7 –  Mwanamke akiwa peke yake basi atapanga safu peke yake nyuma ya wanaume. Hayo ni kutokana na Hadiyth ya Anas (Radhiya Allaahu ´anh) wakati Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipowaswalisha akasimulia:

“Nilisimama mimi na yatima nyuma yake na akasimama bitikizee nyuma yetu.”

Wameipokea kundi isipokuwa Ibn Maajah.

Anas ameeleza:

“Mimi na yatima tulikuwa nyumbani kwetu nyuma ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na mama yangu – Umm Sulaym – alikuwa nyuma yetu.”

Ameipokea al-Bukhaariy.

Ikiwa wamehudhuria wanawake zaidi ya mmoja basi watapanga safu moja au safu nyingi nyuma ya wanaume. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiwatanguliza wanaume mbele ya watoto, watoto nyuma yao na wanawake nyuma ya watoto[1].

Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Safu bora za wanaume ni zile za mwanzoni na safu bora za wanawake ni zile za mwishoni na ovu zao ni zile za mwanzoni.”

Wameipokea kundi isipokuwa al-Bukhaariy.

Katika Hadiyth mbili hizo kuna dalili inayoonyesha kuwa safu za wanawake zinatakiwa kuwa nyuma ya wanaume na wala wasiswali hali ya kufarikiana endapo wataswali nyuma ya wanaume. Ni mamoja ni swalah ya faradhi au swalah ya Tarawiyh.

8 – Imamu akisahau katika swalah basi mwanamke anatakiwa kumzindua kwa kupiga makofi kwa ndani ya kitanga chake juu ya kingine. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Likikupateni jambo lolote katika swalah basi wanaume waseme “Subhaan Allaah” na wanawake wapige makofi.”

Hii pia ni idhini ya wao kupiga makofi katika swalah wakati wa kuzindua na pale imamu anaposahau. Hayo ni kwa sababu sauti ya wanawake ina fitina kwa wanaume. Hivyo akaamrishwa kupiga makofi na asizungumze.

9 – Imamu anatoa salamu wanawake watakimbilia kutoka msikitini na wanaume watabaki wakiwa wamekaa ili wasikutane na wale wataokuwa wameondoka katika wao. Umm Salamah amesimulia:

“Kulipokuwa kunatolewa salamu ya swalah ya faradhi basi wanawake walikuwa wakisimama na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anabaki na wale wanaume walioswali muda anaotaka Allaah. Pale ambapo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anaposimama na wanaume pia husimama.”

az-Zuhriy amesema:

“Tunaona hilo – na Allaah ndiye mjuzi zaidi – ni kwa sababu wamalizike wale wanawake walioondoka.”[2]

Imaam ash-Shawkaaniy amesema katika “Nayl-ul-Awtwaar”:

“Katika Hadiyth tunafaidi kwamba imependekezwa kwa imamu kuchunga hali za maamuma, kuhakikisha kuepuka yanayoweza kupeleke katika makatazo, kujiepusha na zile sehemu za tuhuma machukizo ya wanaume kuchanganyikana na wanawake katika mabarabara sembuse kwenye majumba.”[3]

Imaam an-Nawawiy (Rahimahu Allaah) amesema katika “al-Majmuu´”:

“Wanawake wanawakhalifu wanaume juu ya swalah ya mkusanyiko katika mambo kadhaa:

a) Haikusisitizwa juu yao kama ilivyosisitizwa kwa wanaume.

b) Imamu wao atasimama katikati yao.

c) Mmoja wao atasimama nyuma ya wanaume na si pambizoni mwake tofauti na mwanaume.

d) Wakiswali safu nyingi pamoja na wanaume basi zile safu za mwisho ndio bora kuliko zile safu za mwanzo.”[4]

Kutokana na yaliyotangulia inapata kujulikana uharamu wa kuchanganyikana kati ya wanaume na wanawake.

[1] Ameipokea Ahmad.

[2] Ameipokea al-Bukhaariy. Tazama “ash-Sharh al-Kabiyr ´alaa al-Muqniy´ (01/442).

[3] (02/326).

[4] (03/455).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tanbiyhaat, uk. 60-61
  • Imechapishwa: 05/11/2019