29. Matahadharisho ya Salaf juu ya falsafa

Falsafa ni ile iliozushwa na wanafalsafa katika mambo ya I´tiqaad kama kuthibitisha ´Aqiydah kwa njia yao wenyewe waliyozusha na kupuuza yale yaliyokuja katika Qur-aan na Sunnah. Salaf wametahadharisha falsafa na watu wake kwa njia mbalimbali kutokana na vile inapelekea katika shubuha na mashaka. Imaam Ahmad amefikia mpaka kusema:

“Mwanafalsafa hafanikiwa kamwe.”

ash-Shaafi´iy amesema:

“Ninaonelea kuwa mwanafalsafa anatakiwa kuchapwa kwa bakora na viatu. Azungushwe kati ya watu na kusemwe: “Haya ndio malipo kwa yule mwenye kuacha Qur-aan na Sunnah na akaenda katika falsafa.”

Kwa njia moja wapo wanastahiki yale yaliyosemwa na Imaam ash-Shaafi´iy ili watubu kwa Allaah na liwashtue wengine kufuata madhehebu yao. Lakini mtu akiwaangalia kwa njia nyingine na namna ambavyo wamechanganyikiwa na namna ambavyo shaytwaan amewatawala, basi tunawaonea huruma na kuwasikitikia. Tunamhimidi Allaah ambaye ametuokoa sisi juu ya yale aliyowapa mtihani kwayo.Tunawatazama kwa njia mbili:

1- Mtazamo wa njia ya Kishari´ah. Tunawatia adabu na kuwakemea kueneza madhehebu yao.

2- Mtazamo wa njia ya Qadar. Tunawahurumia na tunawaombea kwa Allaah hali ya salama na tunamhimidi Allaah ambaye ametuokoa kutokamana na hali yao.

Wengi wanaokhofiwa juu yao upotevu katika watu hawa ni wale ambao wameingia katika falsafa pasi na kufikia katika lengo lake. Yule ambaye hajaingia katika falsafa amesalimika. Na ambaye amefikia kina chake basi amekwishabainikiwa uharibifu madhehebu haya. Natija yake akarejea katika Qur-aan na Sunnah, kama ilivyopitika kwa baadhi ya vigogo wao. Khatari inabaki kwa yule ambaye ameacha Njia iliyonyooka na bado hajabainikiwa na uhakika wa mambo yalivyo.

Katika kitabu hichi Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) ametaja maneno ya wanafalsafa wengi juu ya suala hili. Amesema:

“Hata kama Qur-aan, Sunnah na mapokezi ya Salaf yanatosheleza, kuna watu wengi ambao wanajinasibisha na mapote ya wanafalsafa. Wanawadhania vyema na kufikiria kwamba wamelikagua suala hili zaidi ya wengine wote. Lau mtu atawapa Aayah zote, basi hawatozifuata mpaka yatajwe maoni yao.”

Kisha akasema:

“Hatukubaliani na yale yote ambayo yamesemwa na wanafalsafa na wengineo katika maudhui haya na maudhui mengine. Lakini hata hivyo haki inakubaliwa kutoka kwa kila mwenye kuitamka.”

Hapa amebainisha (Rahimahu Allaah) kwamba malengo ya nukuu hizi ni kupokea haki kutoka katika kila pande na kuwasimamishia hoja watu hawa kutoka katika maneno ya maimamu wao wenyewe.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fath Rabb-il-Bariyyah, uk. 75-76
  • Imechapishwa: 11/05/2020