3. Mwenye kuhakikisha Tawhiyd basi ataingia Peponi bila ya hesabu


Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

1- Allaah (Ta´ala) amesema:

إِنَّ إِبْرَاهِيمَ كَانَ أُمَّةً قَانِتًا لِّلَّـهِ حَنِيفًا وَلَمْ يَكُ مِنَ الْمُشْرِكِينَ

”Hakika Ibraahiym alikuwa ni mfano mwema, mnyenyekevu kwa Allaah na mwenye imani safi na ya asli. Hakuwa miongoni mwa washirikina.” (16:120)

2-

وَالَّذِينَ هُم بِرَبِّهِمْ لَا يُشْرِكُونَ

“… na wale ambao Mola wao hawamshirikishi na chochote.” (23 :59)

3- Huswayn bin ´Abdir-Rahmaan amesema:

“Nilikuwa kwa Sa´iyd bin Jubayr pindi aliposema: “Ni nani kati yenu aliyeona kimondo [nyota] jana usiku?” Nikasema: “Mimi.” Halafu nikaeleza kwamba sikuwa nikiswali wakati ule kwa sababu nilikuwa nimedonolewa [na mdumu mwenye sumu]. Akasema: “Sasa ulifanya nini?” Nikasema: “Nilijitibu.” Akasema: “Kipi kilichokupelekea ufanye hivyo?” Nikasema: “Ni kutokana na Hadiyth aliyotuelezea ash-Sha´biy.” Nikasema: “Alikuelezeni nini?” Nikasema: “Ametueleza kutoka kwa Buraydah bin al-Huswayb ambaye amesema: “Ruqyah hairuhusiwi isipokuwa kwa ajili ya kijicho au homa.” Akasema: “Amefanya vyema kukomea kwenye alosikia. Lakini hata hivyo Ibn ´Abbaas ametusimulia ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema: “Ummah zote zilipitishwa mbele yangu, nikamuona Mtume akiwa na kundi dogo la watu, na Mtume akiwa na mtu mmoja au wawili, na Mtume akiwa hana mtu yeyote. Kisha nikaonyeshwa idadi kubwa ya watu niliodhania ni katika Ummah wangu, lakini nikaambiwa:  “Huyo ni Muusa na watu wake.” Kisha nikatazama nikaona kundi kubwa ambalo nikaambiwa: “Hawa ni watu wako, miongoni mwao kuna 70.000 watakaoingia Peponi bila ya kufanyiwa hesabu wala adhabu.” Kisha akainuka na kwenda nyumbani. Huku nyuma watu wakaanza kujadiliana ni nani hao watakaoweza kuwa? Baadhi yao wakasema: “Pengine ni Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam).” Wengine wakasema: “Pengine ni wale waliozaliwa katika Uislamu na hawakumshirikisha Allaah na chochote.” Wakataja mengine kadhaa. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akatoka na kuja na wakamweleza waliyokuwa wakiyajadili. Akasema:  “Ni wale wasioomba kusomewa Ruqyah, hawajichomi chuma cha moto na wala hawaamini rajua nzuri na mbaya, bali wanamtegemea Mola Wao.” ‘Ukaashah bin Mihswan (Radhiya Allaahu ‘anh) aliposikia alisimama akasema: “Muombe Allaah anijaalie kuwa mmoja wao.” Akasema: “Wewe ni katika wao.” Kisha akasimama mtu mwengine na kusema: “Muombe Allaah anijaalie kuwa mmoja wao.” Akasema: “´Ukaashah amekutangulia.”[1]

MAELEZO

Kuhakikisha Tawhiyd maana yake ni kuisafisha na shirki, Bid´ah na maasi. Mwenye kuhakikisha Tawhiyd na akasalimika na shirki, Bid´ah na maasi ataingia Peponi bila ya hesabu wala adhabu. Shirki kubwa inaitengua Tawhiyd na shirki ndogo inatengua ukamilifu wa Tawhiyd. Bid´ah na maasi yanaiathiri Tawhiyd na kupunguza thawabu zake.

