29. Sura ya tatu: Uwekaji Shari´ah na kwamba kuhalalisha na kuharamisha ni haki ya Allaah

Makusudio ya uwekaji Shari´ah ni yale ambayo Allaah amewateremshia waja Wake katika mfumo ambao wanapita juu yake katika ´Aqiydah, mu´amala na mengineyo. Miongoni mwa hayo kunaingia vilevile kuhalalisha na kuharamisha. Hakuna yeyote ana haki ya kuhalalisha isipokuwa yale yaliyohalalishwa na Allaah na kuharamisha isipokuwa yale yaliyoharamishwa na Allaah. Amesema (Ta´ala):

وَلَا تَقُولُوا لِمَا تَصِفُ أَلْسِنَتُكُمُ الْكَذِبَ هَـٰذَا حَلَالٌ وَهَـٰذَا حَرَامٌ لِّتَفْتَرُوا عَلَى اللَّـهِ الْكَذِبَ

“Na wala msiseme yanayosifu ndimi zenu uongo “hii halali na hii haramu” ili mumzulie Allaah uongo.”[1]

قُلْ أَرَأَيْتُم مَّا أَنزَلَ اللَّـهُ لَكُم مِّن رِّزْقٍ فَجَعَلْتُم مِّنْهُ حَرَامًا وَحَلَالًا قُلْ آللَّـهُ أَذِنَ لَكُمْ ۖ أَمْ عَلَى اللَّـهِ تَفْتَرُونَ

“Sema: “Mnaonaje zile riziki alizokuteremshieni Allaah ambapo mkazifanya katika hizo ni haramu na halali. Sema: “Je, Allaah amekuidhinisheni au mnamzulia Allaah?”[2]

Allaah amekataza kuhalalisha na kuharamisha pasi na dalili kutoka katika Qur-aan na Sunnah na akakhabarisha kwamba jambo hilo ni katika kumsemea Allaah uongo. Ni kama alivyokhabarisha (Subhaanah) kwamba mwenye kuwajibisha kitu au akaharamisha kitu bila dalili, basi ameifanya nafsi yake kuwa ni mshirika wa Allaah katika mambo ambayo ni maalum Kwake. Mambo yenyewe ni hayo ya kuweka Shari´ah. Amesema (Ta´ala):

أَمْ لَهُمْ شُرَكَاءُ شَرَعُوا لَهُم مِّنَ الدِّينِ مَا لَمْ يَأْذَن بِهِ اللَّـهُ

“Je, wanao washirika waliowawekea Shari´ah katika dini yale ambayo Allaah hakuyatolea idhini?”[3]

Yule mwenye kumtii mwekaji Shari´ah huyu badala ya Allaah ilihali anajua jambo hilo na akakubaliana naye katika kitendo chake, basi ameshirikisha pamoja na Allaah. Amesema (Ta´ala):

وَإِنْ أَطَعْتُمُوهُمْ إِنَّكُمْ لَمُشْرِكُونَ

“Mtakapowatii hakika mtakuwa washirikina.”[4]

Bi maana wale wanaohalalisha nyamafu zilizoharamishwa na Allaah. Mwenye kuwatii katika hayo basi huyo ni mshirikina. Ni kama alivyoeleza (Subhaanah) kwamba mwenye kuwatii wanazuoni wa kiyahudi na wanazuoni wa kinaswara katika kuhalalisha yale yaliyoharamishwa na Allaah na kuharamisha yale yaliyohalalishwa na Allaah, basi mtu huyo amewafanya kuwa waungu badala ya Allaah. Amesema (Ta´ala):

اتَّخَذُوا أَحْبَارَهُمْ وَرُهْبَانَهُمْ أَرْبَابًا مِّن دُونِ اللَّـهِ وَالْمَسِيحَ ابْنَ مَرْيَمَ وَمَا أُمِرُوا إِلَّا لِيَعْبُدُوا إِلَـٰهًا وَاحِدًا ۖ لَّا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ ۚ سُبْحَانَهُ عَمَّا يُشْرِكُونَ

“Wamewafanya marabi wao na watawa wao kuwa ni waungu badala ya Allaah na al-Masiyh mwana wa Maryam na hali hawakuamrishwa isipokuwa kumwabudu Mungu mmoja. Hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Yeye – utakasifu ni Wake kutokamana na yale yote wanayomshirkisha.”[5]

Wakati ´Adiyy bin Haatim (Radhiya Allaahu ´anh) wakati aliposikia Aayah hii akasema: “Ee Mtume wa Allaah! Tulikuwa hatuwaabudu.” Ndipo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamwambia:

“Je, si walikuwa wakihalalisha yale yaliyoharamishwa na Allaah nanyi mnayahalalisha na wakiharamisha yale yaliyoharamishwa na Allaah nanyi mnayaharamisha?” Akajibu: “Ndio.” Akasema: “Huku ndio kuwaabudu.”[6]

Shaykh ´Abdur-Rahmaan bin Hasan (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Katika Hadiyth kuna dalili inayothibitisha kwamba kuwatii wanazuoni wa kiyahudi na wanazuoni wa kinaswara katika kumuasi Allaah ni kuwaabudu wao badala ya Allaah na ni katika shirki kubwa isiyosamehewa na Allaah. Hayo ni kutokana na maneno Yake (Ta´ala) mwishoni mwa Aayah:

وَمَا أُمِرُوا إِلَّا لِيَعْبُدُوا إِلَـٰهًا وَاحِدًا ۖ لَّا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ ۚ سُبْحَانَهُ عَمَّا يُشْرِكُونَ

“… na hali hawakuamrishwa isipokuwa kumwabudu Mungu mmoja. Hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Yeye – utakasifu ni Wake kutokamana na yale yote wanayomshirkisha.”

Mfano wa hayo ni maneno Yake (Ta´ala):

وَلَا تَأْكُلُوا مِمَّا لَمْ يُذْكَرِ اسْمُ اللَّـهِ عَلَيْهِ وَإِنَّهُ لَفِسْقٌ ۗ وَإِنَّ الشَّيَاطِينَ لَيُوحُونَ إِلَىٰ أَوْلِيَائِهِمْ لِيُجَادِلُوكُمْ ۖ وَإِنْ أَطَعْتُمُوهُمْ إِنَّكُمْ لَمُشْرِكُونَ

“Na wala msile katika ambavyo havikutajiwa Jina la Allaah, kwani hakika huo ni ufasiki, na hakika mashaytwaan wanawanong´oneza wapenzi wao wandani wabishane nanyi – na mtakapowatii hakika mtakuwa washirikina.”[7]

Watu wengi wametumbukia katika jambo hili kwa wale wanaowafuata kibubusa kwa sababu ya kutozingatia kwao dalili ikienda kinyume na yule wanayemfuata kibubusa. Ni katika aina ya shirki hii.”[8]

Kwa hivyo kulazimiana na Shari´ah ya Allaah na kuachana na Shari´ah za wengineo ni katika muqtadha ya “Laa ilaaha illa Allaah”.

[1] 16:116

[2] 10:59

[3] 42:21

[4] 06:121

[5] 09:31

[6] at-Tirmidhiy amepokea mfano wake (3104).

[7] 06:121

[8] Fath-ul-Majiyd, uk. 390.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ´Aqiydat-ut-Tawhiyd, uk. 53-55
  • Imechapishwa: 25/02/2020