[4] Imewekwa Shari´ah kuswali kwa pamoja swalah za nyusiku katika kisimamo cha Ramadhaan. Bali ndilo jambo bora kuliko mtu kuswali peke yake kujengea ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) yeye mwenyewe alifanya hivo na akaonyesha fadhila zake. Abu Dharr (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Tulifunga Ramadhaan pamoja na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na wala hakuswali chochote katika mwezi mpaka kulipobaki siku saba. Ndipo akaswali na sisi mpaka kulipoenda thuluthi ya usiku. Hata hivyo [ule usiku wa] sita hakuswali na sisi isipokuwa alifanya hivo katika [ule usiku] wa tano [usiku wa 25] mpaka kukaenda nusu ya usiku. Nikasema: “Ee Mtume wa Allaah! Ungetuliswalisha tu usiku mzima.” Akasema: “Mtu akiswali pamoja na imamu mpaka atakapomaliza, basi anazingatiwa ni kama ameswali usiku [mzima].”

Ule [usiku] wa nne hakuswali, lakini ulipofika [ule usiku wa] tatu[1], akaikusanya familia yake, wake zake na watu na akatuswalisha mpaka tukachelea kupitwa na kufuzu.” Nikasema: “Kufuzu ni kitu gani?” Akasema: “Ni daku. Halafu hakutuswalisha mwezi uliobaki.”[2]

[1] Bi maana usiku wa tarehe ishirini na saba na ndio Laylat-ul-Qadr kujengea maoni yaliyo na nguvu kama tulivyotangulia kusema. Kwa ajili hiyo ndio maana Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliikusanya familia yake na wakeze katika usiku huo na hapo kuna dalili yenye kuonyesha kuwa imependekezwa kwa wanawake kuhudhuria usiku huo.

[2] Hadiyth ni Swahiyh. Wameipokea watunzi wa “as-Sunan” na wengineo. Kadhalika imetajwa katika “Swalaat-ut-Taraawiyh”, uk. 16-17, “Swahiyh Abiy Daawuud” (1245) na “al-Irwaa´” (447).

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Qiyaam Ramadhwaan, uk. 19-20
  • Imechapishwa: 07/05/2019