Swali 29: Ni ipi hukumu ya mwenye kupeana zawadi vitu vya thamani kwa madai kwamba eti ni vya wale anaowaongoza kazini?

Jibu: Hili ni kosa na ni njia inayopelekea katika maovu mengi. Ni wajibu meneja asikubali zawadi. Zawadi hizo zinaweza kuwa na rushwa na njia inayopelekea kulegezeana na khiyana. Isipokuwa ikiwa kama ataipokea kwa ajili ya hospitali na kwa ajili ya maslahi ya hospitali. Isiwe kwa ajili ya maslahi yake mwenyewe na amweleze yule aliyempa kwamba zawadi aliyompa ni kwa ajili ya maslahi ya hospitali na kwamba hatobaki nayo yeye. Lililo salama zaidi ni yeye kuirudisha na wala asiipokee kwa ajili yake wala kwa ajili ya hospitali. Kwani kufanya hivo kunaweza kumpelekea akaichukua kwa ajili ya nafsi yake. Jengine ni kwamba anaweza kujengewa dhana mbaya. Huenda yule mtoa zawadi malengo yake ni kufanya ujasiri kwake na analenga kutaamiliwa bora zaidi kuliko wafanyakazi wengine. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wakati alipowatuma baadhi ya watu kwa ajili ya kukusanya zakaah mmoja akasema:

“Hii ni yenu na hii nyingine nimepewa zawadi.”

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamkemea kitendo hicho na akawatolea Khtubah watu kwa kusema:

“Ana nini mwanaume mmoja katika nyinyi ambaye tumempa kazi moja wapo miongoni mwa kazi za Allaah ambapo anasema kuwa hii ni yetu na hii nyingine amepewa zawadi yeye. Kwa nini asingelibaki nyumbani kwa baba yake au nyumbani kwa mama yake na akaona kama angepewa zawadi?”

Ameipokea Muslim katika “as-Swahiyh” yake.

Hadiyth hii ni dalili inayofahamisha kuwa lililo la wajibu kwa wafanyakazi wote wa serikali watekeleze vilivyo zile kazi walizopewa. Hana ruhusa ya kupokea zawadi kwa yale yanayohusiana na kazi yake. Akiipokea basi aiweke kwenye hazina ya waislamu na wala haijuzu akaipokea kwa ajili ya nafsi yake kwa sababu ya Hadiyth hii Swahiyh. Jengine ni kwa sababu ya njia inayopelekea katika shari na kutumia vibaya amana.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam Swalaat-il-Mariydhw, uk. 51-53
  • Imechapishwa: 16/10/2019