Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) amesema:

Inatakiwa kuamini adhabu ya kaburi na kwamba ummah huu utapewa mtihani katika makaburi yao. Wataulizwa juu ya imani na Uislamu na ni Mola na Mtume wao? Munkar na Nakiyr watamwendea yule maiti kama anavyotaka Allaah (´Azza wa Jall). Yanatakiwa kuaminiwa na kusadikishwa”

MAELEZO

Miongoni mwa ´Aqiydah za Ahl-us-Sunanh wal-Jamaa´ah ni kuamini neema za ndani ya makaburi ya waumini na adhabu kwenye makaburi ya makafiri, wanafiki na waislamu watenda madhambi. Neema watazopata waumini ndani ya makaburi yao ni jambo la kweli. Adhabu watayopata watenda madhambi ndani ya makaburi yao ni jambo la kweli. Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) ndiye kakadiria hilo, Anakifanya akitakacho na Anahukumu atakavyo.

Kaburi ima ni bustani miongoni mwa mabustani ya Peponi au shimo miongoni mwa mashimo ya Motoni, kwa kutegemea na namna mtu alivyotenda hapa duniani. Imepokelewa ya kwamba kaburi la muumini litapanuliwa kiasi cha upeo wa macho, atavishwa mavazi ya Peponi, atafunguliwa mlango wa Peponi na kwamba ataambiwa alale. Pindi atakapoona neema hizo atamuomba Allaah alete Qiyaamah. Hata hivyo waumini watapata neema kubwa zaidi huko Aakhirah.

Ndani ya kaburi ataadhibiwa kafiri, mnafiki na baadhi ya waislamu watenda madhambi wataadhibiwa kwa kiwango cha madhambi yao. Wataadhibiwa ndani ya kaburi na huko Aakhirah. Baada ya Allaah kuwarehemu na waombezi kuombea, ndipo wataingia Peponi.

Imethibiti ya kwamba mtenda dhambi atapoulizwa: “Ni nani Mola wako? Ni nani Mtume wako? Ni ipi dini yako?” Atasema: “Aah, sijui. Niliwasikia watu wakisema kitu nami nikasema.” Ataambiwa: “Hukujua na wala hukutaka kujua.” Kisha atapigwa chuma mpaka awe udongo. Kisha atapewa uhai na kupigwa tena kiasi cha kwamba atapiga ukelele utaosikiwa na kila kiumbe isipokuwa tu watu na majini. Lau wangelimsikia basi wangelikufa, kama yalivyothibiti kupokelewa[1].

Hivi ndivo wanavyoamini Ahl-us-Sunanh wal-Jamaa´ah, kundi lililooloka na lililonusuriwa, juu ya neema na adhabu za ndani ya kaburi mpaka kisimame Qiyaamah huko Aakhirah. Huko ndiko neema za waumini zitakuwa kubwa zaidi na adhabu za makafiri zitakuwa kubwa zaidi. Rehema ya Allaah imekienea kila kitu. Allaah (Subhaanah) amewaandikia rehema Yake iwazunguke waja wapwekeshaji japokuwa wametenda dhambi. Kama kama wataadhibiwa kwa kitu kwa ajili ya kuwasafisha, mwanzo au mwishoni wataingia Peponi.

Mu´tazilah na Khawaarij wamepinga adhabu na neema za ndani ya kaburi. Kwa sababu hawaamini Hadiyth zilizopokelewa kwa mapokezi ya njia moja katika mambo yanayohusu ´Aqiydah. Wanatendea kazi Qur-aan tu na Sunanh zilizopokelewa kwa mapokezi mengi. ´Aqiydah hii ni mbovu na maneno ya batili. Ahl-us-Sunnah wanatendea kazi yale yote yaliyothibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), ni mamoja yamepokelewa kwa mapokezi mengi au kwa njia moja, katika mambo yanayohusiana na ´Aqiydah na mengine yote ya dini. Kitu muhimu andiko liwe limethibiti kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), ijapokuwa litakuwa limepokelewa kwa njia moja.

[1] al-Bukhaariy (1374) na Muslim (2871).

  • Mhusika: ´Allaamah Zayd bin Muhammad al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Latwiyfah ´alaa Usuwl-is-Sunnah al-Muniyfah, uk. 87-88
  • Imechapishwa: 15/10/2019