30. Allaah ana sifa za kidhati na za kimatendo


Imaam Ibn Abiy Daawuud (Rahimahu Allaah) amesema:

10- Jahmiy anaweza vilevile kupinga mkono Wake wa kuume

     mikono Yake yote miwili kwa fadhila ni mikunjufu

MAELEZO

Jahmiy ni ambaye yuko katika madhehebu ya Jahmiy bin Swafwaan. Mtu huyu alichukua madhehebu yake kutoka kwa Ja´d bin Dirham.

Jahmiy anaweza… – Bi maana wafuasi wa Jahmiy wanapinga majina na sifa. Haya ni moja katika madhehebu yake machafu. Vinginevyo ana madhehebu machafu katika mambo mengi. Miongoni mwa mambo hayo ni kupinga majina na sifa.

… anaweza… – Bi maana hakika. Ni kama mfano wa kusema “hakika wakati wa swalah umewadia”. Ni kama mfano wa maneno Yake (Ta´ala):

لَّقَدْ سَمِعَ اللَّـهُ قَوْلَ الَّذِينَ قَالُوا إِنَّ اللَّـهَ فَقِيرٌ وَنَحْنُ أَغْنِيَاءُ ۘ سَنَكْتُبُ مَا قَالُوا

“Hakika Allaah ameyasikia maneno ya wale waliosema: “Hakika Allaah ni fakiri na sisi ni matajiri.” Tutayaandika waliyoyasema.”” (03:181)

“Inaweza” (Qad) wakati mwingine inakuja ikiwa na maana ya hakika. Hayo ndio makusudio hapa. Wakati mwingine inaweza kuja kwa maana ya pengine. Kama kusema “bakhili anaweza kuwa mkarimu”. Hapa imekuja kwa maana ya pengine. Lakini iliyokuja hapa sio kwa njia ya pengine. Bali ni kwa njia ya hakika. Ni kama mfano wa maneno Yake (Ta´ala):

قَدْ يَعْلَمُ اللَّـهُ الْمُعَوِّقِينَ

“Hakika Allaah ameshajua wenye kuweka kizuizi.” (33:18)

Hii imekuja kwa njia ya kuyakinisha.

… vilevile… – Bi maana kama ambavyo wamekanusha Kuonekana kwa Allaah (´Azza wa Jall), kadhalika wanapinga kumthibitishia Allaah kuwa na mikono miwili.

Allaah (´Azza wa Jall) ana sifa za kidhati. Kama mfano wa mikono miwili, uso, miguu na vidole. Kadhalika Ana sifa za kimatendo. Kama mfano wa kushuka, kulingana, maneno na kuumba.

Kila dalili iliyokuja kumthibitishia Allaah sifa ya kidhati, basi na sisi vilevile tunamthibitishia Allaah (´Azza wa Jall). Tofauti na wanavyofanya wakanushaji (Mu´attwilah) ambao wanakanusha majina na sifa za Allaah. Katika kilele chao kuna Jahmiyyah. Tofauti vilevile na wafananishaji (Mumaththilah) ambao wakapetuka katika kuthibitisha mpaka wanazithibitisha sifa za Allaah na sifa za viumbe Wake. Wamoja wamepetuka mpaka katika kutakasa mpaka wakafikia kukanusha majina na sifa za Allaah. Wengine wamepetuka mpaka katika kuthibitisha mpaka wakamshabihisha Allaah na viumbe Wake.

Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah ndio wako kati na kati baina ya makundi hayo mawili.  Wanamthibitishia Allaah zile sifa za kidhati na za kimatendo Alizojithibitishia Mwenyewe. Tofauti na wanavyofanya wakanushaji. Wanathibitisha pasi na kufananisha. Tofauti na wanavyofanya wafananishaji. Amesema (Ta´ala):

لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ ۖ وَهُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ

“Hakuna chochote kinachofanana Naye – Naye Ndiye Mwenye kusikia, Mwenye kuona.” (42:11)

Katika maneno Yake:

لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ

“Hakuna chochote kinachofanana Naye.”

Hii ni Radd kwa wafananishaji.

وَهُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ

“Naye Ndiye Mwenye kusikia, Mwenye kuona.”

Hii ni Radd kwa wakanushaji.

Haya ndio madhehebu ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah.