Haya ni baadhi ya yale niliyotaka kuyaorodhesha hapa. Lengo ni kujivutia na kujikumbusha mimi mwenyewe kwanza na ndugu zangu. Huenda tukaingiwa na hima. Huenda tukajibidisha katika kujifunza elimu. Huenda tukawa miongoni mwa wale wenye kuwapelekea elimu familia. Huenda tukawa miongoni mwa wale wenye kueneza elimu kati ya watu. Matokeo yake Allaah akazihuisha nyoyo za wale waliokufa.

Hakika watu leo wana haja kubwa kabisa ya elimu. Wamekuwa wengi wazungumzaji na wenye kujifunza, wenye kufundisha na kutenda wamekuwa wachache.

Wanafunzi! Enyi ambao mmezilazimu nafsi zenu na kujifunza elimu sahihi! Mnatakiwa kutambua kuwa elimu ni kitu kizito. Kwa sababu ni kitu kinatokamana na Qur-aan. Qur-aan ni neno zito ambalo Allaah ameliteremsha kwa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hivyo ni lazima kuwa na subira. Hakuna mwenye kuweza kuwa na subira juu ya elmu isipokuwa wanaume wa shoka. Hivyo wanafunzi wanatakiwa wawe na subira.

Watu wengi wanapenda kuhudhuria mihadhara ilio na maneno yenye kuathiri ambayo haina elimu wala athari. Bali ni maneno tu na ngano tupu: “Niliona, nilisikia na vicheko.” Upande mwingine hawawezi kuwa na subira juu ya elimu. Kinachonufaisha ni elimu.

Ndugu wapendwa! Tunatakiwa kupupia kujifunza elimu na tuzisubirishe nafsi zetu juu ya hilo. Tunatakiwa kufuata njia ya wale waliotangulia (Radhiya Allaahu ´anhum) katika hilo. Ninaapa ya kwamba Ummah hauwezi kunufaika isipokuwa kwa wanachuoni. Kuhusiana na wanafalsafa wao wanachojua ni kuzungumza tu na maneno yao ni ya matamanio. Maneno yao ni yenye kupendeza lakini hata hivyo hayaathiri. Maneno yao yanaathiri lakini hata hivyo hayazalishi matendo mema. Bali kinyume chake yanaweza kuzalisha matendo batili.

Ala ala wanafunzi! Jifunzeni elimu na muwe na subira juu ya hilo. Huenda Allaah (´Azza wa Jall) akatuwafikisha kuwa katika wale wenye kulingania Kwake kwa ujuzi.

Swalah na salaam zimwendee Muhammad, kizazi chake na Maswahabah zake.

  • Mhusika: Shaykh Sulaymaan bin Saliymillaah ar-Ruhayliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-´Ilm wa Wasaaailuh wa Thimaaruh
  • Imechapishwa: 22/10/2016