1- Allaah (Ta´ala) amesema:

إِنَّ إِبْرَاهِيمَ كَانَ أُمَّةً قَانِتًا لِّلَّـهِ حَنِيفًا وَلَمْ يَكُ مِنَ الْمُشْرِكِينَ

”Hakika Ibraahiym alikuwa ni mfano mwema, mnyenyekevu kwa Allaah na mwenye imani safi na ya asli. Hakuwa miongoni mwa washirikina.” (16:120)

Allaah amemsifu kipenzi Chake Ibraahiym kwa sifa kubwa. Inafahamisha ukamilifu wa Tawhiyd na imani yake. Mosi:

إِنَّ إِبْرَاهِيمَ كَانَ أُمَّةً

”Hakika Ibraahiym alikuwa ni mfano mwema… ”

Ina maana ya kwamba alikuwa peke yake akilingania katika mema na kwamba alikuwa na subira. Hivyo ndivyo walivyofasiri wanachuoni. Alilingania katika haki na hali ya kuwa imara juu yake pindi watu walipokuwa wameharibika. Mambo haya mawili yalikuwa yamekusanyika kwa Ibraahiym. Alikuwa peke yake juu ya kufuata haki. Hakuna yeyote aliyekuwa pamoja naye. Pamoja na hivyo alilingania katika haki peke yake.

2-

أُمَّةً قَانِتًا لِّلَّـهِ

“Mnyenyekevu kwa Allaah… “

Bi maana alikuwa siku zote ni mwenye kumtii Allaah na mwenye kuendelea kufanya matendo mema. Alikuwa ni mwenye kutii siku zote na akimuabudu Allaah peke yake. Hakuwa akimuabudu mwengine yeyote zaidi Yake.

3-

حَنِيفًا

“… mwenye imani safi na ya asli.“

Bi maana mwenye kuemelea kwa Allaah. Aliwapa mgongo waungu wote kwa ajili ya kumuabudu Allaah (´Azza wa Jall) peke yake. Kisha Akakazia hilo kwa kusema:

وَلَمْ يَكُ مِنَ الْمُشْرِكِينَ

”Hakuwa miongoni mwa washirikina.”

Alitofautiana nao katika ´Aqiydah yake, matendo, maneno na nyumba yake. Muislamu anatakiwa kuwa katika njia iliyonyooka na kuihakikisha Tawhiyd yake. Kwa sifa hizi ndio Ibraahiym (´alayhis-Swalaatu was-Salaam) alihakikisha ukamilifu wa Tawhiyd yake.

2-

وَالَّذِينَ هُم بِرَبِّهِمْ لَا يُشْرِكُونَ

“… na wale ambao Mola wao hawamshirikishi na chochote.” (23 :59)

Hii ni moja katika sifa za wapwekeshaji na watu wa imani. Wanampwekesha Allaah na kumtakasia Yeye dini. Hawachanganyi ´ibaadah zao na shirki. Wanamuabudu Allaah na kumwogopa. Huu ndio ukamilifu wa Tawhiyd. Ikiwa Ibraahiym (´alayhis-Swalaatu was-Salaam) alihakikisha Tawhiyd basi Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alifanya zaidi ya hivo. Kwa sababu yeye ndiye mchaji Allaah na mwenye kumtakasia ´ibaadah Allaah zaidi katika watu.

3- Huswayn bin ´Abdir-Rahmaan amesema:

