Allaah (Ta´ala) amesema:

فَإِنْ حَاجُّوكَ فَقُلْ أَسْلَمْتُ وَجْهِيَ لِلَّـهِ وَمَنِ اتَّبَعَنِ

“Na wakikuhoji, basi sema: “Nimejisalimisha kwa Allaah kikamilifu na wale walionifuata.” (03:20)

al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kupitia kwa Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Uislamu ni kushuhudia ya kwamba hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah, kusimamisha swalah, kutoa zakaah, kufunga Ramadhaan na kuhiji kwenye Nyumba ukiweza kuiendea.”[1]

al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Muislamu ni yule mwenye kuwasalimisha waislamu kwa ulimi na mkono wake na muhajiri ni yule mwenye kuyahama yale Allaah aliyokataza.”[2]

Bahz bin Hakiym amepokea kutoka kwa baba yake, kutoka kwa babu yake ambaye ameeleza kuwa alimuuliza Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) juu ya Uislamu ambapo akajibu:

“Ni kuusalimisha moyo wako kwa Allaah (Ta´ala), kuuelekeza uso wako kwa Allaah (Ta´ala), kuswali swalah za faradhi na kutoa zakaah iliyofaradhishwa.”[3]

Ameipokea Ahmad.

Abu Qilaabah amepokea kutoka kwa mtu miongoni mwa watu wa Shaam ambaye amepokea kutoka kwa baba yake ambaye alimuuliza Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuhusu Uislamu ambapo akajibu:

“Ni kuusalimisha moyo wako kwa Allaah (Ta´ala) na waislamu wasalimike na ulimi na mkono wako.” Akasema: “Ni Uislamu upi bora?” Akajibu: “Imani.” Akauliza: “Ni nini imani?” Akajibu: “Ni kumwamini Allaah, Malaika Wake, Vitabu Vyake, Mitume Wake na kufufuliwa baada ya kufa.” [4]

[1] al-Bukhaariy (4777) na Muslim (102).

[2] al-Bukhaariy (6484) na Muslim (41).

[3] Ahmad (3/5), Ibn Hibbaan (1/376) na al-Haakim (4/643).

[4] Ahmad (4/114)

  • Mhusika: Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fadhwl-ul-Islaam, uk. 13-15
  • Imechapishwa: 23/10/2016