleka katika majazi yanayopingana na udhahiri wake, wakashambuliwa na wale wenye kutegemea mawazo. Wakawalazimisha wayafahamu maandiko yanayozungumzia Aakhirah kama walivyofanya juu ya maandiko ya sifa. Ndipo wakasema wale wenye kufasiri maandiko kimakosa:

“Tunajua fika kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alithibitisha siku ya Mwisho. Tunajua kuwa utata unaosema kinyume ni batili. Hivyo ni lazima Qiyaamah kitokee.”

Hili ni jibu sahihi na hoja ya kihakika. Linajumuisha ndani yake mtu kuwatetea kwa sababu ya kutokufasiri maandiko yanayozungumzia siku ya Mwisho kimakosa vilevile pamoja na kuwalazimisha wale wengine waamini siku ya Mwisho na kuyafahamu maandiko kama yalivyo. Kukiwepo dalili na kusiwepo vikwazo, basi ni lazima kuthibiti kile chenye kinachofahamishwa.

Ahl-us-Sunnah wametumia hoja hii hii dhidi ya Ahl-ut-Ta´wiyl ili na wao vilevile wathibitishe Aayah zinazozungumzia sifa na kuzielewa kama jinsi zilivyo. Na wao wakawaambia:

“Tunajua fika kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimthibitishia Allaah sifa. Tunajua kuwa utata unaosema kinyume ni batili. Hivyo ni lazima zithibitishwe.”

Malazimisho haya ni sahihi na ni hoja iliyosimama barabara ambapo Ahl-ut-Ta´wiyl hawana pa kukwepea. Ambaye haruhusu maandiko yanayozungumzia siku ya Mwisho yakafasiriwa kimakosa, basi vilevile asiruhusu mtu akayafasiri maandiko yanayozungumzia sifa ambayo yamethibitishwa zaidi katika vitabu vya kiungu kuliko ambavyo siku ya Mwisho ilivyothibitishwa. Endapo atafanya hivo, basi kujigonga na kuharibika kwa akili yake.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fath Rabb-il-Bariyyah, uk. 78-80
  • Imechapishwa: 11/05/2020