“Nilikuwa kwa Sa´iyd bin Jubayr pindi aliposema: “Ni nani kati yenu aliyeona kimondo [nyota] jana usiku?” Nikasema: “Mimi.” Halafu nikaeleza kwamba sikuwa nikiswali wakati ule kwa sababu nilikuwa nimedonolewa [na mdumu mwenye sumu]. Akasema: “Sasa ulifanya nini?” Nikasema: “Nilijitibu.” Akasema: “Kipi kilichokupelekea ufanye hivyo?” Nikasema: “Ni kutokana na Hadiyth aliyotuelezea ash-Sha´biy.” Nikasema: “Alikuelezeni nini?” Nikasema: “Ametueleza kutoka kwa Buraydah bin al-Huswayb ambaye amesema: “Ruqyah hairuhusiwi isipokuwa kwa ajili ya kijicho au homa.” Akasema: “Amefanya vyema kukomea kwenye alosikia. Lakini hata hivyo Ibn ´Abbaas ametusimulia ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema: “Ummah zote zilipitishwa mbele yangu, nikamuona Mtume akiwa na kundi dogo la watu, na Mtume akiwa na mtu mmoja au wawili, na Mtume akiwa hana mtu yeyote. Kisha nikaonyeshwa idadi kubwa ya watu niliodhania ni katika Ummah wangu, lakini nikaambiwa:  “Huyo ni Muusa na watu wake.” Kisha nikatazama nikaona kundi kubwa ambalo nikaambiwa: “Hawa ni watu wako, miongoni mwao kuna 70.000 watakaoingia Peponi bila ya kufanyiwa hesabu wala adhabu.” Kisha akainuka na kwenda nyumbani. Huku nyuma watu wakaanza kujadiliana ni nani hao watakaoweza kuwa? Baadhi yao wakasema: “Pengine ni Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam).” Wengine wakasema: “Pengine ni wale waliozaliwa katika Uislamu na hawakumshirikisha Allaah na chochote.” Wakataja mengine kadhaa. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akatoka na kuja na wakamweleza waliyokuwa wakiyajadili. Akasema:  “Ni wale wasioomba kusomewa Ruqyah, hawajichomi chuma cha moto na wala hawaamini rajua nzuri na mbaya, bali wanamtegemea Mola Wao.” ‘Ukaashah bin Mihswan (Radhiya Allaahu ‘anh) aliposikia alisimama akasema: “Muombe Allaah anijaalie kuwa mmoja wao.” Akasema: “Wewe ni katika wao.” Kisha akasimama mtu mwengine na kusema: “Muombe Allaah anijaalie kuwa mmoja wao.” Akasema: “´Ukaashah amekutangulia.”[2]

Kauli yake “Halafu nikaeleza kwamba sikuwa nikiswali wakati ule” ni sifa miongoni mwa sifa za Salaf. Walikuwa wakiogopa kudhihirisha matendo yao ili wasije kutumbukia katika kujionyesha na mtu kuisifu nafsi yake.

Kauli yake ”Nilikuwa nimedonolewa” inaonesha ilikuwa ni nge, nyoka na mfano wake.

Kauli yake “Nilijitibu” inaonesha kuwa alimuomba mtu mwingine amtibu kwa Ruqyah. Allaah hunufaisha kwa Ruqyah.

Kauli yake “Kipi kilichokupelekea ufanye hivyo?” ni swali juu ya dalili kwa alichokifanya. Salaf walikuwa hivyo na masomo yao na pupa yao juu ya dalili.

Kauli yake ”… kutoka kwa Buraydah bin al-Huswayb” ina maana ya kwamba Hadiyth hii imepokelewa na Buraydah na kwamba imepokelewa kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Kauli yake “Amefanya vyema kukomea kwenye alosikia” ni dalili ya kwamba alifanya kwa ujuzi na hakufanya kwa ujinga au kinyume na alivyojifunza.

Kauli yake “Ruqyah hairuhusiwi isipokuwa kwa ajili ya kijicho au homa” ni dalili yenye kuonesha kuwa mwenye kusibiwa na nge, nyoka au maradhi mengine ni sawa akajifanyia mwenyewe matabano na akawaomba wengine wamfanyie matabano. Hadiyth haikukoma kwa hayo yaliyotajwa peke yake. Wanachuoni wanaifasiri kama kipaumbele na kwamba hakuna kinachotibu kijicho na homa kama Ruqyah. Kwa sababu kuna Hadiyth zingine zinazoruhusu matabano katika mnasaba wa mambo mengine mbali na kijicho na homa peke yake. Kwa mfano Hadiyth:

“Kujitibu [kwa Ruqyah] kunaruhusu midhali sio shirki.”[3]

Imethibiti pia ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alifanya matabano na akafanyiwa matabano. Ni dalili inayofahamisha kuwa ni sawa kumnufaisha mgonjwa na kumsomea Aayah za Qur-aan.

