Abu Ja´far at-Twahaawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

25- Kwa sababu Yeye juu ya kila jambo ni muweza. Kila kitu ni chenye kumuhitajia Yeye. Kila jambo Kwake ni jepesi:

لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ ۖوَهُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ

“Hakuna chochote kinachofanana Naye – Naye ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona.”[1]

MAELEZO

Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

إِنَّمَا أَمْرُهُ إِذَا أَرَادَ شَيْئًا أَن يَقُولَ لَهُ كُن فَيَكُونُ

”Hakika amri Yake anapotaka jambo lolote huliambia: “Kuwa!” nalo huwa.”[2]

Yeye ndiye Mwenye kuhuisha na kufisha, Mwenye kuumba na kuruzuku, Mwenye kutoa na kuzuia. Yeye ndiye mwenye kuwahuisha watu baada ya kwamba walikuwa wameshateketea. Hilo ni jepesi Kwake (Subhaanahu wa Ta´ala). Hilo halimkalifu chochote na wala si zito Kwake. Hilo ni tofauti na viumbe ambao wanalazimika kujikalifisha katika kuyafanya mambo. Wakati mwingine hutokea kwamba yamewashinda. Kuhusu Allaah hakuna chochote ambacho ni kigumu Kwake:

وَمَا خَلَقْتُ الْجِنَّ وَالْإِنسَ إِلَّا لِيَعْبُدُونِ

“Sikuumba majini na watu isipokuwa waniabudu.”[3]

Allaah (Subhaanah) si Mwenye kuhitajia chochote. Si Mwenye kuwahitajia viumbe. Yeye (Subhaanah) ndiye Tajiri na Yeye ndiye huwapa viumbe.

لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ ۖوَهُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ

“Hakuna chochote kinachofanana Naye – Naye ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona.”[4]

Njia ya kukata inapinga ufanano kwa Allaah (Subhaanah). Hakuna chochote kinachofanana Naye; si Malaika, Manabii, Mitume, mawalii wala kiumbe mwingine yeyote. Amejiita Mwenyewe kwamba ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona. Mwanzo mwa Aayah kuna Radd kwa Mushabbihah na mwishoni mwake kuna Radd kwa Mu´attwilah. Aayah imefahamisha kwamba kuthibitisha majina na sifa za Allaah hakupelekei kumfananisha na viumbe. Usikizi na uoni wa viumbe haufanani na usikizi na uoni wa Allaah (´Azza wa Jall).

[1] 42:11

[2] 36:82

[3] 51:56

[4] 42:11

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Mukhtaswarah ´alaal-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 46-47
  • Imechapishwa: 24/09/2019