Wakati Sufyaan ath-Thawriy alipofika Baswrah akataka kutazama hali ya Rabiy´ bin Swabiyh na nafasi yake mbele ya watu ambapo akauliza juu ya madhehebu yake. Akaambiwa kuwa hana madhehebu mengine zaidi ya kufuata Sunnah. Watu wakasema kuwa hawajui madhehebu yake mengine mbali na kufuata Sunnah. Akauliza: “Kina nani marafiki zake?” Wakasema: “Qadariyyah.” Akasema: “Basi na yeye ni Qadariy.”

Ibn Battwah (Rahimahu Allaah) amesema katika “al-Ibaadah” akiwa ni mwenye kuwekea taaliki maneno haya ya Sufyaan:

“Allaah amrehemu Sufyaan ath-Thawriy. Amezungumza kwa hekima na amesema kweli. Amesema kwa elimu ambapo akaafikiana na Qur-aan na Sunnah na yale yanayopelekea hekima, jambo ambalo linajulikana na watambuzi na wasomi. Allaah (Ta´ala) amesema:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَتَّخِذُوا بِطَانَةً مِّن دُونِكُمْ لَا يَأْلُونَكُمْ خَبَالًا وَدُّوا مَا عَنِتُّمْ

“Enyi walioamini! Msifanye rafiki mwandani wasiokuwa nyinyi, kwani hawatoacha kukuharibieni. Wanatamani kama mngetaabika.”[1]

Fudhwayl bin ´Iyaadhw (Rahimahu Allaah) amesema:

“Roho ni wanajeshi walioshikana. Wale ambao wataafikiana wataungana na wale ambao hawatoafikiana watatengana. Mtu wa Sunnah hawezi kumnusuru mzushi isipokuwa kwa unafiki.”

Ibn Battwah (Rahimahu Allaah) amesema akiwa ni mwenye kuyawekea taaliki hayo:

“Fudhwayl amesema kweli. Kwani hakika sisi tunayaona hayo waziwazi.”[2]

Hali ilifika Salaf (Rahimahumu Allaah) kutahadharisha wazushi mpaka Ahmad bin Sinaan akafikia kusema:

“Napendelea zaidi kuwa na ujirani na mtu wa ngoma kuliko kuwa na ujirani na mzushi. Kwa sababu mtu wa ngoma nitamkataza na nitavunja ngoma yake. Mzushi anawaharibu watu, majirani na wachipukizi.”[3]

Ibn Battwah (Rahimahu Allaah) amesema akiwa ni mwenye kuwekea taaliki maudhui haya akasema:

“Ala ala enyi waislamu! Kuwa na dhana njema kwa mmoja wenu na uzoefu wa usahihi wa madhehebu yake kusimpelekee kuitia khatarini dini yake ambapo akakaa na baadhi ya watu wenye matamanio haya kwa hoja eti anatangamana nao kwa ajili ya kuwahoji na kumwondosha katika madhehebu yake. Kwani wazushi wana fitina kubwa zaidi kuliko ad-Dajaal, maneno yao yanaambukiza zaidi kuliko upele na ni yenye kuzichoma nyoyo zaidi kuliko moto. Tumeona kikosi cha watu ambao walikuwa wakiwalaani na wakiwatukana. Baadaye wakaketi nao kwa lengo la kuwakaripia na kuwaraddi. Wazushi wakawarembearembea na kuwafanyia vitimbi na kufuru ya chini kwa chini mpaka mwishowe wakajiunga nao.”[4]

Tumewaona watu wa sampuli hiyo katika zama zetu hizi ambao wanasema kuwa wanaketi na wazushi hawa kwa sababu ya kuwanasihi na kwa ajili ya kuona mifumo yao ya kisiri wanayoificha ili huko baadaye tupate kuitahadharisha. Baada ya hapo wakaanguka kwenye kamba zao na wakawa ni wasaidizi wao dhidi ya Ahl-us-Sunnah. Allaah atulinde sisi na nyinyi kutokamana na hayo. Haya ndio yaliyothibitishwa na Salaf.

[1] 03:118 ”al-Ibaanah” (02/456).

[2] ”al-Ibaanah” (02/459).

[3] ”al-Ibaanah” (02/469).

[4] ”al-Ibaanah” (02/470).

  • Mhusika: Shaykh ´Abdus-Salaam bin Barjas
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Usuwl-ud-Da´wah as-Salafiyyah, uk. 70-73
  • Imechapishwa: 12/11/2020