Kauli yake ”… kijicho au homa” yaani kijicho cha mwenye kufanya kijicho, mtazamo wake na yeye mwenyewe na homa imefungamana na kudona kwa nyoka au nge.

Tiba hii ni yenye kunufaisha kwa maandiko na uzowefu. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Anayeweza kumnufaisha ndugu yake kwa kitu basi na amnufaishe.”[4]

Lililo bora ni mtu kutoomba kufanyiwa Ruqyah. Lakini hata hivyo inafaa wakati wa haja. Ndio maana Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliomba Ruqyah kwa mtoto wa Ja´far na kumwambia mama yao Asmaa´ wakati waliposibiwa na kijicho:

“Wasomee Ruqyah.”[5]

 Kisha Sa´iyd akataja kilicho bora kuliko kuomba Ruqyah na akasimulia Hadiyth ya Ibn ´Abbaas.

Maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) “Ummah zote zilipitishwa mbele yangu” imesemekana kwa mujibu wa maoni sahihi ya kwamba ni katika usiku wa Israa´.

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema “Mtume akiwa hana mtu yeyote”. Kuna baadhi ya Mitume waliouawa na watu wao. Ni dalili yenye kuonesha kuwa ni wachache ndio wenye kufuata haki. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَمَا أَكْثَرُ النَّاسِ وَلَوْ حَرَصْتَ بِمُؤْمِنِينَ

“Na wengi wa watu hawatoamini japokuwa utafanya hima.”[6]

Maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) “Huyo ni Muusa na watu wake” ni dalili yenye kuonesha fadhila za Muusa na kwamba wana wa Israaiyl wengi walimuitikia.

Maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) “Nikaona kundi kubwa” na katika upokezi mwingine imekuja “Nikaona kundi kubwa la watu lililofunika upeo” na katika upokezi mwingine imekuja “Nikaona kundi kubwa la watu lililofunika upeo mwingine” ni dalili yenye kuonesha ukubwa wa Ummah huu na kwamba una wafuasi wengi. Kwa sababu ndio Ummah wa mwisho na Mtume wao ndio Mtume wa mwisho. Wao ndio watakuwa nusu ya wafuasi wa Peponi au theluthi, kama ilivyokuja katika Hadiyth.

Maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) “… miongoni mwao kuna 70.000… “. Imekuja katika Hadiyth nyingine kuwa kila mmoja katika hawa 70.000 wataingia 70.000 Peponi bila ya hesabu[7] kutokana na ukamilifu wa uchaji Allaah wao, imani na msimamo wao. Kadri jinsi mtu atavyokuwa na msimamo ndivyo itavyozidi kuwa sahali kuingia Peponi.

Maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) “Huku nyuma watu wakaanza kujadiliana… ” bi maana juu ya sifa zao na ni kina nani. Hapa kuna dalili juu ya kufanya utafiti, kusoma na kupeleleza maandiko kwa ajili ya elimu.

Maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ”Ni wale wasioomba kusomewa Ruqyah” bi maana ya kwamba hawamuombi mtu awasomee. Ni dalili yenye kuonesha kuwa lililo bora ni kutowaomba watu kitu ikiwa ni pamona na Ruqyah. Pamoja na hivyo hakukataza hilo. Lililo bora tu ni kutowaomba hilo. Wakati wa haja ni sawa kuomba tiba na ni bora kutofanya hivo ikiwa hakuna haja hiyo.

Maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) “… hawajichomi chuma cha moto… “. Bora ni kuacha kufanya hivo ikiwa ni pasi na haja kwa sababu ni aina fulani ya kujiadhibu. Ikiwa mtu anaweza kujitibu kwa kutumia dawa nyingine bora ni kufanya hivo. Ikiwa kuna haja ya kufanya hivo hakuna machukizo kuitumia kutokana na Hadiyth:

“Dawa iko katika mambo matatu; kujichoma kwa chuma cha moto, asali na kuumikwa.”

