29. Sema kama alivyosema Mtume (´alayhis-Salaam)


Imaam Ibn Abiy Daawuud (Rahimahu Allaah) amesema:

08- Jahmiy anaweza kuyapinga haya

    sisi kwa ukweli wa tuliyoyasema tuna Hadiyth zilizoweka wazi

 

09- Jariyr amepokea kutoka katika maneno ya Muhammad

       juu ya hayo utafaulu

MAELEZO

Jahmiy anaweza kupinga Kuonekana kwa Allaah (´Azza wa Jall) Aakhirah. Hawana mashiko yoyote kwa hayo. Kuhusu sisi katika kuthibitisha Kuonekana tuna Hadiyth nyingi zilizopokelewa kwa njia nyingi kutoka kwa kundi la Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum). Ibn-ul-Qayyim (Rahimahu Allaah) amezipokea katika “Haadi al-Arwaah ilaa Bilaad-il-Afraah”. Ni kitabu kinachozungumzia Pepo, kimeisifu na kuelezea yaliyomo ndani yake. Ndani yake ametaja Kuonekana kwa Allaah na amesimulia vilevile Hadiyth zilizothibiti kwa mapokezi mengi kwa mtiririko wake, mlolongo wa wapokezi wake na mapokezi yake.

Jariyr… – Anaitwa Jariyr bin ´Abdillaah al-Bajaliy (Radhiya Allaahu ´anh). Ni mmoja miongoni mwa wapokezi katika Maswahabah. Vinginevyo kuna Maswahabah wengine waliopokea. Amechotaka mwandishi (Rahimahu Allaah) ni kupigia mfano peke yake.

kutoka katika maneno ya Muhammad – Bi maana Jariyr alipokea kutoka katika maneno ya Mtume wa Allaah Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

sema kama alivyosema… – Bi maana sema kama alivyosema Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) utafaulu. Usiende kinyume na maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ukaja kula khasara. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hatamki kwa matamanio yake:

وَمَا يَنطِقُ عَنِ الْهَوَىٰ إِنْ هُوَ إِلَّا وَحْيٌ يُوحَىٰ

“Wala hatamki kwa matamanio. Hayo ayasemayo si chochote isipokuwa ni Wahy unaofunuliwa kwake.” (53:03-04)

Maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni haki na hayaingiliwi na shaka yoyote.