Katika matamshi mengine Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Ninaukataza Ummah wangu na kujichoma kwa chuma cha moto.”[8]

Hata hivyo makatazo haya ni kwa ya machukizo na si kwamba ni haramu. Kwa ajili hiyo kuna baadhi ya Maswahabah waliojitibu kwa kujichoma pindi walipokuwa wagonjwa. Ni jambo lenye kujuzu wakati wa haja lakini ni bora zaidi kwa dawa nyingine. Hii ni moja katika sifa za wale watu 70.000. Lakini hata hivyo kama jinsi tulivyosema inajuzu wakati wa haja.

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema “… na wala hawaamini rajua nzuri na mbaya… “. Ni shirki. Kuamini rajua nzuri na mbaya maana yake ni mtu kuamini mkosi pale anapoona au kusikia kitu na hiyo inakuwa ni sababu ya kumzuia kufanya kitu alichokuwa amepanga. Huu ni uovu uliyokatazwa. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Kuamini rajua nzuri au mbaya ni shirki.”[9]

Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa salam) tena:

“Haifai ikamzuia muislamu.”[10]

Kadhalika amesema:

“Mmoja wenu akiona kitu chenye kumchukiza aseme: “Ee Allaah! Hakuna mwengine mwenye kuleta mema isipokuwa Wewe. Hakuna mwengine mwenye kuzuia mabaya isipokuwa Wewe. Hakuna nguvu za kufanya utiifu wala kuacha maasi isipokuwa kwa msaada Wako.”[11]

Mema ni neema na mabaya ni majanga na shida. Vilevile amesema kuwa kafara ya kuamini rajua nzuri au mbaya ni mtu kusema:

“Ee Allaah! Hakuna kheri isipokuwa kheri Yako. Hakuna makadirio isipokuwa ya Kwako. Hakuna mungu wa haki isipokuwa Wewe.”[12]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“… bali wanamtegemea Mola Wao… ” bi maana ni wenye kumtegemea Allaah. Wanamwachia mambo yao Allaah. Hizi ndio hali zao. Wanamtegemea Allaah na kumwamini. Wanatambua kuwa hakuna kitakachowafika isipokuwa kile alichowaandikia. Aidha wanajiepusha na aina zote za shirki na mambo ya kuchukiza kama kujichoma na kuomba kusomewa Ruqyah kwa sababu wanamtegemea Yeye, wanamtegemea na ni wenye kupigania kuwa na dini kamilifu na salama.

Hizi ndio sifa walonazo wale watu 70.000. Ni wale waliotekeleza mambo ya wajibu, wakaachana na mambo ya haramu na ya shirki, wanamtegemea Allaah na kumwachia mambo yote Allaah na pamoja na kuwa wakati huo huo wanafanya sababu zilizoruhusiwa katika kutafuta riziki, kufanya biashara na dawa. Wanaacha yale mambo yenye kuwafanya kuwa na haja na watu wengine kama kuwaomba wawasomee Ruqyah na aina za kujiadhibu maadamu si wenye dharurah ya kufanya hivo. Wanaacha mambo fulani yaliyoruhusiwa kwa sababu tu yana mapungufu. Malipo yao Allaah awaingize Peponi pasi na hesabu wala adhabu.

FAIDA

Ruqyah pasi na kuomba inafaa. Ikiwa Ruqyah imefungamana na mtu kuomba lililo bora zaidi ni mtu kuacha kufanya hivo midhali hakuna haja. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Kujitibu [kwa Ruqyah] kunaruhusu midhali sio shirki.”

Ruqyah inajuzu kwa sharti tatu:

1- Iwe kwa lugha yenye kufahamika.

2- Isiwe na mambo yasiyojuzu katika Shari´ah.

3- Ifanywe kwa kutarajia ya kwamba Allaah ndiye mponyaji. Mtu asitegemee Ruqyah yenyewe.

Katika hali hii Ruqyah inajuzu.

Kadhalika kujichoma kunajuzu wakati wa haja. Lakini hata hivyo kuacha hilo ni bora zaidi kwa sababu ni aina ya kujiadhibu.

Sababu zingine zote ni lazima zifanywe. Ni lazima kula na kunywa. Riziki ni lazima itafutwe. Mambo ya wajibu ni lazima yafanywe na madhambi ni lazima yaepukwe ili mtu aweze kuingia Peponi. Sababu zilizo na mapungufu, kama mfano wa kujichoma na kuomba kusomewa Ruqyah, bora zaidi ni kuziepuka.

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema “´Ukaashah amekutangulia” ili kufunga mlango wasije kuwaomba wale wasiostahiki. Wanachuoni wanatumia Hadiyth hii ili kutolea dalili kuonesha kuwa inajuzu kutaka udhuru kwa ajili ya kuzuia kitu kibaya pasi na kumuumbua wala kumfedhehesha mtu.

Ni jambo lisilokuwa na ubaya kwa mtu kujifanyia Ruqyah mwenyewe na ni bora kutumuomba yeyote akusomee. Ni sawa kwa mtu akamuomba ndugu yake amuombee du´aa. Imetajwa katika Hadiyth:

“Usitusahau katika du´aa yako.”[13]

Ni jambo limewekwa katika Shari´ah kujitenga mbali na mambo yote yenye kudhuru ikiwa ni pamoja na mtu mgonjwa ambaye ana maradhi ya kuambukiza. Ajitenga naye. Imetajwa katika Hadiyth:

“Mgonjwa asiyende kwa ambaye ana afya njema.”[14]

Hata hivyo inafaa kwa mtu kufanya hivo ikiwa mtu huyo anamwamini Allaah na kumtegemea Yeye kutokana na imani yake ya wazi. Imethibiti ya kwamba (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliika na kula pamoja na mtu mwenye ukoma na kusema:

“Kula kwa jina la Allaah kwa kumtegemea Allaah.”[15]

Inafaa vilevile kuyasomea maji na kuyatemea cheche za mate. Imethibiti kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alitemea cheche za mate kwenye maji ya Thaabit bin Qays[16]. Kisomo kinatakiwa kiwe kile ambacho ni chepesi kwa mtu kusoma kutoka katika Qur-aan.

[1] al-Bukhaariy (5705) na Muslim (220).

[2] al-Bukhaariy (5705) na Muslim (220).

[3] Muslim (2200) na Abu Daawuud (3886).

[4] Muslim (2199) na Ahmad (13819).

[5] Muslim (2198) na Ahmad (14163).

[6] 12:103

[7] Ahmad (22). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh-ul-Jaami´” (1057).

[8] al-Bukhaariy (5681) na Muslim (2205).

[9] Abu Daawuud (3910), Ibn Maajah (3538) na Ahmad (3687). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh-ul-Jaami´” (3960).

[10] Abu Daawuud (3919). Dhaifu kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Silsilat-ul-Ahaadiyth adh-Dhwa´iyfah (1619).

[11] Abu Daawuud (3919). Dhaifu kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Silsilat-ul-Ahaadiyth adh-Dhwa´iyfah (1619).

[12] Ahmad (7045). Nzuri kwa mujibu wa Shu´ayb al-Arnaa´uut katika ”Musnad Ahmad”.

[13] Ahmad (195), Abu Daawuud (1498) na Ibn Maajah (2894). Dhaifu kwa mujibu wa al-Albânî i ”Dhwa´iyf-ul-Jaami´ (14425).

[14] al-Bukhaariy (5771) na Muslim (2221).

[15] Abu Daawuud (3925), at-Tirmidhiy (1817) na al-Haakim (7196). Dhaifu kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Dhwa´iyf Sunan at-Tirmidhiy” (307).

[16] Abu Daawuud (3885). Dhaifu kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Dhwa´iyf Sunan Abiy Daawuud” (836).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kitaab-it-Tawhiyd, uk. 20-26
  • Imechapishwa: 18/03/2018